Monday, 11 January 2016
ZAHANATI BUBU YAGUNDULIKA RUNGWE
TIMU ya ukaguzi kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani mkoa wa Mbeya, imebaini kuwepo kwa zahanati bubu iitwayo St. Mary, iliyoko kijiji cha Ndembela, kata ya Makandana, wilayani Rungwe, mkoani hapa.
Imeelezwa kuwa zahanati hiyo inayomilikiwa na Dk.Edward Kalundwa (75), ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Dk.Kibopile, haina usajili na imekuwa inalaza wagonjwa chini.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zahanati hiyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani Mbeya, Dk.Seif Mhina, alisema yeye pamoja na wakaguzi wa hospitali ngazi ya mkoa, walitembelea zahanati hiyo, Desemba 22, mwaka jana, wakiwa wameongozana na maofisa usalama wa mkoa na kujionea hali halisi.
Dk. Mhina alisema timu hiyo ilikwenda kuhakiki hati ya usajili, mazingira, watumishi, jengo linalotumika pamoja na huduma zinazotolewa katika zahanati hiyo bubu.
Kwa mujibu wa Dk.Mhina, baada ya kuihakiki, wamejiridhisha kuwa zahanati hiyo licha ya kukosa usajili, pia haina watumishi, kwani waliopo ni daktari mmoja na mhudumu mmoja wa afya.
“Zahanati ya St.Mary pia haina kichoma taka, badala yake wanatumia shimo la takataka ambalo limejengwa hivi karibuni. Vile vile wagonjwa wanalazwa chini huku pia ikiwa haina kitanda cha daktari cha uchunguzi” alisema Dk.Mhina.
Alisema zahanati hiyo imekuwa ikihudumia wagonjwa wenye matatizo, ambayo yangetibiwa ngazi ya hospitali, huku pia ikiwa na dawa zinazotoka MSD, jambo ambalo ni kinyume na taratibu.
Mganga mkuu huyo alizitaja baadhi ya dawa zilizokamatwa katika zahanati hiyo kuwa ni Giving set 287, X-Pen 151 vial, Paracetamol , Ampicillines, Nifedipines,UPT, PPF, Piroxicum na Chloramphenical Injection.
Alisema tayari mmiliki wa zahanati hiyo amefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria wakati zahanati yake ya St.Mary, imefungwa ili isiendelee kutoa huduma kwa wananchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment