Monday, 21 November 2016

MACHALI ABISHA HODI CCM, ASEMA ANAVUTIWA NA UTENDAJI WA RAIS MAGUFULI

ALIYEKUWA Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR Mageuzi), Joseph Machali ameamua kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akieleza jinsi anavyovutiwa na kasi ya utendaji ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Aidha, Machali, ambaye hivi karibuni alijiunga na chama cha ACT-Wazalendo, akitokea NCCR-Mageuzi, amesema hakuna chama chenye matumaini kwa sasa zaidi ya CCM.

Akizungumza na Uhuru, jana, Machali, alithibitisha kuhamia CCM na kueleza kwamba, anaridhishwa na utendaji wa serikali katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Mbunge huyo wa zamani, aliyeshindwa kurejea bungeni katika uchaguzi wa mwaka jana, alisema anachosubiri kwa sasa ni kukabidhiwa kadi ya uanachama.

Alisema ni kweli ametubu na kuhamia CCM kutokana na kuvutiwa na ufanisi wa Chama katika kuleta mabadiliko ya maendeleo na kusisitiza kuwa, hakuna chama kingine mbadala.

Machali alisema amekuwa akiombwa kwa muda mrefu kurejea NCCR-Mageuzi, ambako alikitumikia chama hicho kwa muda mrefu, lakini ametafakari na kuona hakuna jipya.

Alisema ni ajabu na aibu kwa watu makini na wenye kuhitaji mabadiliko ya kweli, kuacha kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano .

“Naamini katika siasa za upinzani hapa nchini, nikiwa nimepiga kelele na kupinga siasa za kifisadi zilizoitawala nchi, niliyepinga pia ufisadi uliokuwa umeitawala serikali huko nyuma kwa nguvu na uwezo wangu wote, nikishirikiana na wapinzani wenzangu, ninaamua kujiunga na watu wanaoonyesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi yetu ya Tanzania,”alisema.

Aliongeza kuwa watu wenye mwelekeo na dhamira ya kuijenga nchi kwa maendeleo endelevu ni jamii ya Rais Magufuli, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa na watendaji wake.

Machali alisema mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Magufuli na baadhi ya wasaidizi wake, kupitia katika hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya ufisadi uliokuwa umeigubika nchi, ni hatua nzuri na  inatosha kwa mtu yeyote makini kufanya uamuzi wa kumuunga mkono au kutomuunga mkono.

“Ninaposoma rekodi yangu enzi nikiwa mbunge (Hansard) na kabla ya kuwa mbunge, ni kwamba nilipinga mno wizi na ufisadi wa kila aina. Nilipinga matumizi ya fedha serikalini yasiyo ya lazima na yasiyo na tija kwa taifa (rejeeni hotuba yangu ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, nikiwa Waziri Kivuli wa wizara hiyo mwaka 2014/2015 na 2015/2016). Vilevile bila kusahau hotuba zangu mbalimbali bungeni na nje ya Bunge,”alisema.

Mbunge huyo alisema kwa kushirikiana na wapinzania bungeni, enzi hizo, walishauri na kupinga ufisadi wa kila aina na kuitaka serikali kufanya mambo yenye tija kwa taifa na sasa kila mwenye macho anaona hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano.

Machali alisema miradi kama ya ujenzi wa reli, ununuzi wa ndege mbili na mipango ya kununua ndege zaidi kama njia ya kulifufua shirikia la ATCL, ni mambo yaliyokuwa yakipigiwa kelele na wapinzani na sasa yanafanyika, hivyo wenye dhamira ya dhati ya kuona nchi ikipiga hatua, kamwe hawawezi kubeza mambo hayo bali kuyaunga mkono.

“Wale tuliosema na kupiga kelele kwamba serikali ni dhaifu katika kuchukua hatua kwa watu wenye dhamana walioonekana kufanya vibaya katika nafasi zao, leo tunaona kumekuwepo na kasi nzuri. Hata hivyo, leo hii  upinzani umepoteza mwelekeo kwa sababu unapingana na kile ulichokihubiri nchini," alisema.

Mbunge huyo alisema agenda ya kupinga ufisadi siyo ya upinzani tena bali ya JPM na CCM yake au yao. Alisema wapinzani wamegeuka kuwa watu wanaokataa yale waliyoyasimamia na kuyahubiri huko nyuma, hivyo sio uungwana bali aina mpya ya ufisadi nchini na usaliti kwa agenda zao.

