Thursday, 3 September 2015
MANGULA AFICHUA SIRI YA UKAWA
NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, amesema kuna baadhi ya wanasiasa wameanza kutengeneza mazingira ya vurugu na kuhatarisha usalama wa nchi.
Amesema kauli za baadhi ya wagombea kuwataka wapigakura wasiondoke kwenye vituo baada ya kutimiza haki hiyo kisheria ni dalili mbaya.
Mzee Mangula amesema kila chama kinachoshiriki uchaguzi kimepewa fursa ya kuweka mawakala ili kuhakikisha hakuna mizengwe na ambao huteuliwa na vyama husika.
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa kundi la UKAWA wamekuwa wakihamasisha wafuasi wao kuhakikisha wanakuwepo kwenye vituo vya kupigiakura baada ya kupiga kura ili kulinda zisiibiwe.
Hata hivyo, mara kadhaa wamejibiwa kuwa kamwe CCM na wagombea wake haina kawaida ya kuiba kura na kwamba, ushindi wake miaka yote umekuwa ukipatikana kwa njia halali kutokana na kuwa na wanachama na wafuasi wengi.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa CCM, viongozi wa dini, wazee wa kimila (machifu), wazee maarufu jijini Mbeya, pamoja na makada wa CCM katika ukumbi wa Royal Tughimbe, ulioko eneo la Mafiat mjini hapa.
Alisema nchi nyingi duniani huingia katika machafuko wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu na kwamba, dhana ya kuwaamrisha wananchi kulinda kura haiwezekani kwa kuwa mlinzi wa kura ni wakala wa chama na si raia ama kikundi cha watu ama jeshi.
"Kitendo cha wanasiasa kuanza kuwaeleza wananchi kuwa wakipigakura wasiondoke kwenye vituo vya kura ni dalili za kutengeneza mazingira ya vurugu. Na wakifanya hivi watawafanya wapigakura wengine kushindwa kwenda kupiga kura kwa kuhofia vurugu na hiki ndicho wanachokitaka hawa," alisema Mangula.
Aliongeza kuwa CCM inawashukuru wananchi wa jiji la Mbeya na mkoa mzima kwa jumla, kwa jinsi walimvyompa mapokezi makubwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama, Dk. John Magufuli, hali inayoashiria kuwa atapata kura za kishindo.
Mangula aliwataka wananchi wa Jiji la Mbeya kumuunga mkono mgombea ubunge wa CCM, Kapteni Mstaafu Sambwee Shitambala, ili aweze kushinda kwa kishindo.
Kwa mujibu wa Mangula, wananchi wa jiji la Mbeya hawatakiwi kuyarudia makosa waliyoyafanya mwaka 2010, kwa kumchagua Joseph Mbilinyi, ambaye ameshindwa kuleta maendeleo zaidi ya vurugu.
"Hivi mnajisikiaje pale mnapokuwa na mbunge aina ya Sugu. Hana makosa lakini hawezi kuwa taswira ya jiji la Mbeya ambayo ina hadhi yake. Tunatakiwa kumpigania Shitambala ili aweze kuibuka kidedea na kulirudisha jimbo hili ndani ya CCM. Kamwe tusikubali kurudia makosa ya mwaka 2010, kwani itakuwa ni kosa kubwa," alisema Mangula na kupigiwa kofi.
Aliongeza kuwa mchakato wa kuwapata viongozi watakaopeperusha bendera ya CCM, ukiwemo ule wa kumpata mgombea urais, uliendeshwa kwa demokrasia na wote walioshinda wana uwezo na dhamira ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
"Demokrasia ilitumika kwa majina yote ya wana-CCM waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuipeperusha bendera ya Chama kwenye nafasi ya urais, kwa majina yote kujadiliwa kisha uamuzi kufanywa na wanachama," alisema Mangula.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment