WAZIRI
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameagiza watumishi
watatu wa idara ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Monduli, kupandishwa
kizimbani mara moja kutokana na wizi wa fedha za halmashauri hiyo.
Wizi
huo unatokana na watumishi hao kuuza viwanja zaidi ya 200, kwa bei ya kati ya
sh. milioni mbili hadi nne, bila kuingiza fedha hizo katika akaunti ya halmashauri
hiyo.
Lukuvi
alitoa agizo hilo juzi, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Francis Miti,
kwenye mkutano wa hadhara, wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani hapa, baada
ya wananchi hao kutoa malalamiko ya kuuziwa viwanja hewa na watumishi hao wa halmsahauri
hiyo.
Watumishi
hao ni pamoja na Kitundu Mkumbo, ambaye ni Ofisa Ardhi Mteule wa wilaya hiyo,
Leonard
Haule (mpimaji wa ardhi) na Leonard Mkwavi, ambaye ni mchora ramani .
Lukuvi
alisema kuwasimamisha kazi kwa watumishi hao haitoshi, hivyo ni vyema
wakafikishwa mahakamani kwa kukiuka maadili ya watumishi wa umma pamoja na
kurudisha fedha zote za wananchi hao waliowatapeli, kwani wanatumia stakabadhi
za halmashauri.
Aidha,
aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kwa
kushirikiana na polisi katika wilaya hiyo, kufanya uchunguzi wa haraka na wa
kina kisha kuwafikisha mahakamani watumishi hao.
"Huu
ni utovu mkubwa wa nidhamu, ninaagiza uchunguzi ufanyike mara moja dhidi ya
watumishi hawa na wafikishwe mahakamani mara moja, ikiwa ni pamoja na kulipa
fedha zote walizochukua kwa wananchi," alisema.
Akipokea
maagizo hayo, Miti alisema baada ya kutambua ubadhilifu huo, aliagiza watumishi
hao kuwekwa ndani kwa saa 24 pamoja na kuwasimamisha kazi.
Alisema
uchunguzi umeanza na kwamba ukikamilika,
watafikishwa mahakamani mara moja.
Naye
Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Loota Sanare, alimuomba Lukuvi kufikisha ombi
lao kwa Rais Dk. John Magufuli, kufuta hati za mashamba 39, ambayo wawekezaji
wanayoyamiliki bila kuyaendeleza.
Alisema
wananchi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ardhi kutokana na wengi kutokuwa
na ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo na mifugo.
Kufuatia
ombi hilo, Lukuvi aliuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuhakiki mashamba yote
wilayani humo ili hati zake zifutwe na kurejeshwa kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment