NA WAANDISHI WETU
MGOMBEA urais wa CHADEMA
na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward
Lowassa, jana alishindwa kuhimili mikiki ya kampeni, hivyo kutumia dakika 11
kuhutubia wafuasi wao katika mkutano wake wa uzinduzi wa kampeni.
Lowassa ambaye alipanda
jukwaani saa 11:40 jioni alishuka saa 11:52 na muda mwingi tangu kuingia katika
Viwanja vya Jangwani mahali walipozindulia kampeni alionekana mnyonge huku
akitembea kwa kuburuza miguu hali iliyozua hofu kwa wananchi.
Wakati akizindua kampeni
zake za urais wiki iliyopita, mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, alitumia
dakika 58.
Aidha, aliwasikitisha
zaidi wafuasi wake kushindwa kutumia muda wake kunadi ilani ya chama chao na
badala yake aliwataka wananchi wakavisome katika tovuti ya chama chao ambayo
hata hivyo alishindwa kuitamka kwa ufasaha na hata wananchi walipomuomba
kurudia kuitaja hakufanya hivyo.
CHADEMA na UKAWA ambao
walizindua kampeni zao, watu waliofika walilalamika kukosekana kwa utaratibu.
Pia, licha ya kushindwa
kuzungumzia mipango ya Ilani ya chama chake, Lowassa alizidisha machungu kwa
wakulima baada ya kusisitiza serikali yake atakayoiunda itaendelea kukopa mazao
yao.
Alisema wataendelea kukopa
mazao ya wakulima na kulipa kwa riba, kitendo ambacho serikali ya CCM kupitia mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli,
kusisitiza kuwa hakitakuwepo.
Katika mipango ya
utekelezaji wa ilani ya CCM, Dk Magufuli, alisema suala ya wakulima kukopwa
mazao yao halitakuwepo.
Kupitia serikali
itakayoundwa na CCM, mkulima atalipwa fedha zake kwa wakati na kwa bei nzuri.
Licha ya kupeleka kilio
kwa wakulima, Lowassa alionyesha wazi kuwa serikali yake itaingilia uhuru wa
mahakama baada ya kutangaza kuwatoa gerezani viongozi wa kundi la Uamsho
wanaoshikiliwa kwa tuhuma za uchochezi.
Kesi dhidi ya viongozi hao
tayari iko mahakamani, muhimili ambao huendesha mambo yake kwa misingi ya haki
pasipo kuingiliwa na mtu au serikali.
Katika hali iliyoonyesha
kuwa Lowassa na chama chake hawakujipanga kuwaelezea wananchi namna gani
watavyowasaidia, alisema serikali itamtoa gerezani mwanamuziki Nguza Viking Babu
Seya’ na mwanawe Johnson Nguza ‘Papi Kocha na ‘kumrejesha duniani’ aliyekuwa
Gavana wa Benki Kuu (BoT), marehemu Daudi Balali. Balali alifariki dunia Mei
20, 2008 nchini Marekani.
“Nimesikia nitamtoa Babu
Seya na kumrejesha Balali”, alisema
Lowassa.
Kauli hiyo ilizua maswali
kutoka kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza, waliosikika wakidai kuwa
mgombea huyo anawafanyia maigizo ya kisiasa badala ya kuwaelezea namna
atakavyoweza kutatua kero za wananchi.
“Sasa hii kali ya kumfufua
marehemu, hivi Watanzania tuna mahitaji hayo ya Balali na Babu Seya. Hatuwezi
tukaendeshwa na serikali ya maigizo,” alisema mmoja ya wananchi hao.
Wakati Lowassa akiendelea
na hotuba yake, watu walianza kuondoka kana kwamba mkutano wake ulikuwa
umemalizika.
Wananchi hao walisema, uwezo wa Lowassa kuzungumza na
kueleweka bado mdogo, huku wakidai udhaifu wa afya yake unachangia.
Mara kadhaa mgombea huyo
alijikuta akikumbushwa na baadhi ya maofisa wa chama chake kwa kunong’onezwa na
kupewa vijikaratasi kutoka meza kuu baada ya
kuonekana kugusia baadhi ya masuala ambayo yameahidiwa katika Ilani ya
CCM.
Kwa mujibu wa Lowassa
miongoni mwa vitu atakavyofanya ni kuboresha hospitali na ujenzi wa reli ya kati,
jambo ambalo limeshatiliwa mkazo na CCM katika utekelezaji wake.
SUMAYE NAYE
Kwa upande wake, Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alijitosa kumtetea Lowassa ilhali alipotangaza kuomba ridhaa ya CCM awanie
urais, ndiye aliyetamka hawezi kumuunga mkono kwa kuwa ni mgonjwa na hayuko
tayari nchi iongozwe na rais asiye na afya njema iwapo CCM ingemteua.
Katika hali ya kushangaza
Sumaye ambaye ndiye aliyeeleza juu ya hofu ya afya ya Lowassa na hatima ya
urais, jana aliendelea kukiri kuwa Lowassa ni mgonjwa, lakini akimtetea kuwa
atatibiwa Ikulu akiwa rais.
Sumaye alidai Lowassa kuwa
mgonjwa si hoja kwa kuwa marais hutibiwa nje ya nchi wakiwa madarakani, hivyo
achaguliwe pamoja na hali yake kutokuwa nzuri kwa kuwa atatibiwa akiwa Ikulu.
WAFUASI WAHOJI
Wafuasi wa vyama hivyo
walisikitishwa zaidi na hali ya mgombea wao kushindwa kusimama na kuhutubia kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa
mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.
“Kwa kweli hali ya mgombea
wetu ni mbaya afya sio nzuri anaumwa na
amechoka tuombe mungu amtie nguvu asije kudondoka maana hata kuinua miguu
hawezi lakini tupo pamoja naye,” alisema.
Licha ya dosari hiyo,
walilamikia kukaa muda mrefu katika viwanja hivyo bila kuwepo kwa utaratibu na
viongozi wao kufika jioni huku wakiwa hawana sera inayoeleweka ya kile
walichokitaja kuwa matumaini
wanayoyasema.
VIBAKA WAIBA, POMBE NJE NJE
Katika hatua nyingine
mkutano huo ulikuwa na vurugu nyingi, hali iliyosababisha kinamama kupoteza
watoto.
Aidha vurugu hizo
zilisababisha watu waibiwe simu na kufikia hatua ya kuomba uongozi uliopo mbele
kutoa msaada ambapo hata matangazo
yalipotolewa hakuna aliyepata mali yake.
Vurugu hizo zilisababisha
baadhi ya wafuasi hao waliokuwepo katika mkutano kurushiwa chupa za maji.
Kamera za gazeti hili pia
zilifanikiwa kunasa matukio ya unywaji pombe na watoto wadogo waliokuwa
wamevalishwa nguo za CHADEMA, lakini walioonekana kana kwamba walilazimishwa.
Hali ya usalama ilikuwa
mbaya kiasi cha watu mbalimbali kupoteza mali zao zikiwemo simu na mikoba kwa
kinamama.
DK. SLAA, PROF. LIPUMBA WAYEYUKA
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chama cha CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
wameendelea kukacha hafla zinazomhusisha Lowassa kugombea urais.
Wanasiasa hao
hawakuonekana katika kampeni za CHADEMA na UKAWA kama ilivyokuwa ikienezwa na
baadhi ya viongozi wa umoja huo ambao walitamba kuwa wangekuwa nao.
Dk. Slaa ambaye alijiuzulu
baada ya Mbowe kumuingiza Lowassa ndani ya chama hicho hajulikani aliko mpaka
sasa.
Aidha viongozi wa CHADEMA
walishindwa kumzungumzia mwanasiasa huyo wala wale wa CUF kuzungumzia aliko
Profesa Lipumba.
VIONGOZI WA
DINI
Viongozi wa dini waliohudhuria na kuhudumu kwenye uzinduzi
huo, walionyesha dhahiri kununuliwa kutokana na sala zao kujaa vijembe, maneno
ya dharau na kuyaelekeza kwa viongozi wa chama tawala (CCM) na serikali.
Hali hiyo iliwashangaza wananchi ambao si wafuasi wa vyama
hivyo vinavyounda Ukawa, waliofika kwenye viwanja hivyo kusikiliza ilani ambayo
ilisemekana ingetolewa, ambapo walisema sala imefanyiwa mzaha.
“Hawa wanaigiza, sala gani ile sasa? Wanacheza na Mungu hawa!
Utamwombeaje mwenzako ubaya wa namna hiyo kisa tuu hayuko pamoja na
unachokiamini? Lazima watakuwa wamelipwa, inashangaza sana haya ni maigizo,”
walisema.
Katika sala hizo zilizotolewa na viongozi wa dini ya Kiislamu
na Kikristo ambayo kwa niaba, ilitolewa na kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephat Gwajima, zilikuwa na maneno ya kejeli yaliyoonesha ni ya
kipambe.
Mojawapo wa maneno hayo ni kuombea watu wasio pamoja na vyama
hivyo hasa Chadema kuwa wapate saratani ya damu na ugonjwa wa viziba mkojo ili
UKAWA iendelee na harakati zake za kuelekea ikulu - maneno ambayo yaliwaacha
watu midomo wazi.
