SERIKALI inakusudia kutuma timu ya wataalamu kuchunguza iwapo jengo la kituo cha pamoja cha utoaji huduma mpakani (One Stop Border Posts) katika mpaka wa Horohoro, unaozitenganisha Tanzania na Kenya, kama fedha zilizotumika zinaendana na thamani halisi ya jengo hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema hayo juzi, akiwa katika ziara ya siku moja mkoani hapa na kukagua jengo hilo lililojengwa ili kurahisisha taratibu za forodha, uhamiaji, usimamizi wa ubora wa bidhaa, ulinzi na usalama.
Profesa Mbarawa alionyesha kutoridhishwa na ujenzi wa jengo hilo, baada ya kubaini baadhi ya maeneo kuwa na nyufa na kuezuliwa.
Ujenzi huo ulifanywa na Kampuni ya Siha Enterprises ya Tanzania chini ya Mhandisi Mshauri, Kampuni ya Sai Consulting Engineers kutoka India.
Mradi wa ujenzi huo ulianza kutekelezwa Julai, 2011 na ulitarajiwa kukamilika Februari, 2014, kwa gharama ya sh. bilioni 7.3.
Fedha za mradi huo zimetolewa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB), kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo vituo vya Namanga, Holili, Rusumo na Mtukula navyo vilijengwa kwa msaada huo.
Profesa Mbarawa alisema inashangaza kuona jengo hilo kwa kipindi kifupi tangu lilipojengwa, limeanza kuchakaa na kwamba baadhi ya maeneo yanaonekana kushindwa kukamilika.
“Huu ni ubadhirifu ambao sitakubaliana nao kwa kweli. Fedha zilizotolewa na thamani halisi ya jengo hili haviendani kabisa, tayari jengo limeanza kutoka nyufa, paa limeezuliwa,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Edwin Iwato, alisema jenereta la kituo hicho ni bovu na halikuwahi kufanyakazi tangu lilipofikishwa kituoni hapo.
No comments:
Post a Comment