ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam,
Dk. Valentino Mokiwa, ameweka hadharani mawe (majipu) yanayolikumba kanisa na
kuwataka waumini kujisafisha kwa kuwa na moyo mweupe.
Ameyataja majipu hayo kuwa ni pamoja na baadhi ya
maaskofu kuzushiana figisufigisu, wizi, ulaghai, chuki na kutukanana, hivyo
kukwamisha makanisa kusonga mbele.
Dk. Mokiwa aliweka hadharani matendo hayo yanayotishia
uhai wa kanisa jana, alipokuwa akiongoza Ibada Kuu ya Pasaka, ambayo kitaifa ilifanyika kwenye
Kanisa la St. Albans, lililoko Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, alikuwa miongoni mwa waumini waliohudhuria, ambapo aliowaonya viongozi
wa dini wanaochochea uvunjifu wa amani makanisani.
Alisema hatawafumbia macho viongozi watakaoomba wapatiwe
polisi kwa lengo la kutuliza migogoro kwenye makanisa, hivyo viongozi wa dini
watakaofanya hivyo atawaweka ndani.
Dk. Mokiwa katika mahubiri yake alisema, kuna masuala
lukuki yenye kuhusu kanisa, hivyo yanapaswa kuwekwa wazi.
"Kanisani kuna mawe (majipu) makubwa, ambayo
yanazuia kanisa kutoka pale lilipo. Kuna mashindano ya taasisi na madhehebu,
ambako watu wanakaa na kuangalia kanisa lipi kubwa, lina watu gani, askofu
gani, idadi ya shule inazomikili," alisema Dk. Mokiwa.
Alibainisha kuwa kila kipindi cha sikukuu wamekuwa
wakiangalia ya nje ya kanisa na sasa wameamua kujitazama wenyewe nyumbani.
Aliyataja majipu mengine kuwa ni maaskofu kupigana vita
kwa kila mmoja kumchimbua mwenzake na kuanzishiana figisufigisu huku wakiacha
kufuatilia maeneo yao.
“Viongozi wa kiroho wanatukanana, tumeona wachungaji nao
wakikosa utii na kukataa mahali pale walipo. Dhambi ya mapinduzi na ugumu wa
moyo, tumeona kanisani kusemana na kusingiziana," alisema.
Dk. Mokiwa alisema kwa sasa kanisani uongo umekuwa nyumbani
kwake na kumekuwa na nguvu ya makundi, jambo ambalo limekuwa likivuruga kanisa.
Aidha, alibainisha kuwa roho ya uchochezi, dhambi ya
wivu, uzushi na tabia ya chuki iko kanisani, wizi na ulaghai, jambo ambalo
limepunguza upendo.
Pia, alisema injili za kibiashara nazo ni miongoni mwa
majipu yanayotesa kanisa, kwani kuna makanisa mengi yameanzishwa kwa dhumuni la
kufanya injili za namna hiyo.
Dk. Mokiwa alisema makanisa hayo yanayofanya injili za
kibiashara, yamekuwa yakisisitiza utoaji wa sadaka ili muumini apokee miujiza.
"Mkristo anayempenda Mungu anashindwa kumuona Mungu
wake kutokana na watu waliopo kanisani. Kwa kuwa utakuta kanisa halina nidhamu,
haliheshimiani, lina mawe haya. Mawe haya ni majipu, ambayo yanalifanya kanisa
lishindwe kutoka," alisema.
Aliwataka waumini kujisafisha kwa kuwataka
kutosherehekea Sikukuu ya Pasaka ya kukufuka kwa Yesu Kristo kwa mioyo yao
iliyopita, bali kwa moyo mpya uliosafishika.
Alisema iwapo Wakristo watakuwa na mioyo myeupe, hakuna
kitakachoshindikana huku akiwakemea wale wanaoombea mabaya kanisa kwa kuwataka
washindwe.
Pia, aliyapongeza makanisa yanayokataa mawe hayo na
kuyataka yasikae kimya, bali wasaidie makanisa mengine yaliyopotea ili yarudi
na kufanya yale waliyoagizwa na Mwenyezi Mungu.
"Pasaka ya mwaka huu, Mungu anataka wote tuwe na
moyo mweupe na maombi yasiyokoma ili sote tusimame katika njia nyeupe.
"Kanisa lisiwe ni mahali ambapo halitajizungumza
lenyewe, tukatae kwa kuwa kanisa sasa limekuwa la aibu. Nayapongeza makanisa
yote yanayomuenzi Mungu na siyapongezi yale, ambayo hayamtunzi masikini, bali yanatafuta
vyombo vya habari kwa kujivua yenyewe," alisisitiza.
Katika ibada hiyo, waumini wa kanisa hilo wakiongozwa na
Askofu Mokiwa, waliwaombea watoto yatima na wale wenye wazazi, lakini wanaishi
maishi ya uyatima,
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda,
alionya kuwa hataki kusikia viongozi wa dini mkoani humu wakihitaji polisi kwenda
kulinda amani kutokana na mitafaruku baina ya waumini.
"Ni aibu kubwa sana kwa kanisa kukimbilia katika
vyombo vya dola, sisi wanasiasa tunatakiwa kukimbilia kanisani mambo
yanapotushinda. Kwani kufanya hivyo
tunamwaibisha Yesu Kristo, wale watakaomba polisi ndio watakaokuwa wa kwanza
kuwaweka ndani," alisisitiza.
Makonda alieleza namna alivyopigiwa simu na mwanamama aliyedai
kutoka kanisa lililoko Kimara, akiomba msaada wa polisi, akidai kuna watu
wanatoa rushwa kanisani.
"Nilimwambia mama kaa kimya, tunao mfumo wa
kushughulikia watu hao na hakuna mahala kwenye maandiko panasema tukishindwa
tumuite polisi," alisema.
Makonda alisema serikali inahitaji msaada wa taasisi za
dini kuisaidia katika masuala mbalimbali na sio taasisi hizo kuomba msaada wa
polisi.
"Katika mkoa huu, atakayepeleka taarifa ya kuomba
polisi ili waje kulinda amani kutokana na mitafaruku, namtia ndani,"
alisema.
Aidha, aliwaomba waumini wa dini hiyo kumwombea Rais Dk.
John Magufuli, kutokana na kazi kubwa anayoifanya, ikiwemo ya kutumbua majipu
kwa kuwa sio kazi rahisi.
Kuhusu elimu, Makonda alisema Dk. Magufuli amekubali
kutoa elimu bure na ina changamoto zake, hivyo wanapaswa kumsaidia kwa kumuunga
mkono.
Mbali na hayo, aliwaomba viongozi wa dini kusaidia
katika kuhamasisha usafi kwa kuwa kuna watu wengi hawataki kufanya usafi.
Pia, aliwaomba kumsaidia katika masuala ya ulinzi na
usalama na kuwa kwa sasa Dar es Salaam, haiko salama.
Makonda alisema juzi, polisi walifanikiwa kuua majambazi
yakiwa na mabomu maeneo ya Sea Cliff na kwamba, kwenye mpaka wa Mkoa wa Dar es
Salaam na Pwani, wamebaini kuna watoto wadogo wanafundishwa namna ya kutumia
silaha na mabomu.
Alisema baada ya kukamilika kwa siku 90, za uhakiki wa
silaha, ataongoza operesheni maalumu ili kuwakamata watu wanaomiliki silaha
kinyume na utaratibu.
WATANZANIA WAHIMIZWA
KUDUMISHA AMANI, UMOJA
KUDUMISHA AMANI, UMOJA
Katika hatua nyingine, Watanzania wametakiwa kuwa na
umoja na kudumisha amani na kuacha vitendo vya kibaguzi katika kipindi cha
Sikukuu ya Pasaka.
Wito huo ulitolewa jana na Padri Deogratius Charles wa
Parokia ya Mburahati, Dar es Salaam, wakati wa Ibada ya Misa ya Sikukuu ya kukumbuka
kufufuka kwa Yesu Kristo, ambaye alisema kwa sasa ni vyema Watanzania
wakaondokana na dhana ya ubaguzi.
Padri Charles alisema dhana hiyo imejikita sana katika
mioyo ya Watanzania wa sasa, ikilinganishwa na kipindi kilichopita na kwamba, ni dhambi kubwa na ni kikwazo
katika umoja na mshikamano uliojengwa na viongozi waasisi wa taifa.
“Mfano Magdalena alikuwa wa kwanza kushuhudia ufufuko wa
Yesu Kristo na huo ni ushuhuda mzuri kwetu binadamu kuona maisha yasiyokuwa ya
kibaguzi, hivyo lazima tubadilike na kuwa kitu kimoja,”alisema.
Alisema katika maisha ya sasa, vitendo vya kikatili
vimeendelea kushamiri, ikiwemo ukatili wa kijinsia, ambao unatakiwa kupigwa vita
kwa kuwa unazorotesha hali ya umoja, mshikamano na amani.
“Katika kipindi hiki cha kukumbuka ufufuko wa Yesu Kristo,
inatupasa tujifunze kuishi maisha ya unyenyekevu na ya upendo pasipo kuwa na
vitendo vya kibaguzi,” alisisitiza.
Aliwataka Watanzania kuliombea taifa liwe na amani katika
kipindi kigumu kilichopita cha kisiasa na kwamba, kwa sasa wanapaswa kuwa na
moyo mmoja wenye imani wa kiutu na kuacha vitendo vya kinyama.
WAUMINI MBEYA WATAKIWA
KUMUOMBEA RAIS MAGUFULI
KUMUOMBEA RAIS MAGUFULI
Kutoka
mkoani Mbeya, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Mbeya, Mhashamu Evarist Chengula, amewataka
Watanzania kumwombea Rais Dk.John Magufuli, ili wabaya wake washindwe kumzuia
katika kutekeleza majukumu yake kwa taifa.
Alisema nchi hii ina majipu mengi na serikali ya Rais
Dk. Magufuli imekuwa ikifanya kazi zake kwa uwazi bila kufichaficha mambo.
Askofu Chengula aliyasema hayo jana, wakati wa mkesha wa
Sikukuu ya Pasaka, uliofanyika katika kanisa hilo lililoko mjini Mbeya.
Alisema Watanzania leo wanaongea sana juu ya mambo ya
ufisadi na mafisadi, hivyo wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa kuwapatia kiongozi
aliyeonyesha dhamira ya dhati ya kulishughulikia donda hilo.
"Lengo la Mungu kutuletea kiongozi huyu ni
kutufanya Watanzania turudi katika mstari, ambao Mwenyezi Mungu anaupenda, ndio
maana tumekuwa tunafurahia utendaji kazi wake,"alisema Askofu Chengula.
Aliongeza kuwa anaamini hata wale wanaokamatwa wamekuwa
wanaihujumu nchi, hivyo anachokifanya Rais Dk. Magufuli katika kuchukua hatua
hizo ni kuwaonya ili wasirudie tena kufanya hivyo.
Askofu Chengula alisema kazi ya Watanzania hivi sasa ni
kuwaombea waliokuwa wanaiharibu nchi ili Mwenyezi Mungu aweze kuwasamehe na
kwamba, wasiache kuwaombea ili watubu makosa yao.
Aliongeza kuwa wengine licha ya kukamatwa, bado wamekuwa
wanatafuta jinsi ya kujinasua katika tuhuma hizo zinazowakabili.
Aliwafananisha watu wa aina hiyo sawa na Wamisri na
kwamba, Mungu anawataka hao wanaoiba mali za nchi watubu dhambi zao.
Askofu Chengula aliongeza kuwa hivi sasa jambo pungufu
analoliona ni katika shule za serikali, lakini hakuna anayekiri kuwa majengo
hayatoshi huku walimu wakiandikisha watoto wengi kuliko uwezo wa kuwamudu na
hiyo yote inafanywa kwa kuogopa kufukuzwa kazi.
"Hivi kweli mnataka mpaka serikali ije iwajengee
vyoo? Hawa ndio sawa na wauaji, ambao hawastahili kusamehewa. Hili ni tatizo,
ambalo Wakristo tunaweza kuchokoza kwa kueleza tunatakiwa tuwe na madarasa
yanayotosheleza watoto kadri ya taaluma inavyoeleza,"alisema.
Askofu Chengula alisema watoto wakiwa wengi darasani,
mwalimu anakuwa sawa na mhubiri, ambaye kawaida huwa ni vigumu na hawezi kumuuliza
swali na kuwataka Wakristo wawaombee wenzao. ambao hawafikirii kuwatengenezea
watoto mahali pazuri ili waweze kusoma.
Aliongeza kuwa kwa sasa Watanzania wengi wamekuwa
wanamshangilia Rais Dk. Magufuli kutokana na utendaji wake wa kazi hadi kufika
hatua ya kusema hatimaye Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere amefufuka na
kwamba, yote ni mema, lakini Wakristo wanatakiwa kumuombea kwani kuna maadui
wengi.
Alisema Watanzania wanatakiwa wamuombee Rais Dk.Magufuli
ili wale wabaya wake washindwe kama vile mwovu shetani alivyoshindwa na Yesu
Kristo na kisha kufufuka kutoka kwa wafu.
Aidha,aliwataka Watanzania kushirikiana kwa karibu na
serikali iliyopo madarakani ili iweze kuwatekelezea yale yote iliyowaahidi
kupitia Ilani ya Uchaguzi.
