MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema haimuogopi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), ambaye anakabiliwa na kesi ya uchochezi.
Hatua hiyo, inatokana na Mahakama hiyo Novemba 3, mwaka huu, kutoa amri ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo kutokana na mahudhurio yake kutokuwa mazuri na upande wa Jamhuri kushindwa kuitekeleza.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliyasema hayo jana, wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo kwa kutajwa na Lissu kuhudhuria.
“Mahakama haimuogopi mshitakiwa wa nne (Lissu) na wala haitamuonea, labda upande wa Jamhuri ndio unamuogopa kwa kushindwa kumkamata wakati ilitolewa hati ya kukamatwa kwake,” alisema Hakimu Simba.
Awali, kabla ya Hakimu Simba kueleza hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, alieleza kuwa Novemba 3, mwaka huu, mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa Lissu na kwa kuwa yuko mbele ya mahakama, labda upande wa utetezi au yeye mwenyewe aeleze kwa nini dhamana yake isifutwe.
Akitoa maelezo juu ya hilo, Wakili Peter Kibatala, anayemtetea Lissu, alidai mshitakiwa huyo ametii amri ya mahakama kwa kuhudhuria shauri, kwa kuwa dhumuni la dhamana ni kuhakikisha mshitakiwa anakuwepo mahakamani pale kesi inapotajwa.
Hata hivyo, Hakimu Simba alisema hiyo siyo mara ya kwanza kwa mshitakiwa kutokuwepo mahakamani, ambapo Wakili Kibatala alieleza kuwa Novemba 3, mwaka huu, mdhamini wake alikuwepo kwa mujibu wa masharti ya dhamana na sheria.
Kibatala alidai mshitakiwa Lissu ni wakili, hivyo alikuwa katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Bunda, ambayo ina maelekezo ya muda wa kuisha.
Wakili wa Serikali, Mwita alidai mshitakiwa huyo kwa kuwa ni wakili, anajua taratibu za kufuata iwapo hafiki mahakamani, kwani alipaswa kutoa taarifa kwa kuandika barua.
“Tunaomba mahakama iheshimiwe na kwamba jukumu la kumfutia dhamana ama la, bado linabaki kwako mheshimiwa,” aliomba.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Hakimu alimhoji wakili wa serikali na mahojiano hayo ni kama ifutavyo:
Hakimu: Siku ya kutoa hati ya kukamatwa si ulikuwepo na uliitia saini?
Wakili: Ndio.
Hakimu: Ulimkamata lini mshitakiwa?
Wakili: Upande wa Jamhuri huwa hatumkamati mtuhumiwa ila tunapeleka hati kwa wahusika ili wamkamate
Hakimu: Upande wa Jamhuri kwa hilo hamuonyeshi kudharau amri ya mahakama kwa kutomkamata mshitakiwa? Sijui nyie mnamuogopa au mnadharau mahakama?
Kutokana na hilo, Wakili wa Serikali aliomba radhi kwa kitendo cha kutomkamata Lissu.
Baada ya hapo, Hakimu alimtaka Lissu asimame na kuileza mahakama, ambapo mshitakiwa huyo alidai hana nia ya kudharau mahakama wala kuikimbia kesi hiyo.
Alidai mara ya kwanza alipelekwa nchini Ujerumani katika mazingira ya dharura na aliporudi, baada ya siku mbili alipangiwa kwenda kuendesha kesi ya uchaguzi na aliandika barua mahakamani hapo akiomba mashauri yanayomkabili yaahirishwe hadi Novemba 16, mwaka huu.
“Novemba 3, mwaka huu, nilikuwa katika kesi ya uchaguzi na ilielekezwa iishe kabla ya Novemba 18, mwaka huu. Sina nia ya kudharau mahakama na nilitoa taarifa,” alidai.
Hakimu alisema hakuna taarifa yoyote iliyomfikia na kwamba, mshitakiwa huyo ndiye anayesababisha wafike katika mgogoro huo, ambapo kwa hadhi yake, itaonekana katika jamii kwamba anaogopwa.
“Mahakama hatukuogopi, labda upande wa Jamhuri unakuogopa kwa kushindwa kukukamata. Tunataka kutengeneza mfumo wa kuheshimu taratibu na sheria.
“Sisi hatukuogopi na wala hatutakuonea, kuna hati ya kukamatwa, lakini upande wa Jamhuri haujakukamata,” alisema hakimu huyo na kuongeza kuwa, mahakama lazima iwe kali kwa wale wasiofuata taratibu zake.
Baada ya kueleza hayo, Wakili Kibatala alielezea kuondoa nia ya kukata rufani, kupinga uamuzi uliokuwa umetolewa na mahakama wa kutaka washitakiwa kusomewa shitaka la kwanza na la tano.
Wakili Mwita alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 20, mwaka huu, kwa kutajwa na alitoa onyo kwa Lissu na kusema dhamana za washitakiwa zinaendelea.
Mbali na Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, ambalo lilifungiwa na serikali kwa muda usiojulikana, Simon Mkina, mwandishi Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Lissu na wenzake, wanadaiwa kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi kupitia gazeti la Mawio, zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’
No comments:
Post a Comment