Monday, 28 March 2016
WASAFIRISHAJI NYARA WACHARUKA ARUSHA
CHAMA cha Wasafirishaji wa Nyara Nchini Tanzania (TWEA) Kanda ya Kaskazini, kimeiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuwaachia wanachama wao waliokamtwa mwishoni mwa wiki kwa tuhuma za kusafirisha tumbili hai 62 bila vibali.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Arusha Bird Traders na raia wawili wa Uholanzi, waliokamtwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakituhumiwa kusafirisha tumbili hao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa
TWEA Kanda ya Kaskazini, Othman Bhoki, alisema kukamatwa kwa raia hao wawili ni kuwarudisha nyuma wafanyabiashara wenye vibali halali vya kuvuna tumbili.
Aliwataja raia hao kuwa ni Arten Vardanian (52), Edward
Vardanian (46) na mkurugenzi wa kampuni iliyotumika kukamata tumbili hao ya Arusha Bird Traders.
Alisema wasafirishaji wa tumbili hao ambao ni Kampuni ya Arusha Bird Traders, wana vibali halali vya kufanya biashara hiyo kwa maelekezo ya tangazo la Wizara ya Maliasili na Utalii.
"Suala hili ni vyema likachunguzwa kwa kina kwani kampuni hiyo imewasilisha kibali halali cha kusafirisha wanyama hao chenye namba 29655 (Cites), kilichotolewa Februari 24, 2016, ambacho kinaisha muda wake Agosti 23, 2016,” alisema.
Aidha, kibali hicho kimeruhusu tumbili 62, kusafirishwa kwenda
nchini Armenia na kwamba, kukamatwa kwao kunaleta mkanganyiko kwani kwa mujibu wa kibali cha kukamata wanyama hao, kinaonyesha kuruhusu daraja namba
13 la kuruhusu gawio la tumbili kuuzwa nje ya nchi.
Alisema aina ya tumbili waliozuiwa wapo katika mgawo wa taifa
unaoruhusu wauzwe tumbili 5,000, kwa mwaka na wafanyabiashara na gawiwo hilo kwa daraja tajwa lina tumbili wa aina mbili, ambazo ni Vervet Monkey na Blue Monkey (400).
Alisema katika mazingira hayo, wanashindwa kuelewa ni vigezo gani alivyotumia Waziri wa Maliasiali na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, kuzuia wanyama hao kwenda nje ya nchi kwani daraja lililokatazwa kufanyiwa biashara ni la 14, ambalo linahusu wanyama wakubwa hasa wenye pembe na kwato.
Alisema kinachoshangaza zaidi wakati tumbili hao wakizuiwa
kusafirishwa huku wakurugenzi wakishikiliwa na polisi, wanachama hao wa TWEA Kanda ya Kaskazini, bado wana tumbili katika mabanda yao, ambao wanasubiri kusafirishwa nje ya nchi katika masoko mbalimbali barani Ulaya
“Tunalaani kuitwa watoroshwaji wa wanayama wakati tuna vibali vinavyoturuhusu kusafirisha wanyama hawa…tunaomba uchunguzi wa kina juu ya suala hili ili tujue hatma ya raia hao wanaoshikiliwa na polisi, maana hapa kuna mkanganyiko na hatujui Waziri Maghembe amezuia kwa
kibali gani, ni hiki tulichonacho au la,” alihoji.
Katibu wa TWEA , Said Gumbo alisema hatua ya wizara
kuzuia wanyama hao, imewaweka wafanyabiashara katika mazingira magumu kwani wanaofanya biashara hiyo ni raia wa Tanzania, ambao wanatafuta riziki kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.
Mwishoni mwa wiki, vyombo vya ulinzi na usalama katika uwanja wa ndege wa KIA, vilifanikiwa kuwanasa wafanyabiashara wawili ndugu, raia wa Uholanzi wakiwa katika harakatiya kusafirisha tumbili kwenda Armenia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment