Uamuzi huo ulichukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, ulioko mjini Langangabilili wilayani humo.
Mbali na uamuzi huo, Mtaka amefuta posho zote kwa wakuu wa idara na vitengo katika halmashauri zote zilizoko mkoani hapa, wanaoingia katika vikao vya madiwani, likiwemo baraza na kamati za halmashauri.
Mtaka amefikia uamuzi hup kwa madai kuwa hazina tija yoyote na kuelekeza fedha zilizotengwa zifanye kazi nyingine za maendeleo kama utengenezaji wa madawati.
Alisema alipata malalamiko dhidi ya mkurugenzi huyo kupitia wajumbe wa kamati ya fedha na mipango wa halmashauri hiyo waliofika ofisini kwake, hivyo kuamua kuitisha kikao hicho cha dharura ili kusikiliza.
Katika kikao hicho, madiwani hao walisema serikali ilitoa sh. milioni 450, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika halmashauri hiyo, lakini kazi hiyo haikufanyika na kila wanapohoji na kutoa maamuzi, amekuwa hayafanyii kazi.
“Wilaya yetu ni mpya na katika kuondoa tatizo la watumishi wa
halmashauri kuishi mbali na makao makuu ya wilaya, tuliamua kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi na tukaletewa shilingi milioni 450, lakini kila tunapohoji matumizi ya fedha hizo, hatupatiwi majibu na tunapomwagiza mkurugenzi atuletee, hakubaliani na maamuzi yetu,”alisema Kuzenza William, ambaye ni Diwani wa Kata ya Zagayu (CCM).
Walisema hata mapato ya ndani yanayopatikana hayafahamiki licha ya kuwepo kwa ushuru wa mazao mchanganyiko, ambao haulipwi na wafanyabiashara wengi, hivyo kusababisha shughuli nyingi za halmashauri kukwama na kuzua migogoro ya mara kwa isiyoisha kati ya madiwani na
ofisi ya mkurugenzi.
“Mapato ya ndani hayafahamiki kabisa kuwa ni kiasi gani cha fedha kimepatikana, maana hatusomewi na inaonekana hata ushuru wa mazao mchanganyiko wafanyabiashara hawalipi. Hii timu ya mkurugenzi inayosimamia mapato sina imani nayo,”alisema Robert Jongela, Diwani wa Lugulu (CCM).
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Daud Nyalamu, alisema madiwani wa halmashauri hiyo wanaonekana hawana maamuzi kwani waliagiza vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 320, vilivyokopwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa maabara 35, za shule za sekondari vifanye kazi, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na vingi vimeharibika.
“Tulikopa benki shilingi milioni 320, kwa ajili ya ujenzi wa maabara 35, zilizoko katika halmashauri yetu, vifaa vimenunuliwa, lakini hadi sasa vimesambazwa maeneo mbalimbali, vikiwa havifanyi kazi, vimeharibika kwani saruji imeganda na mbao zimepinda na hazifai kwa ujenzi na hii inatokana na uzembe wa mkurugenzi wetu na kila kukicha halmashauri inadaiwa hadi madiwani hatulipwi stahili zetu,”alisema.
Akizungumzia tuhuma dhidi yake, Aloyce alisema tangu ateuliwe miezi sita iliyopita, alikuta sh. milioni 126, zilizokuwa zimebaki katika ujenzi wa nyumba za watumishi na kuamua kuzichukua kwa kukopa na kujengea ukumbi wa halmashauri hiyo kwani ulikuwa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Wakati nafika katika halmshauri hii, nilikuta kati ya shilingi milioni 450, za ujenzi wa nyumba za watumishi zilikuwa zimebaki shilingi milioni 126, tulikaa na wakuu wa idara tukaamua tuzikope na kujenga ukumbi, ukizingatia tulikuwa tunaelekea uchaguzi mkuu, hivyo tungeshindwa mahali pa kukusanyia matokeo,”alisema.
Alisema licha ya tuhuma dhidi ya halmashauri hiyo, iliundwa tume kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuzichunguza, lakini hadi sasa hawajawaletea majibu.
Aliomba iundwe tume huru kutoka nje ya mkoa ili kuweza kuzichunguza tuhuma zilizotajwa na madiwani dhidi yake na ikabainika yuko tayari kuachia ngazi.
No comments:
Post a Comment