Tuesday, 29 March 2016

BARAZA LA WAWAKILISHI KUANZA VIKAO VYAKE KESHO




MKUTANO wa kwanza wa Baraza Jipya la Tisa la Wawakilishi la Zanzibar, umepangwa kuanza kesho kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani mjini Unguja.

Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa juzi kuwa, mkutano huo umeitishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Khamis alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na taratibu za uendeshaji wa baraza hilo, rais ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na mahali pa kufanyika mkutano wa mwanzo wa baraza jipya.

Mkutano huo ni wa kwanza baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa marudio wa rais, wawakilishi na madiwani, uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Khamis alisema kabla ya kuanza rasmi kwa shughuli za mkutano huo, kutakuwa na usajili wa wajumbe wote, ulioanza jana, zoezi ambalo litakwenda sambamba na upigaji picha kwa ajili yavitambulisho.

Aidha, Khamis alisema kabla ya kuanza kwa kikao hicho, kutafanyika mikutano ya vyama vya siasa, itakayofanyika leo.

Katibu huyo wa baraza alisema uchaguzi wa Spika wa Baraza la Wawakilishi, itakuwa shughuli ya kwanza katika kikao cha kesho na mara baada ya kuapa, naye atawaapisha wajumbe wote wa baraza hilo.

"Wajumbe wanapaswa kula kiapo cha uaminifu kabla ya kutekeleza shughuli yoyote ya baraza kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, isipokuwa wanaweza kumchagua Spika hata kabla hawajaapishwa,"alisema Khamis.


Alisema kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu, kinaweza kusimamisha mgombea wa nafasi ya Spika. Alisema mtu anayeweza kugombea nafasi ya Uspika wa Baraza la Wawakilishi, anapaswa aidha awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi au awe na sifa za kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Katibu huyo alisema hadi kufikia tarehe ya mwisho ya vyama kuwasilisha majina ya wagombea wao katika Tume ya Uchaguzi,
ni mjumbe mmoja pekee, ambaye amewasilisha jina lake na tayari tume imeshawasilisha jina lake kwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi.

Khamis alisema shughuli nyingine inayotarajiwa kufanywa katika mkutano wa kwanza wa baraza jipya ni uchaguzi wa Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Alisema wenye sifa za kugombea nafasi ya Naibu Spika ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pekee. Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, nafasi hiyo inatakiwa ijazwe katika mkutano wa mwanzo wa baraza jipya.

Kwa mujibu wa Khamis, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein anatarajiwa kulihutubia baraza hilo kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo kikatiba, katika siku itakayotangazwa baadaye na Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Alisema wajumbe wanaweza kutoa hoja kutaka hotuba hiyo ya Rais ijadiliwe katika Baraza la Wawakilishi, ingawa kwa mujibu wa Kanuni za Baraza la Wawakilishi, hotuba hiyo itajadiliwa katika mkutano wa baraza unaofuata.

Aidha, Khams alisema wajumbe wa baraza wanatarajiwa kufanya uchaguzi wa wajumbe wanaoingia katika Tume ya Bajeti ya Baraza na kwamba tume hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuidhinisha bajeti ya mwaka ya Baraza la Wawakilishi.

"Kwa kuzingatia kuwa, matayarisho ya bajeti kwa mwaka 2016/2017, yanapaswa kukamilika muda mfupi ujao, kuna umuhimu wa kufanya uchaguzi wa wajumbe watano wanaoingia katika tume hii kutoka miongoni mwa wajumbe wasio mawaziri au naibu mawaziri, ili hatimaye iweze kutafakari na kuidhinisha Bajeti ya Baraza la Wawakilishi,"alisema.

Wakati huo huo, Khamis amesema amepokea majina
ya wanachama 22 wa CCM, walioteuliwa kuwa wajumbe wa baraza hilo, kuungana na wajumbe wengine 54, waliopatikana katika uchaguzi mkuu wa marudio uliomalizika wiki iliyopita.

Katika orodha hiyo kupitia viti maalumu vya wanawake, yumo
Naibu Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM Zanzibar, Salama Aboud Talib, Mwenyekiti wa baraza lililopita, Mgeni Hassan Juma na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Bihindi Hamad Khamis.

Wengine ni Shadya Mohamed Suleiman, Salma Mussa Bilali, Mwanaidi Kassim Mussa, Panya Ali Abdalla, Zaina Abdalla Salum, Salha Mohammed Mwinyijuma, Zulfa Mmaka Omar, Lulu Msham Abdalla na  Saada Ramadhani Mwenda.

Wajumbe wengine ni Tatu Mohamed Ussi, Amina Idd Mabrouk , Choum Kombo Khamis, Mtumwa Suleiman Makame , Mwantatu Mbaraka Khamis, Riziki Pembe Juma, Viwe Khamis Abdalla, Hamida Abdalla Issa, Hidaya Ali Makame na mtoto wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Wanu Hafidh Ameir.

Wajumbe hao ambao wanatoka katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba, wamepatika kutokana na ushindi ilioupata CCM, ambapo kilishinda katika majimbo yote 54 ya Zanzibar.

Baraza hilo hadi sasa lina wajumbe 77, kati ya 88, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezka endapo mgombea wa nafasi ya spika, ambaye sio mjumbe wa baraza, atashinda na Rais wa Zanzibar, atafanya uteuzi wa nafasi 10 alizopewa na Katiba ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment