Friday, 11 March 2016

NGELEJA AMPA TANO MAGUFULI





MBUNGE wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja, amemmwagia sifa Rais Dk. John Magufuli kwa kuanza kutekeleza ahadi yake ya ujenzi wa daraja kubwa la kihistoria, litakalounganisha wilaya za Sengerema na Misungwi, katika Ziwa Victoria. 
Wakati Ngeleja akimpongeza JPM, Mbunge wa Jimbo la Chato, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amesema wananchi waliompigia kura za ndiyo Rais Magufuli, nyoyo zao zinafuka faraja kwani kura zao hazikupotea bure.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Ngeleja alisema daraja hilo ni la kivuko cha Busisi Kigongo, lenye urefu wa kilometa 3.2, ambalo utekelezaji umeanza kwa kutangaza zabuni ya kumpata mkandarasi mshauri. 
Alisema mkandarasi huyo atatayarisha mchoro wa daraja hilo na kutathmini gharama zake na kuishauri serikali ipate mkandarsi atakayefanya ujenzi huo. 
“Mheshimiwa Rais wetu alitoa ahadi nyingi, lakini naomba nimpongeze kwa kuanza utekeleza ji wa ahadi yake ya ujenzi wa daraja kubwa, litakalokatisha Ziwa Victoria, la Busisi- Kigongo Ferry,” alipongeza Ngeleja na kudai ujenzi huo utaweka historia ya pekee nchini.
Alieleza kuwa kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), serikali imetangaza zabuni namba AE/001/2015-16/HQ/07 ya kumpata mkandarasi huyo kwenye Gazeti la Serikali la Februari 28, mwaka huu, hivyo ni jambo la kujivunia kwa maendeleo ya taifa, likiwemo jimbo lake. 
“Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza Rais Magufuli pia kwa kuanza utekelezaji wa ahadi ya mtangulizi wake, Rais Dk Jakaya Kikwete ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kamanga-Sengerema ambao pia maandalizi yake yameanza,” alisema. 
Mbunge huyo aliwatoa wasiwasi baadhi ya wananchi wa vijiji vya Busisi na Kigongo, wanaodhani kujengwa kwa daraja hilo kutafanya vijiji hivyo vife kiuchumi kwani vitaunganika moja kwa moja na kuvutia wawekezaji wa ndani au nje kwa kuwa havitakuwa na kikwazo tena cha kupitika muda wote. 
Alifafanua kuwa kama kivuko hicho kilivyo kiungo muhimu kwa wilaya za Sengerema, Misungwi, mkoa wa Mwanza na jirani hadi nchi za Maziwa Makuu, daraja hilo ambalo litakuwa la kwanza kwa ukubwa nchini na katika nchi hizo, likikamilika litawahakikishia watumiaji wa njia hiyo usalama, wepesi na uhakika wa kufika. 
Alidai kwa mujibu wa TANROADS, serikali imetenga sh. milioni 700 kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu wa mradi huo na kuwaomba wananchi wa jimbo lake watakaoguswa na mradi huo wakati utakapofika, waupokee na kuiunga mkono serikali ili lengo na ahadi ya Dk. Magufuli itimie. 
Dk. Kalemani, aliyerithi mikoba ya Dk. Magufuli jimboni Chato, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ibondo, juzi mjini hapa, alisema uongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya JPM umemvutia kila mtanzania mwenye uzalendo, na kwamba waipe ushirikiano na kuacha siasa uchwara ili taifa lisonge mbele haraka. 
“Waliomchagua Dk. Magufuli nyoyo zenu zinafuka faraja, mnaona dhahiri kura zenu hazikupotea bure. Ambao hawakumchagua, dhamira zinawasuta kuwa taifa lingekosa mtu muhimu. Sote tujipongeze kwa kumpata kiongozi bora na shupavu, sasa ni kazi tu, siasa uchwara hazina nafasi tena,” alisema Dk Kalemani na kushangiliwa na wananchi waliokuwa wakimsikiliza.

No comments:

Post a Comment