Saturday 16 July 2016

SHULE ZA SERIKALI ZAREJESHA MAKALI MITIHADI YA KIDATO CHA SITA

SHULE za serikali zimeibuka kidedea kwenye matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita (ACSEE) uliofanyika Mei, mwaka huu baada ya kuingiza shule sita kwenye 10 bora kitaifa.

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa Tanzania (NECTA) Dk. Charles Msonde, alizitaja shule hizo kuwa ni Kisimiri (Arusha) Tabora Boys, Kibaha (Pwani)  Mzumbe (Morogoro) na Ilboru (Arusha) na Tandahimba (Mtwara).

Msonde alisema shule nyingine zilizofanya vizuri katika 10 bora ni Feza Girls na Feza Boys (Dar es Salaam)  Alliance Girls (Mwanza) Marian Boys (Pwani) ambazo ni shule binafsi.

Alisema shule 10 zilizofanya vibaya kwenye ufaulu wa mtihani huo, shule saba zimetoka Zanzibar ikiwemo Mpendae, Ben Bella, Tumekuja, Jang'ombe, Kiembesamaki, Al-Ihsan Girls na Lumumba.

Nyingine ni Green Bird Boys (Kilimanjaro)  Tanzania Adventist (Arusha)  na shule maarufu ya Sekondari ya Azania iliyoko jijini Dar es Salaam.

Dk. Msonde alisema kiwango cha ufaulu cha matokeo hayo kwa ujumla ni asilimia 97.94 ambayo ni pungufu kwa asilimia 0.93 kwenye matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka jana yaliyokua na ufaulu wa asilimia 98.87.

Alisema licha ya kushuka huko kwa viwango vya ufaulu, ubora wa ufaulu umepanda kwa kuwa na idadi kubwa ya watahiniwa waliofaulu vizuri kwenye daraja la 1, 2 na 3.

Ubora huo umepanda hadi kufikia asilimia 93.13 kutoka asilimia 89.41 ya matokeo ya mtihani wa mwaka jana.

Dk. Msonde alisema mwanafunzi aliyefaulu vizuri kuliko wote kwenye mtihani huo ni Hassan Bakari Gwaay wa Tabora Boys aliyekua akisoma mchepuo wa sayansi-PCM.

Alisema kwenye matokeo hayo, somo lililoonekana kufaulisha vizuri ni Historia kwa asilimia 99.96 ya ufaulu huku somo la Uraia likiwa na asilimia chache ya ufaulu kwa asilimia 71.24.

Msonde alisema watahiniwa 71,551 sawa na asilimia 97.32 waliofanya mtihani huo wamefaulu kati yao wasichana ni 26,977 sawa na asilimia 98.31 wakati wavulana ni 44,574 sawa na asilimia 96.73.

Hata hivyo, alisema katika matokeo hayo NECTA imezuia matokeo ya wanafunzi 46 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kiafya zilizosababisha wanafunzi hao ama kufanya mitihani michache au kutofanya kabisa.

"Baraza la mitihani limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 46 waliokua na matatizo ya kiafya wakati wa mitihani, 10 kati yao walifanya mitihani michache wakati 36 hawakufanya kabisa," alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo watahiniwa hao wamepewa nafasi ya kurudia kufanya mtihani huo wa taifa wa kidato cha sita unaotarajiwa kufanyika Mei, 2017.

Katika hatua nyingine,  NECTA imefuta matokeo ya watahiniwa 25 waliobainika kufanya udanganyifu kwenye mtihani huo.

Alisema kati ya watahiniwa hao, 21 ni wa shule na wengine wanne ni watahiniwa binafsi ambao walibainika kutumia simu za mkononi kuwasiliana wakiwa ndani ya vyumba vya mtihani.

"Watahiniwa 25 tumewafutia matokeo yao kutokana na kujihusisha na vitendo vya udanganyifu ndani ya chumba cha mtihani.

"Wengine tuliwakamata wakiwasiliana kwa SMS ili kusaidiana majibu ya maswali ya mtihani husika na wengine waliingia na karatasi zenye notisi za somo husika," alisema Dk. Msonde.

Aidha, alitumia fursa hiyo kufafanua kuwa madai ya mtihani huo kuvuja ni uzushi mtupu na kuwa NECTA ipo makini kuhakikisha usiri kabla ya mitihani, wakati wa mitihani na baada ya mitihani.

Alisema wananchi wanatakiwa kuendelea kuwa wadau wa NECTA kwa kutoa taarifa za udanganyifu wa mitihani kabla, wakati na baada ya mitihani ya taifa ili wahusika wadhibitiwe kwa mujibu wa sheria.

Kwenye mtihani huo uliofanyika Mei mwaka huu, kati ya watahiniwa 74,896 waliosajiliwa, watahiniwa 73,940 pekee sawa na asilimia 98.72 ndiyo waliufanya. Watahiniwa 956 (asilimia 1.28) hawakufanya mtihani huo licha ya kujisajili.


MATOKEO YA UALIMU

Katika hatua nyingine, NECTA imetangaza matokeo ya mtihani wa ualimu wa daraja A ngazi ya cheti na mtihani wa stashahada ya ualimu wa sekondari uliofanyika Mei, mwaka huu.

Dk. Msonde alisema kwenye mtihani wa ualimu daraja A, watahiniwa 10,747 sawa na asilimia 99.81 ya waliofanya mtihani, wamefaulu.

Alisema matokeo ya stashahada ya ualimu yanaonyesha kuwa watahiniwa 337 sawa na asilimia 84.46 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Dk. Msonde alisema kati ya hao, wasichana ni 72 sawa na asilimia 74.23 na wavulana ni 265 sawa na asilimia 87.75.

Aidha, alisema NECTA imemfutia mtahiniwa mmoja wa mtihani wa ualimu daraja A baada ya kumbaini kuwa alitumia njia ya udanganyifu kwenye kujibu mtihani huo.

KUGHUSHI VYETI

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Dk. Msonde alisema udanganyifu wa aina yoyote ukiwemo wa kughushi vyeti ni kinyume na sheria za nchi na kwamba wahusika wanaomiliki vyeti bandia wajitokeze mapema kabla ya kubainika.

Alisema kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, NECTA wana uwezo wa kubaini vyeti vyote bandia ndiyo sababu kumekua na ongezeko kubwa la wahalifu wa masuala hayo nchini.

"Kuanzia mwaka 2008, tulianza kutoa vyeti vyenye picha ya mtahiniwa ni moja ya njia za kupambana na kughushi vyeti hivyo tutaendelea na udhibiti kadri tuwezavyo," alisema.

Aliwataka waajiri, watumishi kuhakiki uhalisi wa vyeti vya watumishi wao ili wawe salama dhidi ya mkono wa dola kwa sababu NECTA wako macho wakati wote kuwasaka wahalifu wa vyeti.

No comments:

Post a Comment