Thursday, 3 September 2015
SLAA AWAVURUGA UKAWA, MAANDAMANO YA KUMKATAA LOWASSA YATUA ARUSHA, WANACHAMA 200 WACHOMA KADI
Na Waandishi Wetu
BAADA ya juzi wafuasi na wanachama wa CHADEMA katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Dar es Salaam, kuandamana wakipinga Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais wa chama hicho, kwa kuwa si msafi, maandamano hayo yametua jijini Arusha.
Maandamano hayo yametajwa kuwa ni kuunga mkono uozo ulioibuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ambaye bila kumung’unya maneno alisema Lowassa hastahili kugombea wala kuchaguliuwa kuwa rais wa nchi kwa kuwa si mwadilifu na ana kashfa nyingi.
Hata hivyo, tangu Dk. Slaa kuibua uozo huo na tuhuma nyingi dhidi ya Lowassa na viongozi wengine wa CHADEMA, yakiwemo makapi yaliyohama na mwanasiasa huyo kutoka CCM, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kufunika mambo hayo.
Tayari Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI Taifa, James Mbatia, amejitoa muhanga na kujaribu kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Dk. Slaa, lakini baadhi ya wasomi na wanasiasa wamesema hajafanikiwa kutokana na kutoa majibu mepesi katika maswali magumu.
Mwingine aliyetumiwa kujibu hoja hizo ni aliyekuwa mke wa Dk. Slaa, Rose Kamili, ambaye jana aliandaliwa mkutano na waandishi wa habari na kumtuhumu mwanasiasa huyo kuwa si mwadilifu kwa kuwa ametelekeza familia na ni mtu asiyeweza kudhibiti hasira zake.
Katika maandamano yaliyofanyika jijini Arusha jana, wafuasi na wanachama wa CHADEMA wameendelea kusisitiza wakiwataka viongozi kumuondoa Lowassa katika kuwania nafasi hiyo huku wengine wakiamua kuhamia ACT Wazalendo na CCM.
Zaidi ya wanachama 200 walichana na wengine kuchoma moto kadi za CHADEMA jana, kutokana na kufichuka kwa siri kuhusiana na namna Lowassa alivyojiunga ndani ya chama hicho.
Huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, wafuasi hao walianza kukusanyika maeneo ya kituo kidogo cha mabasi na wengine eneo la Florida na kuishia Ofisi za ACT zilizoko Levolosi.
Waandamanaji hao wengi wakiwa vijana, walisema hawakubaliani na ubabaishaji unaoendelea ndani ya CHADEMA na kwamba, wameamua kujiengua ili kukiacha chama hicho mikononi mwa Lowassa na makapi yaliyotoka CCM.
“Tumechoshwa na ubabaishaji unaofanywa kwa maslahi ya wachache, tumejitoa kwa hali na mali kuhakikisha CHADEMA kinakuwa chama imara, lakini mchezo huu mchafu hatuwezi kuvumilia, tunajiengua na kuyaacha makapi yafanye yatakavyo,” walisikika vijana hao waliokuwa wakiimba nyimbo za kuwashutumu viongozi wa vyama hivyo.
Mmoja wa waandamanaji hao, Hassan Juma, alisema amekuwa mwanachama mwaminifu wa CHADEMA tangu mwaka 2005, lakini sasa ameamua kukihama kutokana na kugubikwa na tuhuma za ufasadi ambazo ndio ilikuwa ajenda yake.
“Nilivutiwa na CHADEMA kutokana na sera ya kupambana na ufisadi, lakini kwa sasa haipo kwa sababu tumepokea watu wenye tuhuma za ufisaidi…tumebaini tulikuwa tunatumiwa kwa malengo binafsi ya watu. Kwa hiyari yangu nimejitoa na kuingia ACT,” alisema Juma.
Naye mwanachama wa NCCR-Mageuzi aliyejitambulisha kwa jina la Eliphas, alisema viongozi wakuu wa UKAWA wamekuwa na tabia ya kuwaburuza wanachama kwa kufanya uamuzi bila kuwashirikisha kwa maslahi ya wachache.
Alisema siri zilizoibuliwa na Dk. Slaa ni nzito, hivyo kwa watu makini na wanaojitambua, vyama vinavyounda UKAWA havistahili kushabikiwa tena kwa kuwa vimejaa usanii.
“Hatuwezi tukalaani ufisadi na mafisadi waliokua CCM halafu ukija kwetu tunaukumbatia. Tuliondoka CCM kwa sababu ya ufisadi na mizengwe na sasa tunaona viongozi wetu wamekaribisha na kuyakumbatia matatizo yale yale. Hatukubaliani na hilo na ndio maana tunaondoka na wenzetu wengine wapo njiani kutufuata,” alisisitiza Eliphas huku akiichoma moto kadi yake ya NCCR-Mageuzi.
Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alipoulizwa alisema kuwa vijana hao wametumwa kuandamana na kwamba, wana taarifa kuwa ni mkakati wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika hoteli
ya Regency, Msasani, Dar es Salaam, Rose alisema kitendo cha Dk. Slaa
kusema kuwa walikuwa wakila mihogo muda wote kuhakikisha kuwa CHADEMA
inaendelea ni uongo.