WAUMINI
SHINYANGA WAHIMIZWA
KUACHANA
NA VURUGU NA CHUKI
Mkoani
Shinyanga, Askofu Mkuu Mhashamu Liberatus Sangu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Shinyanga, amewataka waumini kuwa na upendo na kutotanguliza chuki
na vurugu kwa wengine.
Askofu huyo aliyasema hayo jana,
katika Ibada Maalumu ya Siku ya Mkesha wa Sikukuu ya Pasaka,
iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma Parokia
ya Ngokolo lililoko mjini
Shinyanga.
Alisema mwanga
huashiria upendo na giza ni mapigano, chuki na vurugu, hivyo aliwataka Wakristo
kuishi katika mwanga zaidi na kutoiga
baadhi ya maataifa ambayo kila siku wao ni giza.
“Leo ni siku ya
pekee tangu kuchaguliwa kwangu kuwa askofu mkuu jimbo la Shinyanga, ni
Pasaka ya kwanza, hivyo nawashukuru wote ila natanguliza salamu zangu kuieleza jamii waimarishe
katika amani na upendo wa pamoja katika makundi ya wafungwa, yatima na
wagonjwa,” alisema Askofu Sangu.
Askofu huyo aliwabatiza
waumini wapatao 41 na kuwapatia
kipaimara kwa ishara ya kumpokea Yesu Kristo, hivyo aliwataka kufuata matendo mema waliyokuwa wakiyafuata kwenye kipindi
kilichopita cha kwaresima na kuyaendeleza.
Paroko Msaidizi wa
kanisa hilo, Pastory Masunga, alipokuwa
akitoa salamu kwa waumini wa parokia hiyo, aliwataka wazazi pia
kuhakikisha siku ya Pasaka hawawaruhusu
watoto wao kwenda kuzurula, kwani kumepitwa na wakati na kuiheshimu familia ili kuondokana na
vitendo viovu, ikiwemo majanga kwao.
RUVUMA WATAKIWA KUWA
NA NYENDO ZA KIZALENDO
Kwenye
ibada hiyo iliyofanyika mkoani Ruvuma, Askofu wa Kanisa Katoliki
Jimbo la Mbinga, Mhashamu John Ndimbo, amewataka Watanzania kuhakikisha
wanafuata nyendo za kizalendo
anazoendelea
kuonyesha Rais DK.Magufuli kwa taifa ili wananchi waweze
kuyafikia maendeleo yanayokusudiwa kwa haraka.
Akiongea wakati wa mahubiri ya Sikukuu ya Pasaka katika
Kanisa la Mtakatifu Wilhelm mjini hapa, Askofu Ndimbo alisema kasi ya Rais Magufuli
ni mfano mzuri wa kuigwa kwani tangu aingie madarakani, Watanzania wameonyesha
kuwa na imani naye.
Alisema hali hiyo
ikiendelea, kutakuwa na mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali.
Alisema binafsi anafurahishwa na utendaji kazi wa Rais
Magufuli kutokana na ukweli kwamba, anachokifanya kitasaidia kupeleka taifa
kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi baada ya miaka mitano ijayo.
Askofu Ndimbo alisema
kinachotakiwa kwa Watanzania pamoja na kuunga mkono juhudi hizo, pia
wasisite kumwombea kwa Mungu kila mara.
“Kumbukeni vigezo vya Rais wetu Magufuli anavyovitaka
katika nchi yetu ili iweze kusonga mbele ni kuwa wazalendo kwa mali zetu kwa
manufaa ya wananchi,” alisema Ndimbo.
Askofu Ndimbo alifafanua kuwa ili Tanzania iweze kupiga
hatua za kimaendeleo haraka kulingana na rasilimali zilizopo, ni lazima kila
mmoja aweke uzalendo mbele, badala ya kutaka kujilimbikizia mali kwa watu
wachache huku walio wengi na hasa wanyonge wakiendelea kubaki masikini.
Alisema kitendo kinachofanywa na serikali ya awamu ya tano
cha kutumbua majipu ni kizuri, kwani kwa miaka mingi nchi ilikuwa ikionekana
haina uwezo wa kujiendesha yenyewe huku nyuma ya pazia kukiwa na watendaji na
viongozi wachache, ambao walikuwa wakiliingiza taifa kwenye lindi la umasikini.
Alisema watendaji hao wamekuwa wakishirikiana na
wafanyabiashara, ambao walikuwa wakwepaji wakubwa wa kulipa kodi.