Alisema kwa wapinzani wa kweli walioonyesha kupinga kwa nguvu zote ufisadi ulioiumiza nchi na kumaanisha yale waliyoyahubiri na kuwaaminisha watu, wanao wajibu wa kuacha tabia ya kuwa vigeugeu kwa mambo waliyoyaamini na kuyahubiri.

“Kutofanya hivyo ni mwendelezo wa ufisadi kwa maslahi binafsi. Ni nani asiyeona kwamba serikali ya awamu ya tano inafanyia kazi mambo mengi tuliyoyapigia kelele? Au tunajifanya kutokukubali ukweli unaoishi kwa ule msingi wa upinzani wa Tanzania kwamba, tukimuunga mkono mtawala, kamwe hatutapata kuaminiwa na wapiga kura nchini,”alisema.

Machali alisema taifa  haliwezi kuendelea kwa kuwa na siasa za kutokukubaliana na ukweli unaoishi, hivyo kama dhamira ya kila mtanzania, ikiwemo wapinzani ni kuona nchi inaendelea,  hakuhitaji kuwa na watu wa kupingapinga hata yaliyo mema bali kuyaunga mkono.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeonyesha njia katika  mambo mengi na inastahili kuungwa mkono, kwa kuwa safari anaamini hata yale yanayoonekana kutofanyiwa kazi, na ambayo yalishindikana huko nyuma, serikali iliyoko inaweza kuyafanyia kazi.

“Daima ninaamini katika  yale ninayoyaamini pasipo kufungwa na ukada, bali kuangalia ukweli ni upi. Hata kelele wanazopiga baadhi ya watu kwamba, maisha yamekuwa magumu, ni propaganda tu kwa sababu hakuna uhusiano wa maisha magumu na suala la kudhibiti wapiga dili wa fedha na mali. Uchumi imara hauwezi kujengwa kwa kuruhusu ubadhirifu wa fedha na mali za umma au hata za mtu mmoja,”alisema.

Alisema kwa sasa nchi inasukwa upya, hivyo ni lazima wainzani kuunga mkono viongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa mema wanayoyafanya na kuwashauri kurekebisha machache na kuacha siasa nyepesi za kutaka kuona mazuri ni yale yanayofanywa na wapinzani.



OLE SENDEKA ANENA

Akizungumzia uamuzi huo wa Machali, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema haoni sababu kwa nini asipokelewe ndani ya Chama.

Ole Sendeka alisema mara baada ya kusoma taarifa hizo za Machali kujiunga na CCM kupitia kwenye mitandao ya kijamii,aliwasiliana naye kwanza ili kujua ukweli wa jambo hilo.

"Ni kweli amenithibitishia kwamba hayo yaliyoko kwenye mitandao ni yake na ameamua kwa hiyari kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli,”  alisema Ole Sendeka.

Aliongeza kuwa wanaheshimu uamuzi wake na kwamba, katiba na kanuni zitafuatwa katika kujadili maombi ya wanachama kutoka upinzani wanaojiunga na CCM kabla ya kuchukua uamuzi.

"Ninamfahamu vizuri Machali, ni mtu aliyekuwa na msimamo (bungeni). Taratibu zipo, sioni kwa nini asipokelewe. Anachopaswa kufanya ni kuomba kujiunga na CCM, vikao husika vitamjadili na kumpokea," alisisitiza Ole Sendeka.

ACT-WAZALENDO YAMTAKIA HERI

Ofisa Habari wa chama cha ACT-Wazalendo, Abdalla Hamisi, alisema wameusoma uamuzi huo wa Machali kupitia kwenye mitandao ya kijamii na kwamba hawana kinyongo naye.

"Tumejitahidi kumtafuta kwa kumpigia simu ili kuthibitisha kama aliyoyasema ni kweli, lakini kwa bahati mbaya hapokei simu zetu.

"Lakini kama kweli ameamua, tunaheshimu uamuzi wake na tunamtakia kila la heri huko aendako,"alisema Abdalla.

Aliongeza kuwa kuwepo katika chama ni imani ya mtu, halazimishwi kuwa sehemu, ambako anaona yuko tofauti nako.

No comments:

Post a Comment