Thursday, 18 May 2017
VIWANDA VIKUBWA 393 VYAANZISHWA
VIWANDA vikubwa 393 vyenye mtaji wa dola za Marekani milioni 2,362 (sh. tilioni 5.198), vimeanzishwa tangu serikali ya Rais Dk. John Magufuli ilipoingia madarakani hadi kufikia Machi, mwaka huu.
Hayo yalisemwa bungeni jana, mjini hapa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, wakati akiwasilisha mpango wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mwijage alisema viwanda hivyo vilitarajiwa kutoa ajira 38,862, zilizosajiliwa na kwamba, miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na mingine katika hatua za mwisho za kuanza uzalishaji.
Alisema kati ya miradi hiyo, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesajili miradi 224, ambayo ipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Tabora, Njombe, Mbeya, Pwani, Mtwara, Iringa, Morogoro, Geita, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Lindi, Tanga, Mara, Singida na Kagera.
Pia, alisema Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZ), imesajili miradi 41 huku Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imesajili miradi 128, wakati Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), likiratibu uanzishwaji wa viwanda vidogo 1,843.
Alivitaja baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni viwanda vya chuma na bidhaa za chuma 22, ambavyo vimeendelea kuongeza uzalishaji mwaka hadi mwaka, viwanda vya saruji, vigae, nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi.
Waziri Mwijage alisema pia kuwa, vipo viwanda vya kusindika nyama, chakula, mbogamboga, matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea, dawa za binadamu, sabuni na sigara.
Waziri huyo alisema viwanda hivyo vimetoa ajira za moja kwa moja 3,660 na zisizo za moja kwa moja 2,000.
“Katika ripoti ya sensa ya viwanda ya mwaka 2013, inaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na viwanda 49,243, ambapo asilimia 85.13 ni vidogo sana, asilimia 14.02, viwanda vidogo, asilimia 0.35 vya kati na asilimia 0.5 vikubwa,” alisema.
Aidha, Mwijage alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017, serikali ilifuatilia viwanda 30, kazi iliyofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na ofisi ya Msajili wa Hazina na kati ya hivyo, 18 vinafanya kazi vizuri, vitatu vinafanya kazi kwa kusuasua na tisa vimefungwa.
Alisema ufuatiliaji huo unafanya jumla ya viwanda vilivyofuatiliwa katika kipindi cha 2015/2016 na 2016/2017, kuwa 110 na kuongeza kuwa, baadhi ya viwanda vilivyofungwa wakati wa ufuatiliaji wa 2015/2016, vilitembelewa tena mwaka 2016/2017, ili kujua maendeleo yake na hatua zilizochukuliwa na wamiliki baada ya kupata maelekezo ya serikali.
“Juhudi mbalimbali zimefanyika kushawishi wamiliki wa viwanda vilivyofungwa wavifufue na matokeo ya juhudi hizo ni pamoja na majadiliano ya kukifufua kiwanda cha Morogoro Canvas Mills Ltd (MCM), ambayo yamefikia hatua nzuri,” alisema Mwijage.
Kwa mujibu wa Mwijage, kiwanda cha MOPROCO kilichopo Morogoro, kimekarabatiwa, ikiwa ni pamoja na kufungwa mitambo yenye teknolojia mpya iliyo na uwezo wa kusindika mbegu za mafuta na kusindika mashudu baada ya kukamuliwa na wakamuaji wadogo.
Akizungumzia malengo ya wizara yake, alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018, serikali imepanga kuendeleza jitihada za kuhamasisha sekta binafsi kuendeleza viwanda vilivyopo na kuanzishwa viwanda vipya, ikiwa ni pamoja na kuwekeza nguvu kwenye viwanda vinavyotoa ajira nyingi, ikiwemo viwanda vya nguo na mavazi na ngozi.
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, aliipongeza serikali kwa kufufua viwanda, kikiwemo kiwanda cha korosho Mtwara, huku akiitaka kujenga viwanda zaidi Lindi na Mtwara, kwani ni ukombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo kwa kuwa ni maskini.
Nape alisema kuna watu wanaopigana vita ili kiwanda cha mbolea Lindi, kisijengwe na vita hiyo ni ya wakubwa, inayotaka kuwaumiza wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba, alisema mfumo wa kodi unaotumiwa sasa kwa wawekezaji sio rafiki na unachangia wawekezaji wengi kutokuja nchini kuwekeza.
Serukamba alisema kama vivutio vya uwekezaji havipo sawa na kuondolewa mara kwa mara, hakuna mwekezaji atakayekuja kuwekeza na ndio maana sera ya uwekezaji imekuwa ikipanda na kushuka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment