Mama Samia akiwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa wakati akienda ukumbini Kulia ni Katibu wa CCM wa mkoa huo, Albaert Mgumba. |
Mama Samia akivishwa shuka nyeupe kuonyesha kukaribishwa kwa ukarimu na Kina mama wa Dodoma, kabla ya kuingia ukubini. |
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Dodoma, Fatuma Mwenda akimzawadia Mama Samia kitenge. |
NA EPSON LUWHAGO, BAHI
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM,
Angellah Kairuki, amesema uongozi wa nchi haupatikani kwa majaribio na maigizo
kama wanavyofanya baadhi ya wanasiasa wa upinzani.
Wakati kiongozi huyo akisema hayo, Mgombea Mwenza
wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kukonga nyoyo za wananchi kila
anakopita kutokana na ahadi zake zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa Mgombea
Mwenza wa Urais wa CCM, Samia, katika mji wa Bahi juzi, Angellah alisema baadhi
ya wanasiasa wanataka kuingia madarakani kwa kuwadanganya wananchi kuwa
wanawaonea huruma kutokana na matatizo waliyo nayo.
Bila kuwataja majina, Angellah ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema baadhi ya wanasiasa
wamekuwa wakienda kwa wananchi huku wakijifanya wanawahurumia kumbe ni usanii
mtupu.
Hivi karibuni, mgombea urais wa CHADEMA, Edward
Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji, walikwenda kwenye Soko la
Tandale na kupanda daladala kwa madai ya kujua matatizo na adha wanazozipata.
“Watu hawa wanaigiza kwenda kwa wananchi eti
wanataka kujua shida zao ili wakiingia Ikulu waweze kuzishughulikia. Uongozi
hauhuitaji maigizo. Hivi walikuwa wapi walipokuwa na nyadhifa kubwa serikalini?
Hawakuona matatizo hayo?
“Niwaulizeni ndugu zangu wa Bahi, hivi watu hawa
wanaweza kuja hapa Bahi na kushiriki kuvuna na kubeba magunia ya alizeti kutoka
mashambani? Tuachane na sanaa hizi. Uongozi ni kazi na anayetaka kuigiza aende
Kaole,” alisema.
Aliwataka Watanzania kuacha kudanganyika na usanii
huo bali wamchague mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kwa kuwa ni
mchapakazi ndiyo maana amekuja na falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) Amina Makilagi, alisema Magufuli ni mwadilifu na hana chembe
yoyote ya usanii, hivyo ndiye anayefaa kuwa rais wa Tanzania.
“Tukimchagua Dk. Magufuli atahakikisha matatizo
yetu yanapata ufumbuzi. Ameonyesha mfano katika ujenzi wa barabara hivyo
tukimchagua tuna uhakika atashughulikia matatizo ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wa mgombea mwenza, Samia, katibu mkuu
huyo alisema ni mwanamke jasiri na mahiri katika utendaji kazi na kwamba akiwa
Makamu wa Rais na kwa kushirikiana na Magufuli, wataipeleka nchi katika
mafanikio makubwa.
“Huyu ni mwanamke hodari na mchapakazi. Ni mcha
Mungu na anayesikiliza matatizo ya wanawake na vijana. CCM haikubahatisha
kumteua kuwa mgombea mwenza, imeona uwezo wake kutokana na historia yake ya
utendaji,’ alisisitiza.
SAMIA AKONGA NYOYO
Katika mkutano huo, Samia alikonga nyoyo za wananchi
wa Bahi pale alipoeleza kuwa kero zinazolikabili jimbo hilo zikiwemo za maji,
afya na elimu zinapatiwa ufumbuzi.
Alisema serikali inatambua kuwa Bahi ina tatizo
kubwa la maji na kwamba katika kulitatua, imetenga sh. bilioni 2.3 kwa ajili ya
kuvuta maji ambayo yatasambazwa sehemu mbalimbali.
“Niwahakikishie kuwa serikali imeshaliona tatizo
la maji hapa Bahi. Suala hili litaanza kushughulikiwa muda mfupi baada ya
serikali ya awamu ya tano chini ya CCM kuanza. Tupeni kura ili tuingie ofisini
na kuanza kutekeleza suala hili,” alisema.
Pia, alisema atafikisha ujumbe kwa Rais Jakaya
Kikwete ili kutekeleza hadi yake ya kutoa sh. milioni 400 kwa ajili ya
kusambaza maji kwenye mji huo.