POLEPOLE AMNANGA
Akizungumza juzi usiku
kupitia kipindi cha Mada Moto cha kituo cha televisheni cha Channel Ten,
aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polelepole,
aliendelea kusisitiza kuwa uadilifu wa Lowassa unatia shaka na kwamba,
hastahili kuwa kiongozi wa taifa hili.
Polepole alisema kuwa,
Tanzania inastahili kuongozwa na rais muadilifu asiyekuwa na makandokando ya
‘uchafu’ unaotokana na utumishi wake kwa umma.
Alisema pamoja na hayo,
Watanzania wanapaswa kuwa mikononi mwa rais aliyeingia kwa siasa za maendeleo
na sio anayeng’ang’ana kuingia madarakani kwa kutumia siasa za nguvu.
“Hawa ni watu wawili
tofauti, huyu wa kwanza (wa siasa za maendeleo) anafanya siasa zake kwa nia ya
kuwanufaisha wengi, lakini huyu wa pili anafanya hivyo kwa manufaa yake na watu
waliomzunguka,” alisema.
CHADEMA BUNDA
Aliyekuwa
mshindi wa kwanza katika kura za maoni za ubunge wa CHADEMA kwenye Jimbo la
Bunda Mjini, Pius Masuruli ambaye nafasi yake alipewa Ester Bulaya, amekihama
chama hicho na kujiunga na CCM.
Ester
alikuwa mbunge wa viti Maalumu (UVCCM) kupitia Vijana mkoani Mara ambapo
alihama CCM na kujiunga CHADEMA.
Mbali
na Masuruli, wengine waliokihama chama hicho ni pamoja na aliyekuwa Katibu
Mwenezi wa jimbo hilo, Emmanuel Malibwa
na walinzi waliorudisha kadi na kujiunga na CCM, juzi, kwenye mkutano wa
uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa CCM, Stephen Wassira.
Uzunduzi
huo ulifanyika katika Viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Bunda na kuhudhuriwa
na mamia ya wananchi.
Alisema
ameamua kuhama CHADEMA kwa sababu ni cha ubinafsi, majungu na ni cha ukanda,
hivyo anakiunga mkono Chama na wagombea wake akiwemo Wassira.
Masuruli
alisema chama hicho kimeshindwa kutambua mchango alioufanya na kibaya zaidi, uongozi wa juu
ulikata jina lake wakati ndiye aliyekuwa ameongoza katika kura za maoni na
alitangaza rasmi kumuunga mkono mgombea wa CCM.
Kwa
upande wake, Malibwa alisema mbinu walizokuwa wanatumia kukijenga chama hicho katika Wilaya ya Bunda
ndizo watakazotumia kukiua na kuijenga CCM.
Wassira
alisema viongozi hao wa CHADEMA wamechukua uamuzi sahihi kuihama na kuhamia
katika chama makini cha CCM na kwamba, kumchukua Ester ni sawa kutwaa kapi
ambalo haliwezi kushinda katika jimbo hilo.
VIJANA NA VURUGU
USIKU wa kuamkia jana,
vikundi vya vijana wanaosemekana kuwa wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakizunguka
kwenye kaya za maeneo mbalimbali Dar es Salaam, kuwashurutisha watu kuhudhuria
uzinduzi huo.
Kitendo hicho
kilisababisha usumbufu kwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo yakiwemo ya Gongo la
Mboto na Chanika katika Manispaa ya Ilala kutokana na kelele na vurugu
zilizofanywa na vijana hao miongoni mwao walikuwa wamelewa.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti, wakazi hao walisema vijana wengi wanaoshabikia chama hicho hawajielewi
kutokana na kufuata mkumbo na kusahau wajibu kama raia kwa taifa lao, ikiwemo
kudumisha amani ina utulivu.
Walisema vijana wanatumiwa
vibaya na wanasiasa wenye uchu wa madaraka na wakipewa fedha kidogo wanatumika
kama ngazi ya wanasiasa husika kutimiza azma yao.
Mmoja wa wafanyabiashara
eneo la Pugu Stesheni, Idd Masoud, alisema alilazimika kufunga duka mapema
kuhofia kuvamiwa na vijana hao waliokuwa wametawanyika maeneo mbalimbali
wakiimba na kupiga kelele kwenye makazi ya watu.
Alivitaka vyombo vya
usalama kuendelea kutimiza wajibu ili kudhibiti vikundi vinavyotishia usalama
wa raia.
No comments:
Post a Comment