Alisema hawakuwahi kula mihogo kama alivyodai Slaa kwenye hotuba yake,
lakini hata hivyo ameonyesha dharau kwa Watanzania kwa sababu mihogo
ni chakula kinachotumiwa na Watanzania wengi.
Aidha, alidai kuwa kitendo cha Dk. Slaa kumnyooshea kidole mgombea
urais wa CHADEMA na UKAWA, Edward Lowassa, si cha kiungwana kwa sababu
Lowassa ndiye aliyemshauri Dk. Slaa kuhamia CHADEMA baada ya
kukorofishana na CCM.
Alimshutumu Dk. Slaa kuwa si mwadilifu kwa sababu alijiuzulu utumishi
kanisani kutokana na hasira kali, ambazo zilimsukuma kumshikia mtu
bastola, huku pia akidai Slaa alihusishwa na tuhuma mbalimbali wakati
akiwa mtumishi wa Kanisa Katoliki na kusababisha kujiuzulu.
Rose aliendelea kusema kuwa Dk. Slaa si mkamilifu kwa sababu mpaka
sasa anazini bila kuwa na ndoa takatifu, hivyo hapaswi kujitokeza na
kuwakosoa wengine juu ya uadilifu wa maisha na utendaji.
Akiwa sambamba na maofisa wa CHADEMA, aliwaambia waandishi wa habari
kuwa Dk. Slaa anatakiwa kupuuzwa na kwamba Watanzania waendelee
kuyaunga mkono malengo ya UKAWA kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
Baada ya kumaliza mkutano huo, Rose alisikika akiomba kupelekwa aliko
wakala wa huduma ya M-PESA, ili akatoe fedha ambapo aliondoka na gari
iliyokuwa na bendera ya CHADEMA kisha alirudi kwenye hoteli hiyo baada
ya dakika zisizozidi kumi.
Aliporudi alipanda mpaka ghorofa ya kwanza ya hoteli hiyo alikokuwa
amewaacha baadhi ya wanahabari na maofisa wa CHADEMA, kisha kuwataka
wasiohusika kutoka nje, jambo lililoashiria kutoa nafasi ya kugawana
fedha ambazo zilikuwa zimeandaliwa baada ya kufanikiwa shughuli hiyo.
Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye hoteli hiyo na kusikia yaliyoendelea
kwenye ukumbi wa mikutano kati ya Rose na waandishi wa habari,
walisikika wakisema baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani wamekusudia
kuiharibu nchi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Walisema ni ajabu mwanamke huyo kujitokeza wakati huu na kutoa hoja
zisizo na mashiko ambazo zilidhamiria kupinga hotuba ya mtalaka wake,
ambaye alikuwa na nyaraka za uthibitisho wa alichokuwa akikisema
kwenye hotuba yake.
Mpaka Uhuru linaondoka kwenye viunga vya hoteli hiyo saa 12.49, jopo
hilo lililokuwa limeongozwa na Rose lilikuwa halijatoka kwenye ukumbi.
Dovutwa: Mbowe amekiua rasmi chama
Naye mgombea urais wa UPDP, Fahmi Dovutwa, amesema Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, amekimaliza chama hicho baada ya kumkaribisha Lowassa.
Amesema CHADEMA kwa sasa kimekuwa na matatizo makubwa ambayo yanaendelea kuota mizizi huku makada wake waliokuwa mstari wa mbele kukijenga chama hicho wakirudi nyuma na kuyaacha makapi yaliyotoka CCM yakishika usukani.
Duvutwa amesema kwa hali ilivyo, mwisho wa CHADEMA itakuwa Oktoba 25, mwaka huu, na kwamba, baada ya hapo kitakachofuata ni kujiandaa kusajili chama kipya ambacho kitakuwa na sera kama za awali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dovutwa aliwataka viongozi wa CHADEMA kukubali kukosolewa na kwamba, Dk. Slaa amesema anayoyafahamu hivyo wajifunze.
“CHADEMA ndio kinaelekea ukingoni kwa sababu ya kupoteza misingi na mwelekeo wake na viongozi wake hawapendi kukosolewa,” alisema.
PROFESA KAYUMBO AKUNWA NA DK. SLAA
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hosea Kayumbo, alisema amefurahishwa na hutuba iliyotolewa na Dk. Slaa, ambaye alimtaka Lowassa kujisafisha mwenyewe dhidi ya tuhuma za ufisadi.
Alisema tuhuma hizo ni pamoja na ya Richmond, ilisayosababisha ajiuzulu uwaziri mkuu, mwaka 2008.
Profesa Kayumbo alisema CHADEMA wamemchukua Lowassa na kudai ni msafi wakati si kweli.
Alisema Dk. Slaa alidai kuwa mgombea urais wa CHADEMA na Waziri Mkuu Mstaafu, Frediric Sumaye walihusika kwa kashfa mbalimbali.
“Dk. Slaa anadai ana ushahidi. Hilo linaweza kuwachafua hata viongozi wengine,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment