Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, amegonga mwamba baada ya jana kushindwa kufika na kuhutubia mkutano wa kampeni wilayani Ludewa.
Lowassa, aliyejiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu kutokana na kashfa ya Richmond, alishindwa kuendelea na mkutano huo kutokana na kutokuwepo dalili ya watu kuhudhuria.
Habari za kuaminika zilisema kuwa mkutano huo ulikuwa ufanyike saa 5:00 asubuhi, lakini hadi saa 6:30 mchana hakukuwa na dalili zozote za mgombea huyo kuwasili wilayani humo.
Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alifika wilayani humo akiendelea na utaratibu wake wa kutumia usafiri wa barabara na kufanya mkutano mkubwa mjini Ludewa, juzi kisha kuendelea na ziara yake.
Habari za kuaminika zilisema kundi la UKAWA lilifanya maandalizi makubwa ikiwemo kusafirisha watu kutoka maeneo ya ndani na nje ya Wilaya ya Ludewa ili kuhudhuria mkutano huo. Hata hivyo, wananchi wenyeji walisusa.
Hatua hiyo inatokana
na wakazi wa Ludewa wamechukizwa na
ajenda ya Lowassa ya kutaka kuwaachia huru wahalifu, wakiwemo waliohukumiwa kwa
ubakaji, mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Papii Kocha.
Kutokana na kukosekana kwa mkutano huo baadhi ya
wapambe waliosafiri jana kwa malori kwenda Ludewa walilazimika kuanza safari ya
kurudi kwa miguu kwenda Njombe na vijijini.Wakizungumza kwa jazba wafuasi hao John Haule kutoka Njombe na Kefa Mbilinyi, walisema waliahidiwa kulipwa fedha kwa kazi ya kuweka ulinzi kwenye mkutano huo, lakini wameambulia patupu licha ya kuanza kuifanya kazi hiyo.
Alisema kukwama kwa mkutano huo kumewafanya baadhi ya wafuasi kukosa hata nauli ya kurejea kwenye maeneo waliyotoka kwani, wengine walikodiwa magari.
Hata hivyo, wakazi
wa Ludewa walisema walishindwa kuhudhuria mkutano huo kutokana na ajenda za Lowassa
na kumtaka kwenda kuomba kura kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa ndiko
alikoweka taarifa yake ya ilani.
Wakazi hao hasa wanawake
walisema kamwe hawatahudhuria mkutano wa Lowassa, ambaye agenda yake kubwa ni
kuwaachia huru wabakaji, hivyo ni sawa na kuwadhalilisha.
Mmoja wa wakazi hao,
Suzan Haule, alisema mkutano huo ulipangwa kuanza saa Saa 5.00 asubuhi katika
uwanja wa mpira wa wilaya ambapo, hadi muda huo kulikuwa na watu watano tu.
“Tumetosheka na
tumemuelewa Dk. Magufuli, hivyo hatuna
haja ya kuhudhuria mikutano ya wagombea wasiokuwa na tija kwani, haiwezekani
mgombea ajenda yake kubwa ni kutetea wahalifu na wabakaji… hii nchi itakuwa ya
aina gani,” alihoji Suzan.
Alidai kuwa viongozi wa UKAWA walijitetea kwa
wananchi kuwa Lowassa alishindwa kufika kutokana na kukosa kibali cha kutua helkopta
na kuhoji kama watu wote wanaokwenda Ludewa wanakwenda kwa helikopta.Waliongeza kuwa utetezi huo hauna mashiko kwa kuwa Dk. Magufuli alikwenda kuzungumza na kuomba kura kwa wananchi kwa kutumia usafiri wa barabara unaotumiwa na walalahoi iweje yeye Lowassa ashindwe.
“Hizi ni dharau, Magufuli amekuja hapa kwa kutumia usafiri wa barabara na kuzungumza na wananchi…yeye anashindwaje na kusingizia hawana kibali cha kurusha helikopta. Kama anatafuta madaraka anashindwa kuja kisa hakuna ndege akipata uongozi si atakuja hapa kwa kubebwa mgongoni?
“Huko Dar alipanda daladala, huku kwetu anataka helikopta…sasa hatumtaki na wala hatuna mpango naye,” aliongeza.
Taarifa zilizopatikana ndani ya UKAWA zinadai kuwa kutofika Ludewa kwa Lowassa kunatokana na kushindwa kusafiri kwa gari kutoka Njombe hadi Ludewa umbali wa kilomita 70 kwa barabara.
DUNI AZOMEWA MASASI
Wakati
Lowassa akikwama Ludewa, mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji, ameshindwa
kuhutubia mkutano wa hadhara kutokana na wananchi kuzomea viongozi wa jukwaa
kuu.
Hatua
hiyo ilitokana na Duni kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro kuhusiana na kumsimamisha
mgombea ubunge, ambapo CUF imesimamisha mgombea kama ilivyo kwa NLD.
Hali
hiyo imejotokeza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Masasi,
ambapo hata hivyo ulivunjika kutokana na zomea zomea hiyo isiyokuwa na kikomo.
Kumekuwepo
na mvutano mkubwa katika jimbo la Masasi Mjini, ambapo kila chama kimesimamisha
mgombea wake huku viongozi wa UKAWA wakitangaza nafasi hiyo kuachiwa Mwenyekiti
wa NLD Taifa, Dk. Emmanuel Makaidi.
Mvutano
huo ulimfanya Duni kusitisha kuzungumza na kumuomba Habib Mnyaa kusaidia
kuwatuliza wananchi waliokuwa na jazba, ambapo hata hivyo hakufanikiwa huku
wananchi wakiimba nyimbo za kumkataa Dk. Makaidi.
Wananchi
hao walieleza bayana kuwa hawana imani na UKAWA na kwamba, wanamsubiri Dk.
Magufuli ili warudishe kadi za vyama vya upinzani na kurejea rasmi CCM.
Katika
hatua nyingine, Duni pia alishindwa kuhutubia wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu
baada ya kutokea kwa mzozo katika ya CHADEMA na CUF juu ya mgawanyo wa majimbo.
No comments:
Post a Comment