NA WAANDISHI WETU
MTAFARUKU umeendelea kutikisa kwenye kundi la UKAWA
baada ya vigogo wa vyama vya upinzani vinavyounda kundi hilo kukiuka
makubaliano ya kugawana nafasi za ubunge na udiwani.
Licha ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kuahidi
kuwa ndani ya siku tatu watamaliza mvutano huo, lakini imedhihirika wameshindwa
kufanya hivyo baada ya siku tatu kupita pasipo kufikia makubaliano.
Awali, vyama hivyo vilisema vitasimamisha mgombea
ubunge na udiwani mmoja katika kila eneo la uchaguzi ili kukabiliana na Chama
Cha Mapinduzi (CCM), lakini vimeshindwa kutimiza lengo hilo kufuatia uroho wa
madaraka waliokuwa nao.
Inadaiwa kuwa majimbo ambayo UKAWA wameshindwa
kusimamisha mgombea mmoja ni matatu ya mkoani Dar es Salaam ambayo ni Ukonga,
Segerea na Kigamboni; Serengeti mkoani Mara, Mtama (Lindi), Mtwara Mjini na
Kilombero lililoko mkoani Morogoro.
Mgawanyiko wa UKAWA ulionekana wakati wa uzinduzi
wa kampeni za mgombea urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa, ambaye aliwahi
kuwa waziri mkuu na kujiuzulu nafasi hiyo kwa kashfa ya Richmond.
Katika uzinduzi huo, UKAWA iliwatambulisha
wagombea ubunge wawili wawili katika majimbo matatu ya Dar es Salaam, pia hali
hiyo bado imeendelea kujitokeza katika jimbo la Temeke.
Kwa mujibu wa makubaliano ya UKAWA, Jimbo la Temeke lilikuwa upande wa CUF, lakini
Chadema wameendelea kumsimamisha kibabe mgombea wao, Richard Mwakyembe, ambaye
pia amekamilisha taratibu za ushiriki kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Licha ya Mwakyembe kupewa Kata ya Mtoni kuwania
nafasi ya udiwani, ametoa masharti kuwa lazima CHADEMA wapewe kata tano ambazo
awali zilikuwa mikononi mwa CUF ili aweze kuachia nafasi hiyo.
Akizungumza sakata hilo, Mwenyekiti wa CUF Wilaya
ya Temeke, Rehema Kawamba, alisema wanashangazwa na madai hayo ya Mwakyembe ambayo
yana lengo la kuubomoa umoja huo.
Alisema katika kikao cha awali cha usuluhishi, Mwakyembe
aligoma kuhudhuria kwa madai kuwa sio halali na wala hatokubaliana na kufanyika
kwake kwa kuwa yeye ni mkubwa zaidi kuliko wajumbe wengine.
Mvutano huo ulisababisha wanachama wa CUF kuhisi
baadhi ya viongozi wao wanahusika katika kukihujumu chama chao.
Imeelezwa kuwa licha ya jitihada zinazofanywa na
uongozi wa CUF Wilaya ya Temeke kuutafutia ufumbuzi mvutano huo, Mwakyembe
anadaiwa kuendelea kukaidi.
Katika Jimbo la Segerea, kufuatia mzozo
unaoendelea ndani ya UKAWA, mgombea ubunge wa NCCR amejitoa kwenye mbio hizo
ili kulinda heshima yake.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, mgombea
huyo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa NCCR, Leticia Musole, amejiengua kutokana
na malumbano yaliyopo ndani ya UKAWA yasiyokuwa na majibu, hivyo kuhofia
kuchafuliwa jina lake.
Hivyo wagombea waliobaki katika jimbo hilo ni
kutoka vyama vya CUF na CHADEMA ambavyo vimekuwa viking’ang’ania nafasi hiyo.
Viongozi wa juu wa UKAWA wamenyooshewa kidole kuwa
ni chanzo cha mvutano huo wa kimaslahi kwa wagombea ubunge kutokana na
kuchelewa kutoa uamuzi.
Mvutano huo pia umejitokeza kwenye Jimbo la Mtwara
Mjini ambapo Mwenyekiti wa NCCR Mkoa wa Mtwara, Hassan Uledi, anawania nafasi
ya ubunge sambamba na mgombea wa CUF, Maftaha Nachuma.
Wagombea hao wote wanadai kupewa baraka zote na
umoja huo.
MBATIA AKIRI
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa
NCCR, James Mbatia, alisema bado kuna majimbo yana mvutano na kusababisha
kushindwa kufikia muafaka.
Alisema bado UKAWA wanaendelea na vikao vya
majadiliano ili kufanya maamuzi na kuwataka wagombea wa vyama vinavyounda kundi
hilo kuacha kulumbana.
Licha ya kuwepo kwa mzozo huo majimboni, Mbatia
alidai kwenye majimbo matatu pekee ndiyo wameshindwa kukubaliana.
Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Serengeti, Mwanga
na Mtwara Mjini.
“Ni kweli majimbo hayo yana utata, lakini yapo
majimbo tuliyoyatolea maamuzi likiwemo Segerea ambalo mgombea wake atakuwa
Julius Mtatiro kutoka CUF.
“Jimbo la Serengeti lina wagombea wawili ambao ni
kutoka CHADEMA na NCCR-Mageuzi, jimbo la Mwanga mgombea ni kutoka NCCR na
Chadema huku Mtwara mjini ni kutoka CUF na NCCR,” alisema.
00000
No comments:
Post a Comment