Thursday, 3 November 2016
MACHINGA WAKABIDHIWA MITAA YA LUMUMBA, MKUNGUNI
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, inatarajiwa kuzindua gulio kubwa na la kipekee kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo (machinga), katika barabara za Lumumba na Mkunguni.
Aidha, serikali imewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa, hakuna atakayepigwa wala kuumizwa wakati wa utekelezaji wa mpango wa kuwaondoa katika maeneo yasiyo rasmi, iwapo watakubali kuondoka kwa hiyari.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, wakati wa ziara yake ya kukagua masoko na kuwaandaa wamachinga kuondoka kwenye maeneo yasiyo rasmi, hususan katikati ya jiji, bila kutumia nguvu.
Sophia alisema uzinduzi wa gulio hilo umepangwa kufanyika Novemba 11, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, gulio la Lumumba litakuwa likianza baada ya swala ya Ijumaa na kuendelea hadi Jumapili.
Alisema barabara ya Lumumba itakuwa ikifungwa upande mmoja usio na maduka ili kupisha magari kupita, ambapo wafanyabishara watakuwa wakifanya bishara zao hadi barabara ya Mkunguni, karibu na soko la Kisutu.
“Barabara ya Lumumba ina urefu wa kilomita moja na ina sehemu mbili zenye upana wa mita saba kila moja. Katika mtaa huu, tunatarajia kuwa nafasi za kufanyiabishara zaidi ya 5,000 zitapatikana,”alisema Sophia.
Aliongeza kuwa barabara ya Mkunguni ina urefu wa mita 600 na ina upana wa mita nane, ambapo kutakuwa na nafasi 1,800, kwa ajili ya wafanyabiashara hao.
“Kutokana na hali hiyo, sehemu ya mwanzo ya barabara ya Lumumba kutokea barabara ya Morogoro, itatumika na magari hadi makutano ya barabara ya Lumumba na Mafia,”alibainisha mkuu huyo wa wilaya.
Aliongeza: “Maeneo yanayoungana na benki za CRDB Tawi la Vijana na CRDB Tawi la Ushirika katika mtaa huo, hayatatumika kwa biashara ili kutokuathiri shughuli za kibenki.”
Mkuu huyo wa wilaya alisema tayari wameafikiana na uongozi wa wamachinga kwamba, biashara zote katika barabara hizo zitakuwa zikifanyika juu ya meza na wauzaji wote watapatiwa vitambulisho kwa utaratibu utakaofaa, ili kuwatambua na kurahisisha ukusanyaji ushuru na usalama.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wamachinga wote, hususan walioko eneo la Kariakoo, kuitumia fursa ya gulio hilo kwani halmashauri itawasaidia kulitangaza ili liweze kuvutia watu wengi.
“Lakini pia tumeongea na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Nchi Kavu na Majini (UMATRA) ili magari yote sasa yapitie kwenye gulio hilo,”alisema.
Akiwa eneo la Gerezani, Sophia alizindua uandikishaji wa wamachinga wasio na maeneo ili waweze kupatiwa maeneo yatakayowawezesha kujipatia kipato.
“Manispaa imetenga masoko matano ili kuwahamishia wamachinga, ambapo kwa kuanzia, masoko mawili ya Kigogo Freshi na Kivule Kerezange, yamekamilika na masoko matatu ya Kivule Center, Kinyerezi na Tabata Muslim yanaendelea kuboreshwa,”alisema.
Aliwatahadharisha wafanyabishara hao kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kuchukua hatua za kuwapa maeneo ili waweze kujipatia riziki.
“Serikali inatambua kwamba shughuli zenu ni halali kwa ajili ya kujipatia kipato, hivyo hatutawaangusha. Tuko tayari kushirikiana nanyi kwa kila hatua ili kuepusha mgogoro. Ila kwa wale ambao watakaidi, hatutashindwa kuwaondoa,”alionya Sophia.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao wa Ilala, Steven Lusinde, alisema wamekuwa na mazungumzo na mkuu huyo wa wilaya, ikiwemo kumpelekea mapendekezo.
“Suala la magulio ni muhimu na tumeridhika nalo na tuliwahi kulipendekeza ili kupunguza msongamano katikati ya jiji,”alisema Lusinde.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment