Monday, 11 January 2016

DK. KALEMANI ACHARUKA


SERIKALI imeitaka Kampuni ya Spencon ya Kenya, kumaliza kazi ya usambazaji umeme katika vijiji 73 vya mkoa wa Singida, ambavyo bado havijapata umeme kabla ya Mei mwaka huu.

Imesema endapo kampuni hiyo itashindwa kumaliza kazi katika kipindi hicho, itanyang’anywa vifaa vyake ili kufidia hasara itakayotokana na kuchelewa kumaliza kazi kwa mujibu wa matakwa ya mkataba.

Hayo yalisemwa juzi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, baada ya kukagua kazi ya usambazaji wa umeme kupitia mradi wa REA 11 katika kijiji cha Heka, wilayani Manyoni, mkoani Singida.

Alisema kwa mujibu wa mkataba huo, kazi ya usambazaji wa umeme iliyoanza Oktoba, 2013, katika vijiji 90, vya mkoa wa Singida, ilitarajiwa iwe imemalizika Novemba, mwaka jana. Hadi sasa ni vijiji 17 pekee vilivyopata umeme huo.

“Serikali imeipa kampuni ya Spencon malipo yake yote, hivyo kwa sasa haina sababu ya kuwachelewesha wananchi kupata nishati hii ya umeme kwa maendeleo yao. Nakuagiza meneja wa TANESCO mkoa wa Singida, simamia kazi hii usiku na mchana, ili vijiji vyote vilivyopo kwenye mradi wa RE II, viwe vimepata umeme kabla ya Mei mwaka huu”,alisema.

Aidha, naibu waziri huyo ameiagiza Kampuni ya Hainan International Ltd ya nchini Korea, inayojenga kituo mbadala mjini hapo cha kusambaza umeme wa kilovoti 400, kumaliza kazi hiyo ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.

Katika hatua nyingine, Dk. Kalemani amewataka wachimbaji wa madini mbalimbali wadogo, waanzishe vikundi na kuvisajili kisheria, ili serikali iweze kuwapatia ruzuku kwa ajili ya kuboresha shughuli zao.

“Serikali ya awamu ya tano inatambua na inathamini shughuli zinazofanywa na wachimbaji madini wadogo, wa kati na wale wakubwa, sababu kuu ikiwa ni kwamba sekta hiyo inazo fursa nyingi za ajira,” alisema.

No comments:

Post a Comment