Monday, 21 November 2016

SAKAYA KUMLIPUA MAALIM SEIF


NAIBU Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya, ameamua kukata mzizi wa fitina kwa kuweka bayana fitna za kisiasa zinazofanywa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Magdalena amesema amefikia uamuzi huo baada ya kubaini mbinu chafu zinazotumiwa na Maalim Seif kwa lengo la kukichafua na kukivuruga chama hicho.

Amesema udikteka wa Maalim Seif unaendelea kukitafuna chama hicho kutokana na kuendelea kwake kukataa kufuata katiba na sheria na  kukiendesha chama kama mali yake binafsi.

Aidha, amemtaka kiongozi huyo kutambua jinamizi la kuzuiwa kwa ziara zake, linatokana na uongozi wake kukiuka kanuni na taratibu huku akimtaka kukubali kufanyakazi kwa kushirikiana na viongozi wengine kwa kuwa hana uwezo wa kufanya kazi peke yake.

Akizungumza na Uhuru, jana, Magdalena alisema anamshangaa Maalim Seif kwa kukataa kufanyanaye kazi wakati kwa mujibu wa kanuni za chama, yeye ndiye mwenye wajibu wa kuratibu na kuandaa ziara na mikutano ya viongozi wakuu wa chama hicho Tanzania Bara.

“Kesho nitazungumza na nitajibu hoja zake zote za kifitina kwa kuwa anataka kuendelea kuendesha chama kwa siasa chafu ili kutimiza lengo lake la kuua chama upande mmoja. Namshauri tu, mimi ni sawa na maji, usiponioga utaninywa. Ninayo mamlaka kikanuni, hususan katika kuandaa ratiba za ziara na mikutano ya viongozi,”alisema.

Aliongeza: “Kinachoshangaza, anafanya ziara Tanzania Bara kwa maslahi ya chama, sasa kuna haja gani ya kukataa kushirikiana na viongozi wengine? Kuna wakati busara zinahitajika zaidi kuliko maamuzi yasiyo na tija. Hakuna wa kumzuia Maalim Seif kufanya ziara, afuate taratibu ndani ya chama na nje.”

Alisema ni muhimu kwa Maalim Seif kutambua kuwa, serikali imezuia mikutano ya vyama vya siasa, kuendelea kwake kushawishi wanachama kukusanyika bila kufuata taratibu, ni kutaka kukichafua chama hicho kwa siasa zisizo na tija.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi lilizuia mkutano uliotarajiwa kuhutubiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, katika  Chuo cha Stella Maris (Stemmuco), mkoani Mtwara.

Taarifa ya CUF ilidai kuwa, mkutano huo ulilenga kukagua shughuli za chama, kupata maoni ya wanachama pamoja na mapendekezo ya namna ya kuboresha utendaji wa chama kwa ngazi za chini.

No comments:

Post a Comment