Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Amon Anastaz Mpanju akisalimia wakazi wa Iwawa kwenye mkutano wa Kampeni za CCM uliofanyika stendi ya Mabehewani Makete |
Mgombea wa Urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa kijiji cha Kikondo kata ya Ilungu Mbeya vijijini akiwa njiani kuelekea mkoa wa Njombe |
Umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo |
Mgombea wa Urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa kijiji cha Ujuni Makete mkoani Njombe . |
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mhe. Wiliam Lukuvi akihutubia wakazi wa njombe mjini kwenye uwanaja wa Saba Saba |
Mgombea wa Urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. John Pombe Magufuli akimkabidhi mgombea Ubunge wa Jimbo la Wanging'ombe Eng.Gerson Lwenge ilani ya uchaguzi ya CCM |
NA SELINA WILSON, NJOMBE
MGOMBEA Urais wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akipata ridhaa ya wananchi, ataendesha
nchi kisayansi na hatawapa nafasi mafisadi na wala rushwa wafanye watakavyo.
Amesema anajua mafisadi
hawatampigia kura, lakini anawaomba wananchi nyingi za kutosha ili aweze kuwa
Rais ashughulike nao kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania.
Dk. Magufuli alisema hayo
jana kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa wa Njombe kwenye
mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka
huu.
Alisema anatambua kero za
wananchi kuwa huduma muhimu kama vile barabara, elimu, maji, afya na uchumi na kwamba,
atahakikisha anazifikisha kwa wananchi kwa kuwa fedha zipo isipokuwa kuna watu
wachache wanaofanya ufisadi.
“Kuna watu wanasema
wanataka kuing’oa CCM madarakani, lakini niwape wosia kwamba kitanda chako
kikiwa na kunguni huwezi kukitupa kitanda na badala yake unatakiwa kuwatafuta
kunguni watatu waliopo unawaua unaendelea kulala na mkeo,”alisema.
Dk. Magufuli aliwataka
wananchi wasiiadhibu CCM kwa ajili ya mafisadi na wala rushwa wachache ambao
waliposikia ameteuliwa kuwania urais wamekimbia, hivyo ataendelea kusafisha na
waliopo kama wanatakakubaki salama watubu na waendane na kasi ya kuleta
maendeleo.
Aliwaambia wananchi kuwa
atazingatia maslahi ya watu wote wakiwemo wafanyakazi, wafanyabiashara,
wanafunzi, wakulima na watu wa makundi mengine.
“Kwanza nataka niwaambie
mimi ni mwalimu, mke wangu ni mwalimu. Kwa hiyo kwa walimu mimi ni shemeji yenu
kotekote,”alisema.
Dk. Magufuli alisema
atafanya kazi kwa karibu na waandishi wa habari kutokana na kazi kubwa
wanayofanya ya kuhabarisha wananchi.
“Ndugu zangu waandishi wa
habari mnafanya kazi kubwa na ahadi yangu kwenu nikishinda uchaguzi nikiwa
Rais nawaahidi nitakuwa pamoja nanyi,”alisema.
UVAMIZI VITUO VYA POLISI
Alionyeshwa kukerwa na
kitendo cha uvamizi katika vituo vya polisi na kueleza akiingia Ikulu
atahakikisha anaboresha maslahi ya polisi ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
“Askari polisi
wanatulinda, nataka wafanye kazi zao vizuri. Wasikose hela ya chakula ili
wasilale vituoni wakaja watu wakachukua SMG.
Nazungumza kwa upole
nataka jeshi liheshimike, watu wanachukua silaha wakati na polisi wana silaha.
“Jambazi
akija unatakiwa kumuwasha kwa kuwa yeye naye anakuja kukuwasha.
Inawezekana maneno yangu ni makali, lakini ndio hivyo,” alisisitiza.
Dk. Magufuli alisema
askari wanalinda benki wanatoka hawana hela ya kununua mboga na ndio maana anakuja
jambazi askari yuko na silaha anaogopa hata kumpiga risasi kwa kuogopa
kushitakiwa.
“Wakati wangu jambazi
akija chapa chapa, nataka watu wafanye kazi, watu wafungue maduka usiku na afungue
pale anapotaka,”alisema.
Alisema kinachotakiwa ni
kuzingatia sheria lakini Jeshi la Polisi linapaswa kuheshimika.
Pia Dk. Magufuli
alimpongeza Rais Kikwete kwa kuanzisha mkoa mpya wa Njombe na ilikuwa ni mapenzi
makubwa ya CCM kusogeza maendeleo karibu na wananchi.
Alisema Rais Kikwete
ameshaanzisha mkoa na kinachotakiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na
Njombe inajengwa na kufunguka kibiashara.
Dk. Magufuli alimnadi
mgombea ubunge wa Wanging`ombe, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge na
kuwaeleza wananchi kwamba ni mchapakazi hodari.
“Nimefanya kazi na Lwenge
namfahamu. Naomba mniletee ili nifanye kazi naye akamilishe ujenzi wa barabara kutoka
Njombe, Makete hadi Mbeya ili wafanyabiashara waweze kusafirisha mazao yao na
wapate maendeleo,”alisema.
Akiwa Makete alimnadi, Dk.
Noman Sigala na kuwaomba wananchi wamchague ili apate mtu wa kufanya naye kazi
na kuibadilisha Makete ambayo bado ipo nyuma kimaendeleo.
MANGULA AWAKOSHA WALIMU
Katika hatua nyingine,
Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa (Bara), Philip Mangula, akizungumza katika Uwanja
wa Sabasaba mjini Njombe, alisema Rais Jakaya Kikwete anaondoka madarakani na
kuwaachia mwalimu mwenzao.
“Walimu mpoo. Nakumbuka
Rais Kikwete akiwa kwenye sherehe za walimu jijini Mwanza kwenye sherehe za
Siku ya Wafanyakazi Mei mosi, mwaka huu, walimu mlimtania mkaamuliza ‘shemeji unatuachaje’,”
alisema.
Mangula alisema sasa Rais
Kikwete, amewapa majibu kwamba anawaachia mwalimu mwenzeo.
Alisema CCM imemleta Dk.
Magufuli ambaye ni mwalimu aliyesoma masomo ya hesabu na sayansi na anayeaminika
kwa kuwa mchapa kazi.
AWANANGA WAZUSHI
Katika hatua nyingine, Dk.
Magufuli aliwazodoa waliomzushia kwenye mitandao ya jamii kwamba amelazwa ICU
na kwamba, taarifa hizo hazina ukweli.
Alisema uzushi huo hauna
tija kwa kuwa amekamilisha mikutano yake Mbeya na amepokelewa na wananchi wa
vyama vyote, hivyo wenye lengo kumchafua wameshindwa.
Mgombea huyo aliesema ni
mzima wa afya na kilichotokea ni kwamba alikwenda Hospitali ya Rufani ya Mkoa
wa Mbeya kumuona Meya mstaafu wa Jiji la Mbeya, Atanad Kapunga, aliyelazwa
baada ya kujeruhiwa ajalini.
Dk.Magufuli alisema hayo
jana wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo baada ya kuhitimisha ziara
yake, ambapo aliwashukuru kwa mapokezi na mikutano ya kampeni kwa mafanikio
makubwa.
Alisema ameshangazwa na
taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba ameugua na amelazwa
ICU.
“Nawapa pole viongozi na
wananchi kwa tukio la ajali iliyotokea siku nne zilizopita wakati viongozi
walipokuja kunipokea nikitoka Nzoka. Gari moja alilopanda meya huyo likapata
ajali.
Katika ajali hiyo
mwanachama mmoja wa CCM alifariki dunia na wengine watatu walijeruhiwa.
Niliacha shughuli zangu nikaenda hospitali kumuona meya na hali yake inaendelea
vizuri,"alisema.
Dk.Magufuli alisema kwa
ubinadamu wa kawaida na kwa watu wanaomjua Mungu ilikuwa ni lazima kwenda
kumuona mgonjwa huyo.
Alisema yeye ni mzima wa
afya na anaendelea kupiga kazi na lengo lake ni kuwaletea maendeleo Watanzania
na kuleta mabadiliko ya kweli.
Dk.Magufuli akiwatubia
wananchi wa jimbo la Makete katika
uwanja wa Iwawa aliwaahidi wananchi kwamba serikali yake itajenga
barabara ya lami ya Njombe/Makete hadi Mbeya.
Aliwaomba wananchi
wamchague kwa kura nyingi ili aweze kutekeleza azma yake ya kuwaletea Watanzania
maendeleo bila kujali itikadi zao za vyama.
No comments:
Post a Comment