MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametangaza kuwa ataanza kuwastaafisha kwa manufaa ya umma, wakuu wa idara na watendaji wasiotimiza wajibu wao mkoani humo, huku akidai kuwa katika ofisi yake, wakuu wa idara wanaowajibika kikamilifu ni wanne kati 120.
Aidha, amesema kuwa daima haogopi kutumbuliwa jipu kama wengi wanavyomuombea na kwamba, yuko tayari kugombana na mtu yeyote kwa ajili ya kuwatetea wananchi.
Amesema tayari amewasiliana na ngazi za juu za serikali, ili kuona uwezekano wa kuwapunguza watumishi hao, ikiwa ni pamoja na kuwastaafisha kwa manufaa ya umma.
Akizungumza na watumishi wa halmshauri hiyo, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na wabunge wilayani Temeke, jana, Makonda alisema hayuko tayari kumvumilia mtendaji yeyote, ambaye hawajibiki ipasavyo katika kutatua kero za wananchi.
“Watu hawawajibiki. Wanakula tu mishahara, ambapo katika bajeti yetu ya shilingi bilioni 600, ni shilingi bilioni 100, tu ambazo zinaelekezwa kwenye sekta ya maendeleo. Shilingi bilioni 400, zinaishia kuwalipa mishahara na mambo mengine, huku wananchi wakiendelea kuteseka na changamoto,”alisema Makonda.
Alisema wao watendaji, ambao hawana ubunifu na wengi wamekuwa wakijitetea kuwa, hawana bajeti au hawajapata bajeti hizo bila kubuni njia za kutatua changamoto za wananchi.
“Hatuwezi kwenda kwa namna hii. Tutawajibishana tu na tutatumia njia za kuwawajibisha, ikiwemo ya kuwastaafisha kwa manufaa ya umma,”alisema Makonda.
Aliongeza: “Mimi siogopi kutumbuliwa jipu na niko tayari kukosana na kila mtu huku nikitetea wananchi wangu. Siwezi kuvumilia kuona wakuu wa idara na watumishi wa umma wakikaa ofisini bila kuwajibika.”
“Ninataka uwajibikaji, kuanzia serikali ya mtaa hadi idara. Kila mtu awajibike kwa nafasi yake. Atakayeshindwa, ajiondoe la sivyo tutamstaafisha au kumpunguza. Watendaji wasiowajibika wajihesabie kuwa wana bahati mbaya ya kuwa viongozi katika mkoa huu,”alisema Makonda.
Akiwasilisha ripoti ya wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, alisema wamejipanga kikamilifu, hususan katika kukabiliana na kero za wananchi, kusimamia ukusanyaji wa mapato na kumaliza changamoto ya madawati, ambapo hivi sasa wanashughulikia changamoto ya vyumba vya madarasa na uhalifu.
No comments:
Post a Comment