Thursday, 3 September 2015

WAPINZANI HAWANA SERA-MTOPA



Na Khadija Mussa, Ruangwa

MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Lindi, Ally Mtopa, amewataka wananchi kutowapigia kura wagombea wa upinzani kwa kuwa hawana sera wala malengo mazuri kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Badala yake amesema wagombea hao wanatangaza uroho wa madaraka ambao hauna tija kwao.

Pia, amesema wananchi hawana budi kuendelea kuichagua CCM kwa kuwa imetekeleza ahadi zake kwa vitendo, ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama vile barabara, hivyo kuwezesha kupitika kwa urahisi katika kipindi chote cha mwaka.

Akizungumza na wakazi wa Kata ya Mbekenyera wilayani hapa, jana, katika kampeni ya ubunge, aliwataka wananchi wasidanganyike na wapinzani kwa kuwa hawana nia ya kuwaetea maendeleo.

Alisema CCM ndicho chama pekee mkombozi kwao, hivyo hawana budi kuchagua viongozi kutoka katika Chama.

Mtopa alisema wananchi wasidanganyike kwani hakuna jambo la maendeleo, ambalo linaweza kuletwa na wapinzani kwa kuwa wengi wao ni watafuta fursa tu na si vinginevyo. Aliwataka wawe macho na wawakatae kwa kuwanyima kura siku itakapofika.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa, aliwaomba wakazi wote bila kujali itikadi zao za vyama wilayani hapa, kuhakikisha wanampigia kura yeye pamoja na wagombea wote wa CCM.

Majaliwa, ambaye anatetea nafasi hiyo, anaomba kuchaguwa kwa awamu ya pili akiwa na mtaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoitekeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo uboreshaji wa sekta ya elimu, maji, afya, miundombinu na mawasiliano.

Alisema anaomba kuchaguliwa kwa awamu nyingine ili waweze kuendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili, ambazo nyingi ameshazitafutia ufumbuzi ikiwemo ajira kwa vijana.

Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Lindi,Amiri Mkalipa alisema watahakikisha katika mkoa huo hakuna jimbo au kata itakayokwenda kwa wapinzani, hivyo aliwaomba vijana wote kuhakikisha wanahamasisha wenzao wa vyama vingine kuwapigia kura wagombea wa CCM.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, wakazi wa jimbo hilo walisema hawana sababu ya kutoichagua CCM kwani imeweza kuwaletea maendekeo makubwa, ambayo yamebadisha muelekeo wa maisha yao, likiwemo suala la elimu ambapo kwa sasa limepewa kipaumbele tofauti na miaka ya nyuma.

Pia, walisema wameridhishwa na utendaji wa mgombea wa urais wa CCM, Dk. John Magufuli na mgombea ubunge, Majaliwa, kutokana na jitihada kubwa za kuboresha maendeleo alizozifanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Naye Katibu wa CCM wa mkoa wa Lindi, Adelina Defi alisema mkoa umejipanga kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika nafasi zote, hivyo viongozi wa mkoa watafanya ziara katika majimbo na kata zote ili kuhakikisha malengo yao yanafanikiwa.

Aliwasisitizia wakazi wa jimbo la Ruangwa kutotoa kura zao kwa wapinzani kwa sababu hawana dhamira ya kuwaletea maendeleo, badala yake wachague wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.

No comments:

Post a Comment