Thursday, 3 September 2015

SAMIA AWATOA HOFU WAKAZI WA KIGAMBONI



MARIAM MZIWANDA NA EPSON LUHWAGO

WANANCHI wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam, wameondolewa wasiwasi juu ya kuporwa ardhi yao na kwamba atakayeuza viwanja kinyemela atachukuliwa hatua kali.

Hayo yalisemwa jana na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan,  katika mkutano wa kampeni uliofanyika Vijibweni, Jimbo la Kigamboni.

Alisema katika upangaji wa mji mpya wa Kigamboni, wako wananchi ambao wana hofu na maeneo yao kudhulumiwa,  lakini aliwataka wasiwe na wasiwasi kwa kuwa serikali itawalinda.

Kwa mujibu wa Samia, ujio wa mji mpya wa Kigamboni ni kwa manufaa ya wananchi wa eneo hilo na kwamba hakuna mtu yeyote atakayefanya dhuluma au kujinufaisha kupitia mradi huo.

“Natambua kuwa wananchi wamekuwa na wasiwasi juu ya viwanja vyao. Lakini nawahakikishia kuwa hakuna mtu atakayeuza ardhi kinyemela na atakayebainika tutashughulika naye. Pia nawatahadharisha msirubuniwe na kama kuna watu wanafanya mchezo huo mtoe taarifa ili hatua zichukuliwe,” alisema.

Samia alimmwagia sifa Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndungulile, kwa kuwa imara katika kuhakikisha hakuna watu wanaojinufaisha na kwamba amekuwa akilisemea jambo hilo mara kwa mara.

Pia alimsifia kwa kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Kigamboni, hususan huduma za afya, maji safi na salama na umeme.

Akizungumzia kero zinazoendelea ndani ya jimbo hilo, alisema serikali inafahamu kuwa baadhi ya wananchi hawajafikishiwa huduma ya umeme kwamba wataupata muda mfupi kuanzia sasa.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kujihadhari na watu wanaopita na kuwarubuni kuwa wanawafanikishia upatikanaji wa nishati hiyo kwa sababu kazi hiyo inafanywa na serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kuhusu maji, alisema mpango wa uchimbaji wa visima virefu katika eneo la Kigamboni umekamilika kwa jimbo zima, hivyo maji safi na salama yataanza kupatikana punde.

“Jambo lingine ni kwamba yametengwa maeneo 5,000 kwa ajili ya wafanyabiashara ili kuwaondolea bughudha ya kufanya shughuli zenu kutokana na kukosekana kwa maeneo,” alisema.

Sambamba na hilo, alisema anatambua kuwa suala la kodi kwa wafanyabiashara hao ni kikwazo kutokana na kuwepo kwa mlundikano wa kodi nyingi.

Alisema CCM kupitia Ilani ya Uchaguzi itaangalia upya makato ya kodi ili kupunguza kero na kuwapa wananchi unafuu wa maisha.

Katika hatua nyingine, Munira Masanja, mke wa mgombea udiwani wa CHADEMA,  Kata ya Somangira, Francis Masanja, alijiengua katika chama hicho na kujiunga na CCM.

Akizungumza baada ya kukabidhi kadi ya CHADEMA, Munira alisema anaamini sera za CCM na mwelekeo wake na kwamba ataipigania kwenye kampeni zake.

AAHIDI NEEMA MBAGALA

Katika jimbo la Mbagala, Samia aliahidi ujenzi wa masoko ya uhakika kwenye kata zote ili wafanyabiashara  wafanyebiashara zao kwa uhakika.

Alisema masoko hayo yatakuwa na miundombinu yote yakiwemo maduka, vituo vya polisi na sehemu za kuuzia bidhaa mbalimbali kama vile vyakula, nguo na mahitaji mengineyo.

Pia alisema wakati mipango hiyo inaandaliwa, serikali ijayo ya CCM itapambana na mgambo ambao wamekuwa wakiwakera wafanyabiashara na kuwanyang’anya bidhaa zao.

“Tunatambua kuwa mgambo ni kero kwa wafanyabiashara katika jiji la Dar es Salaam. Lakini sasa ninaomba niwape ujumbe kwamba mwisho wao umekaribia. Waache kunyanyasa wafanyabiashara, sasa watafute kazi nyingine,” alisema.

Alisema maeneo 5,080 yametengwa kwa ajili ya wafanyabiashara katika jimbo la Mbagala na kwamba mpango wa kuundwa mamlaka maalumu ya kuunganisha wajasiriamali unafanyika.

Samia pia alisema mpango mwingine ni wa majisafi na salama ambao umepewa kipaumbele kwenye Ilani utafatekelezwa ili kuwaondolea wananchi kero ya kusaka huduma hiyo kwa umbali mrefu.

“Sitastahimili kuona wanawake wakiendelea kuteseka katika kutafuta maji. Nikiwa mwanamke natambua kuwa katika familia kukiwa na tatizo la maji ni kero, hivyo naahidi nitalisimamia kwa nguvu zangu zote,” alisema.

Akizingumzia msongamano wa magari katika jimbo la Mbagala, alisema katika Ilani, umeandaliwa mpango wa kufufua reli na kutengeneza barabara 16 za mchepuko ambazo zimepandishwa  kuwa chini ya Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania (TANROADS).

“Nikisaidiana na Dk. John Magufuli, tutahakikisha tunaisukuma TANROADS kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa haraka, ili kuwondolea adha ya wananchi kusafiri muda mrefu katika masafa mafupi,” alisema.

Samia alikuwa akijibu hoja hiyo baada ya kuambiwa kuwa wananchi wamekuwa wakisafiri kwa zaidi ya saa tatu hadi nne kutoka Mbagala kwenda katikati ya jiji na kurejea nyumbani kutokana na msongamano wa magari.

AMNANGA JUMA DUNI HAJI

Katika mkutano huo, Samia alimshangaa mgombea mwenza wa CHADEMA, Juma Duni Haji, kuzungumzia suala la uzazi kwa wanawake wakati hajui lolote.

“Napenda nimwambie kuwa hasara yake, najua hajui yaliyoko leba (chumba cha kujifungulia). Mimi ni mwanamke na nimezaa watoto wanne, hivyo najua kero zilizoko huko na nasema kwa uchungu. Nikisema  nitazishughulikia nitafanya kweli kwa sababu nizifahamu fika,” alisema.

Samia alisema atahakikisha wanawake wanajifungua katika mazingira na hali salama na uwepo wa madaktari na wakunga wenye uwezo kwa ajili ya kupokea watoto.

Kuhusu ulinzi na usalama, alisema anatambua kuwa Mbagala kuna kero ya vituo vya polisi, hivyo serikali ijayo itahakikisha inajenga vituo vingi, vidogo na vikubwa.

No comments:

Post a Comment