Friday, 11 March 2016
WAZIRI AFUNGA MOCHWARI, JIPU LA MKURUGENZI LAIVA
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, amefunga chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufani ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani.
Amempa hadi leo mchana, Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba, kutoa maelezo kwa maandishi, kueleza kwanini asitumbuliwe jipu na kung’olewa kwenye nafasi hiyo kutokana na kufifia kwa maendeleo ya Hospitali ya Tumbi.
Pia, amepiga marufuku kuanzia sasa shirika hilo kuingilia mapato na matumizi ya fedha za Hospitali ya Tumbi na kuwaagiza viongozi na watumishi wa hospitali hiyo kupanga wenyewe.
Dk. Kigwangala ametoa maagizo hayo jana, wakati alipofanya ziara ya kushtukiza hospitali hapo na kukuta mambo mengi hayaendi sawa, hivyo ikamlazimu kuingilia kati.
Alianza kwa kushtushwa na hali ya mochwari hospitalini hapo, ambapo alitangaza kuifunga na kutoa siku tatu kufanyiwa maboresho, ikiwemo kununua mashine za kisasa.
“Kwa sasa hospitali inaendeshwa endeshwa tu bila mwelekeo, hakuna anayetazama wala hakuna mikakati. Madaktari hawana msaada na hili haliwezekani likaachwa, ni lazima tuangalie mwarobaini wa kutatua matatizo haya,” alisema Kigwangala.
Kuhusu Mpemba, Dk. Kigwangala alisema mkurugenzi huyo anatakiwa kutoa maelezo ya kina na ya msingi ya kwanini asiondolewe katika wadhifa huo wakati hastahili kuendelea kuongoza.
“Atoe maelezo ya kueleweka kwani hali niliyoiona hapa haifai. Hospitali haifai, hali ya chumba cha kuhifadhia maiti haifai, chumba cha upasuaji kama stoo, yaani yeye ni Mungu mtu kwa kweli hili haliwezi kuvumilika,” alisema.
Alisema tatizo kubwa hospitalini hapo ni utawala, hali inayosababisha kuvuruga msingi na ukuaji pamoja na utoaji wa huduma.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, kutafuta namna bora ya kupata ushauri utakaojenga mahusiano mazuri ya kiutawala ili kufahamu sekretarieti ya mkoa, ofisi ya mkoa na hospitali yenyewe wana mahusiano ya namna gani ya kiutendaji.
Alisema hospitali hiyo inapaswa kujiendesha na kuwa na mbinu mpya za kuiendesha, pasipo kuwa tegemezi kwa serikali kama ilivyo kwa hospitali za Rufaa za Muhimbili na Mbeya.
Alimwagiza Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Peter Datan, kuangalia vipaumbele na mahitaji ya watumishi katika matumizi ya fedha za makusanyo, pasipo kutegemea maelekezo ya shirika hilo ambalo linawayumbisha.
Alisema tatizo la dawa, mifuko ya damu na vifaa tiba, linatakiwa kutatuliwa kwa haraka pamoja na motisha za watumishi ili waweze kufanyakazi kwa morali, kuliko ilivyo sasa, matatizo hayo kuwekwa kando na kuangalia masula yasiyo ya tija.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment