Na Selina Wilson, Ludewa
ADHA ya kutegemea kivuko cha Mto Ruhuhu kwa
wananchi wa Ludewa na Nyasa itamalizika baada ya kujengwa daraja
linalounganisha wilaya hizo.
Daraja hilo linatarajiwa kujengwa na serikali ya
awamu ya tano na ujenzi wake utakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya lami
kutoka Njombe/Ludewa/Nyasa.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Mgombea urais wa CCM
Dk. John Magufuli alipozungumza na wananchi wa Lipingu kabla ya kuvuka mto huo
kwa kivuko cha MV Ruhuhu.
Dk. Magufuli alisema anatambua adha wanayopata
wananchi wa Lituhi na Lipingu
vilivyotenganishwa na mto huo kutokana kivuko hicho kushindwa kufanya kazi maji
yapopungua.
Alisema baada ya kuingia madarakani ujenzi wa
daraja hilo na barabara za lami itakuwa miongoni mwa vipaumbele vyake na kwa
kuwa ipo kwenye ilani ya uchaguzi ni lazima itekelezwe.
Aliwataka wananchi wa vijji hivyo wamuamini
wampigie kura za ndio ili aingie madarakani atekeleze mipango ya maendeleo na
daraja hilo litakuwa la kwanza.
Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi wa Lipingu kwamba
ataanzisha skimu ya kilimo cha umwagiliaji ili wananchi waendeshe kilimo bora
na wapate mazao mengi ya chakula na biashara.
Alisema anazijua changamoto zao za pembejeo na
vifaa vya uvuvi hivyo atahakikisha vifaa hivyo vinashuka bei ili wananchi
wamudu kuvinunua na kuvua kwa ajili ya biashara.
Akiwa katika kijiji hicho pia alimnadi mgombea
ubunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na kuwasisitiza wananchi kwamba: "Deo
nampenda, ninamhitaji kwa kuwa ni kijana mchapa kazi mwenye kupenda maendeleo
ya wananchi wa jimbo lake."
Dk. Magufuli na msafara wake walivuka kwa kivuko
hicho cha MV. Ruhuhu ambacho kilivusha magari manne manne kwa awamu pamoja na
abiria.
No comments:
Post a Comment