Friday, 11 March 2016

DK SHEIN ATETA NA RAIS TRUONG WA VIETNAM





RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Truong Tang Sang, ambaye yuko nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku nne, kufuatia mwaliko wa Rais Dk. John Magufuli.
Katika mazungumzo hayo rasmi, yaliyofayika juzi, Ikulu, jijini Dar es Salaam, Dk. Shein alisema uhusiano mzuri wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Tanzania na Vietman, unatoa fursa ya kipekee kwa nchi mbili hizo kuimarisha ushirikiano katika maeneo mengine, ambayo yataharakisha maendeleo na kujenga ustawi wa wananchi wa pande mbili hizo.
Alisema kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, zina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam, hivyo alihimiza ushirikiano zaidi kati ya Zanzibar na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji wa samaki, utalii, biashara na uwezeshaji wananchi vijijini.
Dk. Shein na Rais Truong walikubaliana kuwa mapendekezo ya miradi miwili mikubwa katika kilimo na uvuvi kati ya Zanzibar na Vietnam, ambayo ni matokeo ya ziara ya Dk. Shein aliyoifanya nchini Vietnam mwaka 2012, utekelezaji wake ushirikishe pia sekta binafsi za nchi hizo.
Alisema mapendekezo ya miradi hiyo ni hatua moja muhimu kuelekea ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na maendeleo kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Dk. Shein alisema azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha usalama wa chakula na kwamba, chakula kikuu cha wananchi wa Zanzibar ni mchele, mkakati wa serikali ni kuimarisha kilimo cha mpunga.
Alisema Zanzibar ingependa kutumia uzoefu na maarifa kutoka Vietnam  kufanikisha azma hiyo.
Dk. Shein alimueleza Rais Truong kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji na kwamba, milango iko wazi kwa wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza katika sekta mbalimbali, zikiwemo kilimo, uvuvi wa bahari kuu pamoja na utalii.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Rais Truong kuwa amefurahishwa na ziara yake nchini Tanzania, ambapo imewawezesha kukutana kwa mara ya pili baada ya ziara yake aliyoifanya nchini Vietnam mwaka 2012.
Dk. Shein alibainisha kuwa, Vietnam na Tanzania ni marafiki wa kweli na daima serikali na wananchi wa nchi hizo wameonyesha kwa vitendo utayari wao wa kuzidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao.
Kwa upande wake, Rais Truong alisema ziara yake nchini Tanzania, imekuwa ya mafanikio makubwa na anaamini kuwa imefungua ukurasa mpya katika kuimarisha uhusiano wa nchi hizo.
Alibanisha kuwa mazungumzo yake na Rais Magufuli pamoja na makubaliano yaliyofikiwa, yataongeza kasi ya ushirikiano katika maeneo mbali mbali ya ushirikiano ikiwemo biashara.
Rais Truong alisema iko haja ya kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi yake na Tanzania na kuongeza kuwa, anatambua fursa nyingi za uwekezaji zilizopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Alisema mafanikio ya baadhi ya wawekezaji waliowekeza nchini yataongeza hamasa ya wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza Tanzania.
Alisema nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Zanzibar, katika sekta za kilimo, utalii, uvuvi na katika maeneo mengine na kusisitiza kuwa, Vietnam ingependa kuona ushirikiano madhubuti zaidi na Zanzibar.
Rais Troung alipendekeza kuwepo uhusiano kati ya miji ya Zanzibar na Vietnam, pendekezo ambalo lilikubaliwa na Dk. Shein.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alifuatana na mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara za Kilimo, Afya, Biashara, Uvuvi na Mifugo pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Dk. Mwinyihaji Makame.   

No comments:

Post a Comment