Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwapungia waumini baada ya Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam leo Machi 27, 2016 |
RAIS Dk. John Magufuli, amewasihi
Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kushirikiana kuijenga nchi yao, badala ya
kubaguana.
Rais Magufuli alitoa wito huo jana,
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Azania
Front, Dar es Salaam, ambako alisali ibada ya Pasaka na waumini wa kanisa hilo.
Alisema Mwenyezi Mungu alimtoa mwanawe
wa pekee Yesu Kristo kuja kuikomboa dunia bila kuwabagua binadamu, hivyo na
binadamu wanapaswa kutobaguana, iwe kwa dini zao, makabila yao, mitazamo ya
kisiasa na hata rangi zao.
Rais Magufuli aliwakumbusha
Watanzania kufanya kazi
kama ambavyo vitabu vitakatifu
vinasisitiza umuhimu wa kufanya kazi na amebainisha kuwa, Tanzania yenye neema
inawezekana endapo kila mtu atazingatia kufanya kazi.
“Tukifanya kazi hatuhitaji hata
misaada kutoka nje, nchi
hii ina neema nyingi. Kwa kweli
tukifanya kazi kwa bidii
nchi yetu inapaswa kuwa inatoa
misaada kwa nchi
nyingine na sio kuomba misaada
kutoka nchi nyingine,”
alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Dk. Magufuli alisali kwenye
kanisa hilo kwa mara ya
kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ikiwa ni mara yake ya nne kusali katika
kanisa hilo hata kabla ya kuwa rais.
Aliwaomba Watanzania kuendelea
kuliombea taifa na kumwombea yeye ili afanikiwe kutekeleza jukumu kubwa na zito
la kuiongoza nchi.
Pamoja na kuongoza maombi ya kumwombea
Rais Magufuli na mkewe, Mama Janeth Magufuli, waliohudhuria ibada hiyo, Askofu Mkuu
wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, alimpongeza Rais
Magufuli kwa tabia yake ya kupenda kuhudhuria ibada na kuwasihi viongozi
wengine kufanya hivyo.
Askofu Malasusa aliuelezea ufufuo wa
Yesu Kristo kuwa jambo la kuleta matumaini, hivyo amepongeza mwelekeo wa nchi
kwa sasa na kwamba kanisa linaona matumaini kwa taifa.
No comments:
Post a Comment