Tuesday 8 September 2015

WANAOJARIBU KUMTOA VIBANZI MACHONI LOWASSA, WANAMPOFUA KABISA MACHO





NA CHRISTOPHER LISSA
TANGU mwanasiasa mahiri nchini na mwenye ushawishi mkubwa kutoka kambi ya upinzani, Dk. Willibrod Slaa,  aibuke  na kusema mgombea urais wa UKAWA,  Edward Lowassa, hafai kuwa kiongozi  kutokana na kashfa nyingi za  ufisadi, bado hakuna hoja ya msingi  iliyotolewa kumfanya mgombea huyo kuwa katika kundi la wasafi.
Hii inamaanisha kuwa, aliyoongea Dk. Slaa yanabaki kuwa hai  katika  ukweli wake kwenye mioyo ya Watanzania waliochoshwa na vitendo vya kifisadi.
Kimya cha Lowassa  katika kuzungumzia  jinsi anavyonyooshewa kidole juu ya suala la ufisadi, si kwa ajili ya kujibu hoja za  Dk. Slaa tu, bali  hata katika harakati zake za kugombea urais.
Tofauti na mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli,  kuliongelea kwa uchungu suala la ufisadi kiasi cha kufikia kuahidi kwamba akichaguliwa  ataanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za mafisadi na yale aliyoyaita ‘mijizi’, Lowassa  na UKAWA  hawagusii kabisa suala hilo.
Lowassa,  anajua wazi kuwa moja ya masuala mazito ambayo Watanzania wanadai kuchoshwa nayo ni ufisadi. Si wale wa CCM na si wa UKAWA. Alijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa hiyo.
Kama kweli ana uchungu kwamba alionewa, basi huu ulikuwa ni wakati wake wa kupaza sauti kwamba  akipata urais atapambana vipi na ufisadi.
CCM  ilikwishatanganza vita ya kuondoa watendaji wasio waadilifu  na mafisadi. Mkakati huo uliitwa ‘kujivua gamba’.
Vyama vya upinzani hususan CHADEMA, ndivyo vilivyochochea  zaidi  vita dhidi ya ufisadi hapa nchini.
Inashangaza kuona  kwamba katika mikutano ya hadhara inayoendelea  hivi sasa,  wafuasi wa UKAWA  ndiyo wanaoongoza  kukumbusha viongozi wao  juu ya ufisadi uliowahi kufanyika hapa nchini, ukiwemo wa  Richmond, Kagoda, Meremeta, EPPA na  Escrow, wakitumia mabango na hata kujitahidi kupaza sauti.
Ajabu ni kwamba viongozi wa UKAWA  wamekuwa wakipotezea manung’uniko hayo huku wakiibebesha lawama CCM.  Wametia pamba masikioni.
Hawaelezi wazi kwamba  wao kama UKAWA watafanya nini kukabiliana na changamoto hiyo ya ufisadi. Pia hawaelezi wana mikakati gani juu ya watu wanaonyooshewa vidole kuwa  wamejihusisha na ufisadi.
Lowassa, anaeleza nini juu ya hukumu atakayotoa kwa wale wote waliotajwa katika kashfa za ufisadi, ambao wanachama wake wamekuwa wakilalamika katika mikutano yake?
Je, atawasamehe? Atawafungulia mashitaka au ataacha suala hilo kama lilivyo? Nini kauli yake Lowassa? Mbona huzungumzii hatua hizo kama alivyofanya Dk.  Magufuli?  Ukawa mnahoji hilo?
Kilio chenu kikubwa mbona ni ufisadi? Kwanini hamshangai viongozi wenu hawalipi uzito katika majukwaa? Kwanini hawaelezi jinsi watakavyo lishughulikia suala hilo na kufuatilia kwa karibu kashfa  za kifisadi zililolitafuna taifa hili?
Suala hili  halimo hata kwenye Ilani ya UKAWA, ambayo hata hivyo hatuamini kama ni kweli wanayo. Halikuzungumzwa?  Halikutajwa popote?
Ninahofu kuwa huenda Ilani hiyo ilizungumzia suala hilo kwa uzito mkubwa kwa sababu iliandaliwa wakati Lowassa  hajajiunga na CHADEMA, hivyo ikatupwa baada ya Lowassa kuingia.
Hapa nakumbuka msemo  maarufu wa ‘Usiyempenda kaja’. Yule ambaye walikuwa hawampendi akiwa CCM kaja UKAWA. Watu kimyaa!
Na kwa kuwa wakati huo Dk. Slaa  alikuwa ndiye Katibu Mkuu wa CHADEMA, sina shaka  alilikemea kwa uzito unaostahili suala hilo katika Ilani na  ndiyo maana imefichwa na hivi sasa CHADEMA na UKAWA vinaongozwa na fikra za Lowassa.
Analopanga  yeye ndiyo Ilani hiyo hiyo na hata kama ipo basi haizingatiwi.
Ni ukweli uliowazi kwamba  suala la ufisadi  halizungumziwi UKAWA kwa sababu wameshindwa kumsafisha mgombea wao kwa hoja ambazo zitawafanya waeleweke.
