Friday, 11 March 2016
VIETNAM KUMWAGA WAWEKEZAJI NCHINI
RAIS wa Vietnam, Truong Tan Sang amesema atafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anawavutia wawekezaji wa nchi yake, kuwekeza Tanzania katika maeneo huru ya ukanda maalumu ya kiuchumi.
Troung, aliyasema hayo jana, wakati wa ziara yake alioifanya kwenye Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya Uwekezaji (EPZA), ambapo alisema hakuna mwekezaji wa kutoka Vietnam aliyekuja kuwekeza kwenye maeneo hayo.
Alisema ukiondoa kampuni moja ya mawasiliano kutoka Vietnam ya Halotel, hakuna kampuni nyingine iliyowekeza Tanzania, hivyo ni wakati wa yeye kuwashawishi wawekezaji wengine waje Tanzania.
“Ninakubaliana na maamuzi ya Tanzania katika harakati zao za kuelekea kwenye mapinduzi ya viwanda. Ninaamini uamuzi wa kuanzia mamlaka hii (EPZA) ni hatua madhubuti ya kwenda kwenye mapinduzi ya viwanda,''alisema.
Aliongeza: “Naamini kwa kuwekeza kwenye ukanda huru wa kiuchumi, Tanzania itasogea zaidi, sio kwa soko la ndani pekee, bali kwa jumuia nzima ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla,'' alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema serikali hivi sasa inashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha inaboresha miundombinu iliyoko kwenye maeneo ya ukanda maalumu ya uchumi.
“Ningependa kuwashawishi wafanyabiashara wa Kivietnam, kuja nchini kuwekeza kwa kuwa kuna fursa nyingi za kiuwekezaji ndani ya EPZA,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Joseph Simbakalia, alisema katika eneo la ukanda huru wa kiuchumi wa Benjamin Mkapa, vipo viwanda 20, huku 11 kati ya hivyo ndivyo vinavyofanyakazi.
Majaliwa ainadi Tanzania
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewahakikishia wawekezaji kutoka Vietnam kuwepo kwa fursa za uwekezaji hapa nchini.
Majaliwa alisema hayo katika kongamano la ujumbe wa Rais Troung na wadau wa uwekezaji kutoka nchini humo, ambao wanatarajia kufanya ziara ya siku nne, wakitazamia fursa za uwekezaji nchini.
“Nchi yetu ina mazingira mazuri ya uwekezaji, usalama wa kutosha na pia kuna uhahika wa soko kwani ipo mikataba ya kikanda ya kukuza masoko katika nchi wanachama kama EAC na SADC kwani, katika nchi hizo kuna watu zaidi ya milioni 300,” alisema.
Alisema serikali imekuwa ikiboresha mazingira ya uwekezaji nchini na hivyo imechangia ongezeko la wawekezaji.
Majaliwa alisema serikali imekuwa ikiboresha sheria na kuimarisha ushirikishwaji wa wadau wa sekta binafsi, lengo likiwa ni kuchochea mazingiraya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa pamoja na kukuza kipato cha kila mtanzania.
Hata hivyo, Majaliwa aliipongeza kampuni ya VIETTEL Tanzania Ltd, kutoka Vietnam, ambayo imewekeza katika sekta ya mawasiliano kwani imewasaidia Watanzania wengi wa vijijini kupata mawasiliano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment