Wednesday 7 October 2015

TUSIKUBALI KUTUMIWA NA WANASIASA-PENGO



NA MWANDISHI WETU
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amevishanga baadhi ya vyama vya siasa vinavyodai kuwa vitalinda kura mara baada ya kupiga kura.

Aidha, amewataka Watanzania kutokubali kutumiwa na wanasiasa wenye nia ya kutaka kuleta machafuko yasikuwa na lazima kwani, kubaki katika vituo vya kupigakura kunaweza kusababisha mtafaruku.

Pia, amesema ni uvunjifu wa sheria kwa wanasiasa kuhamasisha wananchi kukaa kwenye vituo baada ya kumaliza kupigakura na kuwashauri Watanzania kutii sheria ili Taifa liendelee kuwa na amani.

Wakati Kadinali Pengo akitoa tahadhari hiyo, Jeshi la Polisi Nchini, limesema halitaruhusu mtu au kikundi cha watu kuendelea kuwepo katika vituo vya kupigia kura kwa madai ya kulinda kura.

Akizungumza jana Dar es Salaam, katika mahojiano maalumu kuhusu masuala ya uchaguzi mkuu, Kadinali Pengo alisema ni jambo la kushangaza kwa vyama kuwataka wananchi kubaki vituoni.

“Tunafanya kila njia ili kuzuia kura zisiibwe, hii ni hali nyeti na tete na sijawahi kupata wasiwasi kama wakati huu. Wasiwasi huu unatokana na Watanzania kutafuta kitu bila kufahamu sababu za msingi za jambo wanalohitaji.

“Nawaomba Watanzania kuwa makini na wasikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa wasiokuwa na nia njema na taifa, badala yake watulie na kuwa na subira. Baada ya kumaliza kupigakura wasubiri utaratibu wa sheria uchukue mkondo wake kwa maana wahusika kutangaza matokeo,” alisema.

Alisema iwapo kutakuwa na mtu hataridhika na matokeo hayo, ni vyema kwenda kwenye vyombo husika, ikiwemo Mahakama badala ya kujaribu kutengeneza mazingira ya vurugu.

Kadinali Pengo amewataka wananchi kujiepusha kushikiana mapanga ama silaha iwapo itatokea mtu au mgombea wanayemshabikia atashindwa.

Akizungumzia madai ya kuibiwa kura, Kadinali Pengo alisema suala hilo sio zuri na kama kiongozi wa dini asingependa kusikia linatokea hapa nchini kwa kuwa mara baada ya uchaguzi mkuu, maisha ya kawaida yanaendelea.

Alisema baadhi ya watu wanasema wanataka mabadiliko na kwamba tatizo lililopo asilimia kubwa ya watu wanaosema wanataka mabadiliko, hawajui wanataka kitu gani zaidi ya kutaka chama kibadilike.

“Nimezungumza na msomi mmoja wa chuo kikuu nikamuuliza unataka mabadiliko gani, alichonijibu ni kuwa anataka mabadiliko bila ya kutaja ni mabadiliko gani, huyo ni msomi anajibu hivyo je, hawa wengine,” alihoji.

Aidha, alisema anashangazwa na kusikitishwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa ambazo zimekuwa za kuwadanganya wananchi.

“Kama wapo wanasiasa wa aina hiyo huo ni udhalilishaji wa wananchi na taifa kwa ujumla, pande zote watangulize kusema ukweli,” alisema.

Akizungumzia siku ya kupigakura kuwa Jumapili, alisema haoni kama ni tatizo kwa kuwa siku hiyo ibada zipo nyingi za kutosha na waumini wana wajibu wa kuchagua ibada ya kusali ili pia apate muda wa kupiga kura.

No comments:

Post a Comment