Monday, 21 November 2016

KESI YA VIGOGO 11 TRL KUANZA DESEMBA 5



KESI ya matumizi mabaya ya madaraka, inayowakabili vigogo 11 wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, itaanza kwa usikilizwaji wa awali Desemba 5, mwaka huu.

Kisamfu na watendaji wengine wa TRL, walipanda kizimbani jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Maghela Ndimbo, akishirikiana na Wakili wa taasisi hiyo, Max Ali, walidai shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo kwa usikilizwaji wa awali.

Hata hivyo, upande wa utetezi uliomba usikilizwaji wa awali wa shauri hilo, uahirishwe kwa sababu nakala ya maelezo hayo wamepatiwa mahakamani hapo, hivyo wanahitaji muda wa kujiandaa na washitakiwa wa tano na wa 10 mawakili wao hawapo.

Mawakili wa upande wa Jamhuri hawakuwa na pingamizi juu ya ombi hilo, hivyo Hakimu Victoria aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 5, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa shirika hilo, Jasper Kisiraga, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomwiles, Mhandisi Mkuu, Mathias Massae na Kaimu Mhandisi Mkuu, Muungano Kaupunda.

Pia, wamo Mhandisi Mkuu, Paschal Mfikiri, Mhandisi wa Karakana, Kedmon Mapunda, Kaimu Mhandisi wa Mawasiliano, Felix Kashaigili, Mkuu wa Usafirishaji wa Reli, Lowland Simtengu,  Mkuu wa Michoro, Joseph Syaizyagi na  Kaimu Meneja Mkuu wa Usafirishaji, Charles Ndenge.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka tisa ya matumizi mabaya ya madaraka na kutumia nyaraka za uongo kwa nia ya kumdanganya mwajiri.

No comments:

Post a Comment