Wednesday 9 September 2015

SAMIA AAHIDI KUWAPIGANIA WANAWAKE NA VIJANA




NA ABDALLAH MWERI, NYASA
MGOMBEA mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema atatumia uzoefu wake wa uongozi kuhakikisha wanawake na vijana wanapata asilimia tano ya fedha zilizotengwa kwa kila halmashauri nchini.

Akizungumza na wakazi wa wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, Samia alisema atakuwa mkali kusimamia fedha hizo kwa kuwa zimetengwa kwa ajili ya kuwakomboa wanawake na vijana kiuchumi.

Samia alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani hapa, ambapo aliwasihi wakazi wa Kijiji cha Tingi, Kata ya Tingi, kumchagua Dk. John Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano.

Alisema halmashauri nyingi nchini zimeshindwa kutekeleza agizo hilo kwa mujibu wa sheria, lakini wakimchagua Dk. Magufuli kuwa rais, wanawake na vijana watapata fedha hizo ili ziwakomboe kiuchumi.

"Nafahamu wanawake na vijana kuna fedha zenu asilimia tano mnatakiwa kupata kutoka halmashauri, lakini hamzipati, sasa serikali mtakayoichagua ya awamu ya tano na mimi nikiwa mama, nitahakikisha mnapata fedha zenu," alisema Samia.

Samia alisema anachukizwa kuona baadhi ya kina mama na vijana wanashindwa kupata maendeleo wakati halmashauri husika zinatakiwa kuwapa fedha hizo kwa mujibu wa sheria.

Alisema serikali ya Dk. Magufuli itaongeza pembejeo za kilimo ili kutoa fursa kwa wakazi wa wilaya ya Nyasa kulima kitalaamu kwa lengo la kupata mazao bora, ambayo yatainua kipato cha kila mkazi wa Kijiji cha Tingi na maeneo ya jirani.

"Uchumi wa nchi yetu kwa kiasi kikubwa unategemea kilimo, hivyo mkimchagua Dk. Magufuli na mimi msaidizi wake tutahakikisha tunaongeza pembejeo kwa wakazi wa Nyasa ili mlime kwa ufanisi," alisema Samia.

Aidha, Samia alisema serikali hiyo itaongeza kasi nzuri iliyoanza kufanywa na Rais Jakaya Kikwete, kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata umeme kwa kutumia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) ili kutoa fursa kwa vijana kujiajiri.
Mjumbe wa Kampeni ya CCM, Taifa, Angella Kairuki, alisema Dk. Magufuli na Samia ni wachapakazi hodari na wamejipanga kuwakomboa Watanzania endapo watapewa ridhaa ya kuongoza serikali ya awamu ya tano.
Kampeni za kuwania nafasi za urais, ubunge na madiwani zimepamba moto, baada ya kuzinduliwa rasmi Agosti 22, mwaka huu, ambapo uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment