Wednesday, 9 September 2015

'CHAGUENI VIONGOZI MAKINI NA WENYE SIFA'





Na Clarence Chilumba, Nachingwea
WANANCHI wilayani hapa mkoani Lindi, wameombwa kuchagua viongozi makini na wenye sifa ya kuliongoza taifa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), mkoa wa Lindi, Amiri Mkalipa, alitoa ombi hilo jana, wakati wa uzinduzi wa kampeni za  CCM zilizofanyika katika viwanja vya Mauridi mjini hapa.
Alisema wananchi wanapaswa kuwa makini kipindi hiki ili kuchagua viongozi wenye sifa ambao wanatoka CCM.
Alisema  kwa kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, ameweza kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo miundombinu ya barabara, elimu, afya, kilimo na maji.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Nachingwea, Hasani Masala, alisema kilichomsukuma kuwania nafasi hiyo ni kuwatumikia wananchi wa wilaya hiyo.
Aliwaomba wananchi wamchague ili aendele kuboresha huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo maji safi na salama, elimu na afya.
Masala alisema katika kipindi cha uongozi wake, atahakikisha anaisimamia halmashauri ya wilaya hiyo ili iweze kuongeza mapato na kunyanyua uchumi wa wananchi.
Aidha, alisema atahakikisha kilimo kinaboreshwa kwa kuongeza zana za kisasa, ikiwemo matrekta na kwamba atasimamia kwa ukaribu kuona wakulima wananufaika na mfumo wa ununuzi wa mazao.

No comments:

Post a Comment