Friday, 11 March 2016

DK, ASHATU KIJAJI: HATUTASHINDWA KUKUSANYA KODI




SERIKALI imesema haishindwi kukusanya kodi na mapato mbalimbali ili kuliwezesha Taifa kuwa na bajeti inayojitegemea bila utegemezi wa nchi wahisani.
Imesema kulingana na mikakati bora ya ukusanyaji kodi na mapato iliyoko na inayoendelea kubuniwa, kamwe serikali haitashindwa kukusanya sh. trilioni 22, kwa mwaka, kama ilivyo bajeti ya serikali ya mwaka huu.
Imesema lengo ni kuhakikisha kuwa inakuwa na bajeti inayojitegemea.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema hayo jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa uboreshaji ukusanyaji wa kodi na mapato, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Norway.
Alisema katika kipindi cha miezi mitatu, Tanzania haijawahi kukusanya chini ya kiwango na mpango uliopo ni kuhakikisha kwamba, wanawafikia walipa kodi wote nchini.
“Hatushindwi kukusanya sh. trilioni 22 kwa mwaka, kama ilivyo bajeti ya mwaka huu, tunaweza. Nia tunayo na uwezo huo tunao. Kikubwa ni wananchi kutuunga mkono na kutambua umuhimu wa kulipa kodi,” alisema.
Alisema nia ya serikali ni kuwa na bejeti  ya taifa inayojitegemea, hivyo  wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekuwa wakiimarisha usimamiaji wa vyanzo vya mapato na kodi kwa kutekeleza mikakati mbalimbali muhimu.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mpango huo, Dk. Ashatu alisema katika kuufanikisha, Norway imeipatia Tanzania, Dola za Marekani milioni tano.
Aliishukuru Norway kwa ufadhili huo unaotekelezwa kupitia Mamlaka ya Mapato ya Norway (NTA) na TRA na kwamba, nchi hiyo imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuimarisha ukusanyaji wa kodi hapa nchini.
“Serikali yetu na Norway zimekuwa zikitia saini mikataba mbalimbali katika nyanja ya ukusanyaji mapato. Mpango wa kwanza wa uboreshaji ukusanyaji mapato umemaliza Desemba, mwaka jana,” alisema.
Alisema mpango huo utasaidia TRA, kuimarisha mikakati yake ya ukusanyaji wa kodi, kuongeza elimu kwa walipa kodi na kwa wananchi kulipa bila kushurutishwa.
“Fedha hizi zilizotolewa na Norway, zitatumika vizuri ili zisaidie kutufikisha katika lengo letu la kukusanya mapato makubwa yatakayoliwezesha taifa kuwa na bajeti inayojitegemea,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen, alisema amefurahishwa kuzindua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo katika nyanja ya ukusanyaji kodi.
Alisema mkakati huo umefanyika wakati muafaka, ambapo suala la kodi linapewa kipaumbele na serikali inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
Skogen alisema: “Nipongeze mafanikio makubwa yaliyopatikana ya ukusanyaji wa kodi, kuanzia Desemba, mwaka huu.”
Aidha, alipongeza hatua madhubuti zilizofanywa na serikali ya Tanzania, katika kupambana na ufisadi na rushwa na kwamba mafanikio hayo ni mazuri.
“Nina uhakika mkakati huu tuliozindua leo, utasaidia kuboresha sekta ya ukusanyaji kodi, ambapo tokea nchi hizi mbili zilipoanza kushirikiana katika sekta hiyo, kumekuwa na mafanikio makubwa,” alisema.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kupitia uhusiano baina ya Norway na Tanzania katika sekta ya kodi, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alisema umeweza kuimarisha uwezo wa wataalamu, hasa katika kukagua mahesabu ya vyanzo vya kodi, hususan katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya madini.
Alisema katika awamu iliyopita, Norway ilitoa Dola za Marekani milioni tatu, ambapo kutokana na kuridhishwa na mafanikio yaliyopo, imeamua kuongeza msaada wake.

No comments:

Post a Comment