WANANCHI
wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mikutano kama hii hutumiwa na wagombea wa nafasi ya urais kunadi sera na ilani
ya vyama vyao.
Na John
Kiroboto
KIPINDI
hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu nchini kinashuhudia watu wengi wakijitokeza kwa
njia mbalimbali kuzungumza kwa kisingizio cha kutoa mchango wao katika
kuhakikisha uchaguzi unafanyikka kwa amani, uhuru, utulivu na haki.
Makundi
yanayojitokeza ni wanasiasa wenyewe ambao ndio wanaowania kuchaguliwa, tume za
uchaguzi ambazo ndizo zenye dhamana ya kusimamia uchaguzi, Jeshi la Polisi
ambalo linatazamiwa kulinda amani na utulivu, wanahabari wanaotazamiwa
kuelimisha na kuhabarisha jamii, lakini na asasi za kiraia, zinazojinasibu
kutoa elimu na kusimamia haki.
Wote hawa
hujitokeza kupitia majukwaa mbalimbali yakiwamo ya kuzungumza moja kwa moja
kwenye mikutano ya hadhara na ya ndani, kuandika na kutangaza, lakini pia
kufanya midahalo na mijadala inayoelimisha na kuhabarisha jamii kuhusu
uchaguzi.
Katika
majukwaa yote hayo, ni dhahiri kauli zinazotolewa huambatana na hisia za
wachangiaji hao na moja kwa moja kwa kusoma hisia hizo, msikilizaji, mtazamaji
na msomaji anaweza kubaini nini kinamaanishwa na kwa ajili gani na ya nani kwa
wakati huo.
Wapo
ambao wakizungumza moja kwa moja hujibainisha na vyama fulani au makundi fulani
ya watu katika jamii; lakini hivi sasa ni kwa vyama vya siasa hususan tawala
cha CCM na vingine ambavyo vinaunda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kwa
kifupi ni kuwa katika yote hayo kambi mbili hujibainisha wazi, moja ya CCM na
nyingine ya Ukawa, huku vyama vingine visivyo na nasaba na pande hizo mbili
vikibaki ama kutazama na au kushangilia malumbano yanavyoendelea.
Baadhi ya
vyombo vya habari na hata asasi za kiraia maarufu kama AZAKI, vimekuwa
vikijibainisha katika pande hizo, huku vikijisahau kuwa vinatakiwa kutokuwa na
upande na hivyo kutenda mambo yao kwa usawa ili kuepuka lawama na malalamiko.
Isipokuwa vile vilivyo maalumu kwa propaganda.
Hilo
limekuwa likishindikana kutokana ama na viongozi wa vyombo au wamiliki wao
kusimamia upande mmoja ama kwa makusudi au kwa maelekezo maalumu au pia kwa
matarajio fulani, kwamba kiongozi huyu akiingia madarakani pengine neema
itawashukia.
Lakini
pia wamekuwapo wazungumzaji ambao pengine kwa makusudi au kwa kuekelezwa,
hujikuta wakiongeza chumvi katika wanayoyasema au kushawishi umma ili uwaamini,
kwa sababu tu ni wasemaji au viongozi wa vyombo au taasisi hizo.
Lawama
nyingi zinaelemea vyombo vya habari na AZAKI ambao wamejikuta wakiingia katika
mkumbo wa vyama vya siasa ambavyo vina ajenda kuu za ‘kuing’oa CCM madarakani’
kwa vyovyote vile iwavyo na kujikuta wakihanikiza lugha hiyo hiyo kwa jamii.
Hapa
chama tawala na serikali yake vimekuwa vikitupiwa madongo na tope na kuonyesha
kwamba havijafanya lolote tangu kuzaliwa kwa Taifa hili, kwa kutumia kauli za
miaka 50 ya Uhuru hakuna kitu kilichofanyika, na watoaji wa matamshi hayo
wakionekana wenye siha njema wakiwasemea masikini waliosawajika.
Jumamosi
nilisikiliza kipindi cha Power Breakfast on Saturday kinachorushwa na
kituo cha Clouds Radio, ambapo Mratibu wa AZAKI, Onesmo ole Ngurumwa
alikuwa akizungumzia Ilani ya Uchaguzi iliyoandaliwa na Azaki, akisisitiza kuwa
ndiyo inayostahili kuzingatiwa kutokana na kwamba za vyama vinavyogombea
uongozi havina mashiko.
Nilimsikia
Ngurumwa akidai kuwa Azaki ni mhimili wa nne wa Dola baada ya Serikali, Bunge
na Mahakama, kwa hiyo zina nafasi kubwa katika jamii kwenye kuelimisha na hata
kusimamia haki za ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi na chama
kinachofaa kuiongoza Tanzania ijayo.
Niliheshimu
mawazo yake kama alivyotumwa na Azaki na akiwa mwanasheria nikaamini kwamba ni
mtu ambaye atasimamia kwenye ukweli na hataupindisha wala kuongeza chumvi
katika anayoyasema katika kuelimisha umma wa wananchi.
Nilitarajia
asingejinasibu kuwa Azaki ni mhimili wa nne, labda kama angerekebisha kauli na kusema
‘tunajiita mhimili wa nne’. Asubiri abatizwe si kujibatiza mwenyewe kwa kudhani
kuwa kazi anayofanya ni kubwa sana katika jamii kuliko makundi mengine kama
yaliyotajwa hapo juu.
Alikwenda
mbali zaidi pale alipoamua kuiponda serikali iliyoko madarakani, kwamba kwa
miaka zaidi ya 50 sasa bado inakalia kujenga barabara badala ya hivi sasa
“tungekuwa tunazungumzia kupeleka ndege Marekani…!”
Lakini
pia katika kuongeza chumvi akitaka kusisitiza na kuhalalisha anachokisema,
akadai kuwa nchini wapo watu ambao hawapati hata mlo mmoja kwa siku! Mwenye
akili timamu lazima aamini kwamba watu wa aina hiyo hawapo nchini kwani
wameshafariki dunia wote, kwa sababu kukosa mlo mmoja kwa siku ina maana hawana
uhai.
Nilimsikia
pia akiponda vyombo vya habari kuandika habari za wagombea na badala yake
waandike habari kuhusu wananchi, akitaka wananchi ndio wazungumze ya kwao ili
yaandikwe badala ya kila siku “kusikia Lowassa, Magufuli”.
Mbona
wananchi wakiuliza maswali kwenye mikutano ya hadhara wagombea wanakataa
kuyajibu na kudai hayana maana? Mwananchi wa Mvumi, Chamwino Dodoma, anamuuliza
mgombea kuhusu kutuhumiwa na sakata la mtambo wa kufua umeme wa Richmond,
anajibiwa kuwa hilo swali halina maana! Yapi yataandikwa ya wananchi?
Ieleweke,
kuwa matatizo ya wananchi yanajulikana kwa wagombea, hivyo hivi sasa ni fursa
yao kuyatafutia majawabu, badala ya kutaka kuulizwa maswali tena. Nani hajui
matatizo ya elimu, afya, maji nakadhalika? Ngurumwa hataki wagombea
hususan wa CCM wakalalamikia matatizo yaliyopo na eti badala yake waseme
mazuri waliyoyafanya tu? Inasikitisha, kwani wananchi hawana macho?
Kiongozi
wa Azaki anapaswa aelewe, kuwa mataifa yote duniani hivi sasa yanaendelea
na ujenzi wa barabara, aende Marekani, aende Afrika Kusini, aende Finland,
China na kwingineko, barabara na madaraja vinajengwa kama hapa kwetu licha ya
mataifa hayo kupata uhuru wao miaka zaidi ya hii ya Tanzania.
Kauli
kama hizi na zingine ndizo zinashawishi kuhitimisha kuwa wapo watu wanaongoza
taasisi na asasi kama hizi tayari wakiwa na misimamo ya pande na wanatumia
nafasi walizonazo kudanganya umma kwa malengo yao ya kisiasa.
Hawa ndio
wanaokuwa ndani ya taasisi hizo wakizitumia kama ngozi za kondoo huku wao mbwa
mwitu wakiwa ndani, kwa maana kuwa ni wanasiasa wanaojivika ngozi za taasisi na
asasi za kiraia na kuonekana wanatetea watu bila kuzingatia itikadi, kumbe wao
wakiwa na itikadi zao rohoni.
Si siri,
kwamba zipo baadhi ya asasi nchini ambazo zilishaingia ‘mikataba’ na wafadhili
wanaotaka kuona CCM inang’oka madarakani kwa udi na uvumba na zilishashuhudiwa
zikishirikiana na baadhi ya wapinzani kupanga mikakati ya kufanikisha azma hiyo
ambayo haina chembe ya demokrasia hata kidogo.
Ni bahati
mbaya hata wafadhili hao nao wamekuwa wakiwaaminisha kuwa hilo litawezekana na
“mtashinda saa nne asubuhi…watake wasitake na Ikulu mtaingia”. Huo ni
upotoshaji mkubwa na ni vema badala ya kulazimisha wananchi kumeza sumu,
waachwe waamue wenyewe kwenye masanduku ya kura Oktoba 25.
No comments:
Post a Comment