Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi limewataka wananchi kufuata
sheria na kuweka uzalendo mbele ili kuhakikisha kampeni za uchaguzi mkuu
zinafanyika kwa amani bila misuguano baina ya polisi na raia.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba,
alisema jana kuwa Watanzania wote wanaoshiriki kwenye kampeni wanapaswa kuweka
mbele utaifa badala ya ushabiki wa kisiasa unaoweza kuvuruga amani.
“Wote tunapaswa kushirikiana kulinda amani
yetu. Hivyo wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa wanapaswa kutambua kwamba
kulinda amani ni jambo la msingi zaidi,” alisema.
Aliwatahadharisha wanasiasa na wafuasi wa
vyama kuepuka kujiingiza kwenye makosa ya jinai, kutokana na siasa kwa vile
sheria zinazosimamia uchaguzi hazitoi mwanya kwa wanasiasa kufanya mambo
yanayopitiliza na kuivuruga jamii.
Alisema jeshi la polisi limejipanga vizuri
kwa muda wote wa kampeni, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi na
litamshughulikia yeyote atakayevunja sheria bila kuangalia anatoka kwenye chama
gani cha siasa ili kulinda amani ya nchi.
Kwa mujibu wa Advera,watu kadhaa wamekamatwa
na wanaendelea kuhojiwa kutokana na kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa
amani.
Akifunga mafunzo ya wiki mbili kwa polisi wa
kada mbalimbali kuhusu haki za binadamu na matumizi ya nguvu kwa kiasi wakati
wa uchaguzi yaliyofanyika hivi karibuni Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa
Polisi, Mary Nzuki, alisema jeshi hilo limechukua tahadhari zote kuhakikisha
kuwa kampeni na uchaguzi unafanyika kwa amani.
No comments:
Post a Comment