Thursday, 3 November 2016

UKWEPAJI KODI WAIKOSESHA SERIKALI BILIONI 319/-




UKWEPAJI wa kodi kupitia nguo zitokazo nje ya nchi umeiingizia serikali hasara ya sh. bilioni  319 kwa mwaka.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, mjini Dar es Salaam, jana, wakati wa Tamasha la Mwezi la Wanawake Wajasiriamali (MOWE).

Alisema kiasi hicho cha fedha hupotea kila mwaka na kuisababishia serikali hasara kubwa, kutokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kushindwa  kusimamia ipasavyo makusanyo ya kodi yayotokana na nguo zinazoingizwa nchini.

Mwijage alisema serikali kupitia wizara yake, itahakikisha bidhaa zinaingia nchini, lakini kutakuwa na bei halisi, hivyo bidhaa za ndani ya nchi zinatakiwa kuwa na ubora.

Pia, alisema ili kuhakikisha bidhaa za haa nchini zinakuwa bora,  serikali  itahakikisha inaweka mtambo mzuri wa kutengeneza vifungashio kwa lengo la kuwasaidia wateja kupata huduma bora na ya uhakika.

Aliwataka wajasiriamali kuhakikisha wanajiunga na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO), ili kupata uwezo wa kuzalisha bidhaa na kuongeza thamani.

Waziri Mwijage aliwataka wajasiriamali hao kufanya biashara yenye faida, badala ya kunakili kutoka kwa wengine kwa kuwa lengo ni kuhakikisha kunapatikana upenyo wa kuleta faida zaidi.

“Ili kuhakikisha viwanda vidogo vinakuwa, nitahakikisha ninaihamisha ofisi  yangu kwenda mikoani kwa ajili ya kutoa elimu ya biashara baada ya miezi miwili  kuanzia sasa,”alisema.

Mwenyekiti wa MOWE, Eliaika Mrema, alizitaja changamoto ambazo  wajasiriamali wanakumbana nazo kuwa ni uwezo wa kuyafikia masoko ya uhakika, ugumu wa upatikanaji habari na mtaji wa kuendeshea biashara.

Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni uwezo wa kufanyika kwa maadhimisho hayo mikoani kutokana na kipato kuwa kidogo.

Aliiomba serikali kuhakikisha inazitoza kodi kubwa nguo zitokazo nje ya nchi kwa lengo la  kuwahamasisha wajasiriamali wa ndani kutengeneza bidhaa zilizo bora.

No comments:

Post a Comment