Thursday, 3 September 2015

BILIONI 650/- KUTUMIKA KUWAWEZESHA WANANCHI KIUCHUMI


Na Selina Wilson, Mtwara

SHILINGI bilioni 650 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya uwezeshaji wa wananchi ili wajikwamue kiuchumi na kubadilisha hali za maisha yao.

Fedha hizo ambazo zinayalenga makundi ya kina mama na vijana, zitaanza kutolewa na serikali ya awamu ya tano ili kuwaongezea wananchi uwezo wa kuondokana na umasikini.

Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli alitoa ahadi hiyo katika mikoa sita aliyopita kufanya mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu utakafanyika Oktoba 25, mwaka huu.


Mikoa hiyo ambayo Dk. Magufuli alivuta umati mkubwa wa watu kwenye mikutano yake ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Mtwara.


Akizungumza juu ya uwezeshaji huo, alisema fedha hizo zitatolewa kwenye vijiji 12,500, nchini kote kwa mgawanyo wa sh. milioni 50 kwa kila kijiji.


"Fedha hizi watakopeshwa vikundi vya kina mama na vijana. Tunataka wafanye biashara za ujasirimali ili waondokane na umasikini," alisema kwenye mikutano ya kampeni.


Dk. Magufuli alisema matatizo madogo madogo ndio kero kubwa za wananchi, hivyo akiwa rais atahakikisha anazimaliza katika kipindi kifupi atakachoingia madarakani.

Akiwa Mtwara, Dk. Magufuli alisema watu wanaweza kuhoji fedha hizo atazipata wapi, lakini aliwahakikishia kwamba fedha zipo kinachotakiwa ni usimamizi madhubuti.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alisema baadhi ya watu wanawatisha wafanyakazi kwamba akiingia madarakani watamkoma.


Akijibu hilo, Dk. Magufuli alisema yeye anapenda wafanyakazi wanaojituma sio wazembe ambao kazi hawafanyi, lakini wanataka walipwe vizuri.


Dk. Magufuli aliwaeleza wananchi katika maeneo mbalimbali kwamba amesimamia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wafanyakazi wanachapakazi na wanalipwa vizuri.

Alisema wapo watu wanalipwa mshahara hadi sh. milioni tano kutokana na kufanya kazi na watu wengi wanakimbilia kufanya kazi TANROADS.


Aliwataka wafanyakazi kufanyakazi kwa bidii na akiingia madarakani atahakikisha wanalipwa vizuri, lakini wale wanaoingia kazini saa nne na kutoka saa tano hawatakuwa na nafasi.


Katika mikutano yake, Dk.Magufuli aliongozwa na wajumbe wa kamati kuu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Wakizungumza kwenye mikutano mbalimbali, viongozi hao waliwaeleza wananchi kwamba CCM haikukosea kumteua Magufuli kuwa mgombea urais kwa kuwa ni kiongozi makini, mwenye uzoefu na uadilifu wa hali ya juu kwenye utendaji.

Dk. Magufuli kesho anatarajiwa kuendelea na mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu katika mkoa wa Morogoro, ambapo atapita katika maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa huo, ikiwemo mikutano mikubwa ya hadhara itakayofanyika katika makao makuu ya wilaya.

No comments:

Post a Comment