Kuhusu viwanda, alisema mpango kamambe umeandaliwa
kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo na vya kati ambavyo vitawezesha wananchi
kusindika mazao kama vile alizeti na hatimaye kupata maendeleo badala ya
kulanguliwa na wafanyabiashara wanaonunua mazao hayo kwa bei ndogo.
Kuhusu tatizo la njaa katika maeneo mbalimbali,
ikiwemo Bahi, lililotokana na ukame, Samia alisema serikali imeanza kufanya
tathmini ili kuhakikisha wananchi wanapata chakula.
“Hili tunalitambua fika na tutalisimamia
kikamilifu. Lakini napenda niwahakikishie kuwa hakuna mwananchi ambaye atakufa kwa
njaa kwa sababu ya ukosefu wa chakula,” alisisitiza.
Ili kuhakikisha kilimo kinaleta tija, alisema
mpango mahsusi umeandaliwa wa kujenga skimu mpya za umwagiliaji na kukarabati
za zamani ili wananchi wa Bahi wajikite katika umwagiliaji badala ya kutegemea
mvua.
Mambo mengine aliyoahidi ni ujenzi wa mabweni
katika shule za sekondari za kata ili kuhakikisha wanafunzi wote, hususan wa
kike wanalala shuleni na kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha baadhi
kukatisha masomo kwa sababu ya ujauzito.
AWAPA SOMO WANAWAKE
Katika hatua nyingine, Samia aliwataka wanawake
kuhakikisha wanaichagua CCM ili iendelee kuongoza
Alisema Chama kinawategemea wanawake katika
kukipatia ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, hivyo wana
wajibu mkubwa wa kuhakikisha azma hiyo inatimia.
"Kina mama huu ni mwaka wetu kwani sisi
wanawake ni jeshi kubwa. Najua tutafanya kazi nyumba kwa nyumba hadi tuingie
madarakani,” alisema alipozungumza jana na wanawake wa Mkoa wa Dodoma, katika
ukumbi wa White House Makao Makuu ya CCM mjini hapa.
Samia alitumia muda huo pia kuipongeza CCM kwa
kuwapa kpaumbele wanawake ili kutimiza azma ya uwiano wa 50 kwa 50 katika
uongozi. Alisema katika kutambua hilo, CCM imetoa nafasi kwake kuwa mgombea
mwenza wa urais.
“Wanawake wamepewa nafasi za juu za uongozi
kutokana na kuwa CCM inawajali na ndio wengi na wapigakura wakubwa.
Nitahakikisha nafanya kazi kwa karibu na Dk. John Magufuli,” alisema.
Kuhusu vipaumbele alisema jambo kubwa litakuwa
huduma za afya hasa huduma ya mama na mtoto na kwamba dawa katika hospitali
zitakuwa za kutosha.
Kuhusu elimu, alisema jambo la kwanza atakalofanya
ni kujenga mabweni katika shule zote pamoja na kujenga vyoo vya shule ili
watoto wapate stara nzuri. Suala la maabara pia alisema litakuwa la kipaumbele.
Kwa upande wa kilimo, alisema serikali ijayo
itahakikisha kinapatiwa msukumo wa kipekee kwa kuwa ndicho mwajiri wa wananachi
wengi ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija, alisema msisitizo utakuwa
upatikanaji wa pembejeo hadi vijijini.
Sambamba na hilo, alisema maslahi ya walimu
yataboreshwa ambapo katika serikali ijayo itaanzishwa Tume ya Utumishi wa Walimu
ambayo alisema itakuwa imara.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi
wasitishike na ukame ambao umetokea katika baadhi ya maeneo na kusababisha njaa
kwa kuwa vserikali ina chakula cha kutosha kwenye maghala.
"Nimepita katika maeneo mengi na kushuhudia
ukame na njaa inaweza kutokea. Msijali serikali yenu ni sikivu na hakuna
mwananchi anayeweza kufa kwa njaa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma,
Alhaji Adam Kimbisa, alimhakikishia Samia kuwa Dodoma ni ngome ya CCM miaka
yote na wanawake waliowasili katika mkutano huo ndio wanamhakikishia ushindi.
"Hawa wanawake ndio watakaokwenda kufanya
kampeni nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, shuka kwa shuka hadi tuhakikishe
inaendelea kuwa ngome yetu, hivyo msiwe na wasiwasi na mkoa huu," alisema
Kimbisa.
0000
No comments:
Post a Comment