Askofu Ndimbo alisema matumizi mabaya ya madaraka
yaliyokuwa yakifanywa na vigogo wa ngazi ya juu sio peke yao, bali katika
halmashauri za wilaya, miji, manispaa na hata majiji, wao vibaraka ambao
kimsingi hushirikiana na walioko wizarani kufanya hujuma, hivyo kinachotakiwa
kwa serikali ni kuhakikisha safisha safisha inahamia huko.
“Matumizi mabaya
ya madaraka tuyaache, muda mwingi tunapokuwa katika ofisi za umma tufanye kazi
kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, hali hiyo itasababisha tujijengee
historia nzuri katika maisha yetu”, alisema.
Askofu huyo aliwataka wananchi bila kujali itikadi zao
za kidini au vyama vyao, kuungana na kutekeleza maagizo yanayotolewa na Rais
kwani uzoefu wa siku chache za uongozi wake, umedhihirika wazi kwamba, kila
anachokiagiza kinalenga kuwasaidia Watanzania wote bila ubaguzi.
Alisema iwapo itaonekana kujitokeza kwa baadhi ya watu
kubeza shughuli zinazofanywa na serikali iliyopo madarakani, watapaswa
kutoungwa mkono na si vinginevyo.
Hata hivyo, alisema ili maendeleo yaweze kupatikana kwa
haraka, amani na utulivu uliopo nchini lazima uenziwe kwa kulindwa na kwamba,
pasitokee mtu au kikundi cha watu kutaka kuvuruga hali hiyo, ambayo imedumu tangu
nchi kupata uhuru wake mwaka 1961.
ASKOFU DODOMA AWAHUBIRIA
WAUMINI UMUHIMU WA UPENDO
Mkoani
Dodoma, imeelezwa kuwa kukosekana kwa hofu ya Mungu miongoni mwa watu, kumechangia
kwa kiasi kikubwa kutokuwepo kwa upendo miongoni mwa jamii.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Parish ya Mlimwa, Robert Ligolei, alipokuwa akihubiri katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka, ambapo Wakristo wanakumbuka kukufuka kwa Yesu Kristo, ambaye alikufa ili kuwakomboa binadamu.
Alisema
Wakristo wanaposherehekea sikukuu ya Pasaka, wanapaswa kukumbuka upendo mkuu
aliouonyesha Yesu Kristo katika kuwakomboa binadamu na kuitumia siku hiyo kama
fundisho.
Mchungaji huyo alisema kanisa na waumini kwa ujumla wana jukumu la kutunza na kuwalea yatima, wajane na watu wasiojiweza, hivyo katika siku hii ni wajibu wa kila mmoja kukumbuka hilo.
“Sio wewe na familia yako mnakula na kusaza bila kujua kuna watu wanauhitaji na maandiko yametuagiza kuwasaidia na kuonyesha upendo kwao ili nao wajione kama ni sehemu ya binadamu,”alisema.
Alifafanua kuwa kukosekana kwa hofu ya Mungu na kutokuwa na upendo, kumesababisha jamii kushindwa kusaidia kundi hilo lenye mahitaji.
Ligolei alisema hivi sasa kila familia kwa familia, ukoo kwa ukoo na jamii kwa ujumla, zote zimekosa upendo, hivyo kujikuta kila mmoja akiishi kivyake, tofauti na miaka iliyopita, ambapo watu walikuwa wakiishi kwa upendo, umoja na mshikamano.
Alisema kifo cha Yesu Kristo ni ukombozi na ishara ya upendo mkuu kwa binadamu na ndio mana alikubali kujitoa na kufa kifo cha aibu pale msalabani ili binadamu waweze kukombolewa.
Mchungaji huyo alisema hivi sasa jamii imetawaliwa na ubinafsi mkubwa kiasi, ambacho watu wanathubutu kuuana kwa kugombania mali na hata mambo mengine yasiyo na msingi na kusahau kuwa tayari walishapata ukombozi.
Alisema Yesu kabla ya kufa msalabani, aliagiza upendo kwa binadamu, pia aliwapenda watoto hata akasema wawaache waende kwao maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Sambamba na hilo aliwasihi kutoitumia siku hii kama siku ya kufanya uovu na kuchafua toba yote waliotubu kwa siku 40, wakati wa kipindi cha kwaresma kabla ya Pasaka.
Alisema waumini watakuwa ni watu wa ajabu kama watatumia kipindi hiki kutubu na kumuomba Mungu awasamehe, lakini wakati wa pasaka wanatumia nafasi hiyo kujipaka matope kwa madai ya kusherekea sikukuu hiyo si sawa kabisa.
No comments:
Post a Comment