Monday, 15 August 2016

WASIOENDELEZA ARDHI WAZIUZE- LUKUVI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametoa miezi mitatu kwa watu wanaomiliki hatimiliki za ardhi, ambao wanashindwa kuyaendeleza maeneo yao, kuanza kuyauza kwa wananchi wanayoyahitaji.

Aidha, amesema watakaoshindwa kuyauza kwa kipindi cha muda huo aliotaja, atawafutia hati hizo na kuyataifisha mara moja.

Akizungumza jana, Dar es Saalam, katika mkutano na kampuni ya upimaji na upangaji wa ardhi, Lukuvi alisema kuna baadhi ya watu, ambao wana hatimiliki zaidi ya 1,000, huku wengine wakiwa wanakalia hatimiliki 700, bila kuyaendeleza maeneo husika kwa shughuli yeyote.

Alisema kwa watu watakaokiuka agizo hilo la kuuza hati hizo ataingilia kati kuanza kuyauza kwa wananchi, ambao wamekosa fursa ya kupata maeneo ya ardhi yaliyokaliwa na watu wasioyaendeleza.

"Hivi inafika wakati mtu anakalia hati za ardhi 700, huyo ni mtu mmoja tu anamiliki na kwamba, wapo wengine wanamiliki 1,000, bila kuyaendeleza. Imefikia wakati lazima tuyauze kwa lengo la kuwapatia usawa na Watanzania wengine, ambao wanayataka kuyaendeleza katika shughuli mbalimbali,"alisema.

Aliongeza kuwa nia ya serikali kwa sasa ni kuyaendeleza maeneo zaidi ya 20, ambayo yamekwishaiva kwa ajili ya kuwa miji na hivyo kinachotakiwa ni kuanda mkakati wa kupima na kupanga maeneo hayo kuwa rasmi.

Lukuvi alisema asilimia kubwa ya maeneo ya miji yote hapa nchini, hayajapimwa wala kupangwa, akitoa mfano kwa mji wa Kisarawe na Mkurunga kuwa, hayajapimwa huku wananchi wakiwa hawana hati miliki, hivyo serikali inaanza kasi ya mradi wa umilikishaji wa ardhi kwa Watanzania wanyonge.

Waziri huyo alizitaka kampuni binafsi za upimaji na upangaji ardhi, kuanza mradi mkubwa wa umilikishaji ardhi kwa wananchi kwa gharama nafuu na kuanza kuwashirikisha wananchi katika shughuli za upimaji na upangaji maeneo hayo nchi nzima.

"Nchi nzima kuna kampuni 58 za upimaji na 38 za upangaji, hivyo inaonyesha kabisa namna kulivyokuwa na changamoto ya mipango miji nchini na kwamba, kuna haja ya kuwashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu vya ardhi ili kutoa fursa za ajira za muda na za kudumu katika mradi huo wa upimaji ardhi na upangaji,"alisema. 

No comments:

Post a Comment