Wednesday 9 September 2015

KISHIMBA AAHIDI NEEMA KAHAMA





Na Chibura Makorongo, Kahama

MGOMBEA ubunge wa  jimbo la Kahama mkoani Shinyanga, Jumanne Kishimba (CCM), amesema iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha hospitali ya wilaya hiyo inapandishwa hadhi na kuwa ya rufani.

Pia, alisema atashughulikia kwa haraka uanzishwaji wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kahama.

Kishimba alitoa ahadi hiyo juzi alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Kahama na vitongoji vyake, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CDT mjini hapa, kwa ajili ya kampeni za kuomba kura kwa wananchi na kunadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Aliwaomba wakazi wa jimbo la Kahama, kuhakikisha kuwa Oktoba 25, mwaka huu, wanampigia kura za kishindo ili aweze kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vile amedhamiria kwa dhati kushirikiana nao katika suala zima la maendeleo.

Akifafanua kuhusu ahadi ya kuipandisha hadhi hospitali ya sasa ya serikali wilayani humo, alisema wilaya hiyo hivi sasa ina ongezeko kubwa la wakazi huku wengine wakitoka mikoa jirani, ambao wanategemea huduma za matibabu kutoka katika hospitali hiyo na hivyo kuzidiwa na idadi ya wagonjwa.

“Ndugu zangu wakazi wa Kahama, tumekutana katika mkutano huu kwa lengo la kuwaomba kura kutoka kwenu, naomba mnichague niweze kuwa mwakilishi wenu bungeni, na moja ya mambo muhimu ninayowaahidi iwapo nitachaguliwa ni kupigania hospitali yetu hii iweze kupandishwa hadhi,” alisema.

Kuhusu kuanzishwa kwa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kahama, alisema pia itakuwa ni moja ya vipaumbele vyake na kwamba kuanzishwa kwa baraza hilo ambalo tayari mamlaka husika zilisharidhia uanzishwaji wake, utasaidia kupunguza migogoro mingi ya ardhi iliyopo kwa sasa.

“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, asilimia 75 ya migogoro yote ya ardhi inayofikishwa katika Baraza la Ardhi mkoani Shinyanga, inatoka wilaya ya Kahama, sasa ni vizuri tukawa na baraza letu wenyewe ili kuwapunguzia wananchi gharama za kwenda mkoani kila mara,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM wilayani Kahama, Mabala Mlolwa, aliwaomba wakazi wa wilaya hiyo  wasifanye makosa Oktoba 25, mwaka huu, na wahakikishe wanawapigia kura wagombea wote wa CCM, kuanzia rais, mbunge na madiwani waliosimamishwa na Chama.

No comments:

Post a Comment