Hiki ni kibanzi katika macho ya Lowassa. Lakini cha ajabu  ni kwamba kuna watu ambao Lowassa ameomba wamsaidie kukitoa  badala yake.
Lowassa ni kama ameomba vipofu ili watoe vibanzi hivyo. Wanachofanya ni ‘kukorokochoa’ macho yake kiasi cha kumfanya asione kabisa  wafuasi wake  wanaopita mbele yake na mabango ya kupinga ufisadi.
Na si kwamba wamemharibu macho tu, bali hawa watu wameharibu mpaka mfumo wa kusikia.
Katika kitabu kitakatifu  cha ‘Biblia’,  Yesu alisema ‘Mtu hawezi kutoa kibanzi kilicho katika jicho la mwenzake mpaka kwanza atoe kibanzi kilicho katika jicho lake mwenyewe.’
Ukimya wa Lowassa katika suala hilo si kwamba amepuuzia hoja za Dk. Slaa. Si kwamba amedharau. Si  kwamba anakifua kipana cha kuhifadhi kashfa hiyo moyoni. Si kwamba anajiamini juu ya ukweli kuhusu jambo hilo.
Kama  Lowassa hana nia ya kumjibu Dk. Slaa, basi asingekuwa anahangaika  kutuma watu hawa  ili wajibu tuhuma hizo badala yake. 
Anachoshindwa ni kufanya mazingaombwe ya kuubadili ukweli huo kuwa uongo mbele za Watanzania wenye kiu na haja ya kujua ukweli.
Lowassa,  kukaa  kimya ni udhaifu, lakini wale anaowatuma kumjibia hoja zinazomkabili ni dhaifu zaidi.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia  ni mfano wa kutosha wa ‘mitume’ dhaifu wa Lowassa. Kipofu anayejaribu kutoa vibanzi katika macho ya Lowassa.
Mbatia ni  kiongozi wa juu wa chama, haifai   kutumika  waziwazi kumkingia kifua  Lowassa, ambaye  hata cheo cha  uwaziri mkuu anatajwa tu kwa sababu alipitia kabla ya kutibua mambo vibaya  na kuandika historia ya pekee ya  waziri mkuu wa kwanza Tanzania kushika wadhifa huo kwa kipindi kifupi.
Lakini kibaya zaidi ni udhaifu mkubwa wa hoja za Mbatia katika kumtetea ‘bosi’ wake dhidi ya kashfa lukuki zilizomzunguka  kuanzia utosi wake mpaka kwenye unyayo .
Inawezekana Mbatia akawa anaamini kuwa kusimama na kuongea lolote mbele ya kamera na kalamu za waandishi wa habari kutamfurahisha ‘bosi’ wake huyo kuwa kafanya kazi nzuri aliyotumwa, lakini kama Lowassa atafurahia hilo, basi ni kama aliyepungukiwa na upeo.
Lakini pia hoja za  aliyekuwa mke wa Dk. Slaa , Rose Kamili, ambaye  hakuna ubishi kwamba alitumwa kumjibia  UKAWA, ni kielelezo tosha cha mitume dhaifu wa Lowassa
Hivi katika hoja nzito alizoibuka nazo Dk. Slaa, Rose alitumwa ili ajibu  hoja ya kula mihogo tu? Hii ndiyo  waliona ni hoja ya msingi sana na si ufisadi uliotajwa?
Rose, alifanyia mkutano katika hoteli ya Regency, alilipa gharama kwa ajili ya kujibu hoja ya kula mihogo tu?  Aliita waandishi  wa habari  vyombo vyote,  tena kwa usimamizi wa karibu wa msemaji wa CHADEMA, Tumaini Makini, na baada ya mkutano huo, alitangaza kuwa anatoka kidogo ili kuwachukulia nauli waandishi hao. Kwa ajili ya umuhimu gani wa alilokuwa ameongea?
Potelea mbali muendelezo wa  hoja  ‘mbovu’ za Frederick Sumaye,  ambaye ameingia UKAWA akiamini kuwa  ni ukweli kwamba Lowassa atashindwa  vibaya katika uchaguzi mkuu 2015, na akishindwa hana ujanja wa kugombea tena kutokana na afya pamoja na umri alionao.
Hivyo Sumaye anasubiri Lowassa amuandalie wafuasi  wa kutosha ili atakaporithi nafasi hiyo, awe na mtaji wa wafuasi.
Mara ameibuka Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na  Uzima, Josephat Gwajima na utetezi wake, ambao  unathibitisha fika kwamba ameanza  kutoka kwenye njia sahihi ya kutangaza neno la Mungu  na kuingia kwenye masuala ya siasa.
Hata utetezi wa wafuasi wa UKAWA juu ya kashfa hiyo ni dhaifu sana, kwani wengi wanadai kuwa wanahitaji mabadiliko tu.
 Lowassa awe na kashfa kibao, lakini wanahitaji mabadiliko. Hawa ni vipofu wanaojaribu kuliweka rehani taifa hili kwa mzaha mzaha, ambao baadaye unaweza kutunga usaha.

No comments:

Post a Comment