Na Mariam Mziwand na Emmanuel Mohammed
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta amemwelezea
mgombea urais kupitia UKAWA, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye, kuwa ni walaghai na wenye hadaa kwa wananchi.
Mbali na hilo alisema CCM itapata ushindi mkubwa
na mzuri katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa UKAWA kwa sasa ni vipande vipande.
“Ninachoweza kuwaeleza hawa watu ni kuwa ni
walaghai na wenye kujaa hadaa…wanachokifanya hivi sasa ni kutaka kucheza na
akili za Watanzania,” alisema Sitta.
Alifafanua kuwa hadaa na ulaghai huo unatokana na
viongozi hao kutoa ahadi ambazo wanajua serikali ipo karibu kuanza utekelezaji
wake.
Sitta alisema inashangaza kusikia Lowassa akisema
wakiingia madarakani watajenga reli ya kati ili hali anajua kuwa wakati wowote
mwezi huu, Rais Jakaya Kikwete atakwenda kuweka jiwe la msingi Soga – Mpiji kwa
ajili ya ujenzi wa reli hiyo.
Alifafanua kuwa tayari serikali imeomba heka 1,000
kwa ajili ya kufanya eneo hilo kuwa kituo kikubwa na kuwa treni ndogo ndiyo
pekee zitakuwa zinaingia mjini.
Waziri Sitta ambaye ni mmoja wa walioomba ridhaa
ya kupeperusha bendera kupitia CCM, kabla ya kuchaguliwa Dk. Magufuli, alisema
mradi huo utagharimu sh. trilioni 16 na kuwa utajengwa na mkandarasi Kampuni ya
China Railway Construction (CRCC).
Treni katika reli hiyo itakuwa na uwezo wa
kutembea kilomita 120 kwa saa, hivyo itachukua chini ya saa 12 kwa safari ya
kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma.
Pia, alisema baadhi ya kodi kwenye mazao ni
makubaliano ya kimataifa, hivyo haiwezekani akatokea mtu na kusema atafuta kodi
kama alivyotangaza Lowassa kwenye kampeni za UKAWA mkoani Iringa.
“Kuna sheria za kimataifa katika mambo ya kodi za
mazao mfano ni zao la tumbaku,” alifafanua Waziri Sitta.
Pia, alisema serikali ipo katika hatua za mwisho
za ununuzi wa ndege mbili na kukodisha nyingine moja na kuwa mipango hiyo
itakamilika kabla ya serikali ya awamu ya nne haijandoka madarakani.
Kuhusu matarajio ya matokeo ya uchaguzi mkuu,
Sitta alisema kwa kujiamini kuwa CCM itaibuna na ushindi mkubwa.
“Ushindi upo na tena mkubwa na mzuri…hata katika
nafasi za ubunge na udiwani matokeo yatakuwa mazuri na wabunge wengi watakuwa
wa CCM,” alisema Sitta.
Akizungumzia madai kuwa CCM imepanga kumchafua
Lowassa, Waziri Sitta alisema kazi hiyo haijafanyika na wala CCM haina mpango
huo bali kwa kuwa ameomba kuwania nafasi ya umma, atafuatiliwa kwa karibu ili
kujua uadilifu wake.
“Lowassa ni nani aonewe, CCM imemlea na inamjua
vizuri kuliko hao wengine huko alikokwenda. Mtu wa kutumia cheo vibaya na
kujilimbikizia mali…amejaa ulaghai na mbwembe na hana sifa za kuwa rais,”
alisema Sitta.
Alisema kutokana na mambo hayo, Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, alimkataa mapema na kumuona ni hatari kwa taifa.
“Mwalimu Nyerere alitoa angalizo na hakuficha
hisia zake kuwa Lowassa ni hatari na hafai kupewa nyadhifa za juu za uongozi na
alionya hata wale waliokuwa wakimuunga mkono,” alibainisha Sitta.
Hata wakati wa kipindi cha serikali ya awamu ya
nne, Sitta, alisema ndani ya miaka miwili alibainika tabia zake na ndiyo maana
alitoswa baada ya kukumbwa na kashfa ya Richmond.
Alisema suala la kutokuwa na uadilifu kwa Lowassa
halina kificho kwa kuwa utajiri mkubwa alionao umetokana na kujilimbikizia mali
akiwa madarakani.
Sitta alirudia kusisitiza kuwa angependa kuwe na
mdahalo utakaomjumuisha yeye, Dk. Harrison Mwakyembe (aliyekuwa mwenyekiti wa
tume ya Bunge) dhidi ya Lowassa na jopo la wanasheria atakaopenda
kuwashirikisha na kuwa licha ya kufanya hivyo hatakuwa na la kujitetea kuhusu
Richmond.
Kuhusu sakata la mabehewa chakavu, Sitta alikiri
kuwepo kwa matatizo katika uagizaji na uingizaji wa mabehewa hayo hapa nchini.
Hata hivyo, Sitta alisema wahusika wote katika
sakata hilo lililosababisha serikali kupata hasara ya sh. bilioni 230, watafikishawa
mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment