Friday, 11 March 2016

JPM AVAMIA BoT, ASHTUKIA MCHEZO

 RAIS Dk. John Magufuli, amefanya ziara ya kushtukiza katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kuzuia malipo ya zaidi ya sh. bilioni 925.
Mabilioni hayo ni malimbikizo ya malipo, ambayo tayari yameidhinishwa kufanyika na kuagiza ulipaji wake usitishwe mara moja na kuagiza kurejeshwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kuhakikiwa.
Pia, amemwagiza Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, kufanya uhakiki na kuwaondoa watumishi wote, ambao hawana ulazima wa kuwepo kwenye taasisi hiyo.
Akizungumza na watendaji wa BoT, akiwemo Profesa Ndullu, Naibu Magavana, Wakurugenzi na Mameneja, Dk. Magufuli ameagiza kufanyika kwa uhakiki wa kina kuhusiana na malipo hayo ili kubaini iwapo walengwa waliodhinishwa kulipwa wanastahili au la.
Wakati Dk. Magufuli akishtukia na kuzuia malipo hayo ya mabilioni ya shilingi, BoT ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo hayo ambapo, tayari Wizara ya Fedha na Mipango ilishatoa idhini.
“Haya malipo yasitishwe mara moja na wizara ifanye uhakiki wa kina. Lazima tubaini kama walengwa walioidhinishwa kulipwa wanastahili ama vinginevyo,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli pia amemwagiza Profesa Ndullu kupitia upya orodha ya wafanyakazi ndani ya BoT ili kubaini iwapo waliopo wote wana ulazima wa kuwa watumishi katika benki hiyo.
Ameagiza watumishi ambao hawana ulazima, kuondolewa mara moja. BoT ina wafanyakazi 1,391.
"Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani," alisema Dk. Magufuli na kusisitiza uhakiki wa haraka ufanyike.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli ameagiza kurejeshwa kwa Kitengo cha Madeni ya Nje, ambacho awali kilikuwa chini ya BoT na baadaye kikahamishiwa Wizara ya Fedha, kirejeshwe Benki Kuu mara moja.
Hatua hiyo ya Dk. Magufuli inalenga kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.
Ziara hiyo ya Dk. Magufuli katika Benki Kuu, imefanyika wakati Tanzania ikiendelea na ugeni wa Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Truong Tang Sang, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kiserikali.
Juzi, Dk. Magufuli alimkaribisha Rais Truong, Ikulu ya Dar es Salaam, ambapo masuala mbalimbali ya ushirikiano yalijadiliwa na mikataba kusainiwa.

No comments:

Post a Comment