Thursday, 3 September 2015
SAMIA AVUNA WANACHAMA 50 CHADEMA
NA EPSON LUHWAGO, DODOMA
MGOMBEA Mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, jana alihitimisha awamu ya kwanza ya kampeni kwa kishindo baada ya kuhutubia maelfu ya wananchi katika eneo la Chang’ombe mjini hapa.
Mkutano huo ulikuwa wa mwisho kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Dodoma. Awamu hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwani mikutano yake imekuwa kivutio kutokana na sera alizokuwa akizinadi ili wananchi waichague CCM.
Vilevile aliibomoa kambi ya upinzani baada ya kuvuna zaidi ya wanachama 50, akiwemo aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Vijana wa CHADEMA Mkoa wa Dodoma, Peter Chivuyo,
Kwenye mkutano huo wa jana, ambao ulihudhuriwa na mwanasiasa mkongwe, Mzee Job Lusinde, wananchi walikuwa wakishangilia kila alipokuwa akitoa ahadi, hali iliyoonyesha kuwa wamevutiwa na maneno yake.
Katika masuala ya ilani, alisema mkazo mkubwa utakuwa ujenzi wa viwanda vya kutengeneza mvinyo kutokana na zabibu ambazo zinastawi kwa wingi mkoani hapa.
Alisema ujenzi wa viwanda hivyo utaongeza thamani ya zao la zabibu na kuongeza ajira kwa vijana kwa kuwa watapata kazi na kuondokana na umasikini wa kipato.
Kwa upande wa maji na barabara, alisema si tatizo kubwa kwa sababu zile zinazozunguka mji zimejengwa kwa kiwango cha lami.
“Tatizo kubwa limekuwa la umeme kwani hata wakati nikiwa hapa nimeona unakatika katika. Sababu kubwa ni kutoka kwenye mitambo ya mafuta kwenda kwenye gesi. Muda si mrefu hali itakuwa shwari na kukatika itakuwa historia,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege, alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaeleza kwa undani suala hilo kwa kuwa kiwanja hicho kitajengwa eneo la Msalato na kukamilika katika miaka mitano ya serikali ijayo.
Pia, aliahidi kuwa serikali ijayo ya CCM inatarajia kuisuka upya Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu (CDA) ili iweze kuwa ya kisasa na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wa elimu, alisema mkazo mkubwa utakuwa ujenzi wa mabweni ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vishawishi ambavyo huchangia kupata ujauzito na kukatisha masomo.
LUSINDE AMCHANA LOWASSA
Mjumbe wa Kampeni ya Kitaifa ya CCM, Livingstone Lusinde, jana alimshambulia waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwamba ana uchu wa madaraka.
Alisema anashangazwa na kitendo cha Lowassa kuhamia CHADEMA na kuikashifu CCM wakati ndiyo iliyomlea na kumpandisha chati mpaka kupata nafasi ya waziri mkuu.
“Huyu Lowassa na CHADEMA yake hawana chochote cha maana na hawawezi kuwaletea Watanzania maendeleo yoyote. Kinachowatoa udenda ni gesi ili waweze kujichotea rasilimali zetu kwa manufaa yao.
“Mbaya zaidi ili aweze kunufaika nayo ameamua kuinunua CHADEMA kwa pesa. Wakristo tunasema fedha zilimuuza Yesu na sasa pesa za Lowassa zimeinunua CHADEMA.
“Lakini mbaya kuliko yote ni kwamba wale CHADEMA hawana nia ya uongozi wa nchi, wanachotaka ni pesa za Lowassa tu. Namsikitikia Regina (mke wa Lowassa), badala ya kumlinda mume wake kama Biblia inavyosema, ameshindwa. Wenzake sasa wanataka kummaliza kwa sababu ya fedha zake,” alisema.
Lusinde alisema CHADEMA imekodi watu wa kugombea kwa sababu haina watu ndani. “Wamemchukua Lowassa toka CCM na Juma Duni Haji (mgombea mwenza) kutoka CUF. Wote hawa ni ma-TX (wataalamu wa nje). CCM ndiyo yenyewe kwa sababu wagombea wake wametoka humuhumu ndani,” alisema.
Pia, alisema Ikulu ni sehemu ya kupeleka watu wenye uwezo wa kufanya kazi na si legelege kama Lowassa. Aliwataka wananchi wa Dodoma kuichagua CCM ili iendelee kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema Lowassa amepitwa na wakati kwa sababu umri wake umekwenda na kumchagua kuwa rais ni sawa na kumrejesha mchezaji mkongwe wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, acheze mpira leo.
Lusinde alisema: “Kibadeni alikuwa mchezaji nyota kwa wakati wake, lakini si sasa. Hata Lowassa zama zake zimepita, kama ni soka ni sawa na Kibadeni ni vyema akapumzika kwani nyota yake imekwisha.”
Akizungumzia uchaguzi mkuu kwa mkoa wa Dodoma, Lusinde alisema CCM itaibuka na ushindi wa kishindo kuanzia urais, ubunge na udiwani na kwamba wapinzani hawataambulia chochote.
“Hapa Dodoma Mjini kuna mtu anaitwa Singo (Benson Kigaila), amekimbilia hapa kugombea ubunge baada ya kupigwa na George Simbachawene kule Mpwapwa. Sasa amekuja hapa tutammaliza na atajua CCM si ya mchezo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa, alisema umati uliofika kwenye mkutano huo ni ishara tosha kwamba mkoa huo ni ngome ya Chama.
Alisema miaka yote Dodoma imekuwa ikibeba CCM katika uchaguzi kwa kuipa kura nyingi na mwaka huu itafanya hivyo tena kwa kishindo ili iendelee kuongoza dola.
Kwa mujibu wa Kimbisa, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, CCM haijawahi kupoteza kiti cha ubunge na pia imekuwa ikishinda kwenye udiwani na kuunda mabaraza ya madiwani katika halmashauri zote.
Alisema ili kuhakikisha ushindi unapatikana, watafanya kampeni za nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu, kitanda kwa kitanda, shuka kwa shuka na uvungu kwa uvungu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment