Wednesday 7 October 2015

IGP MANGU ATOA ONYO KWA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA



Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu, amesema hawataruhusu mtu au kikundi cha watu kuendelea kuwepo kwenye vituo vya kupigiakura baada ya kupigakura kwa madai ya kulinda kura zao ili zisiibiwe.

Amesema nafasi ya jeshi la polisi kwenye uchaguzi mkuu ujao ni kuhakikisha amani inatawala, jambo litakalosababisha uchaguzi husika kuwa wa huru na haki, hivyo hawatamvumilia yeyote atakayekaidi sheria na utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Tume (NEC) wana taratibu zao zenye lengo la kufanikisha uchaguzi mkuu kuwa huru na haki, moja ya sheria zilizoko ni mpigakura kutakiwa kuondoka kituoni baada ya kumaliza kupiga kura, kwa hiyo mtu ukibaki hata baada ya kupigakura ni kosa,” alisema.

Alisema mtu kuwepo kwenye vituo husika baada ya kupigakura kunaweza kusababisha mkusanyiko wa watu wenye lengo moja linalofanana kama wanavyoshauriwa na baadhi ya wanasiasa (kulinda kura), hatua itakayochangia uvunjifu wa amani.

“Mtu mmoja akiamua kubaki kwa madai ya kulinda kura, atashurutisha wengine, watakuwa wengi, polisi wanaweza kushindwa 'kuwacontrol’ kwa sababu miongoni mwa watu hao kila mtu ana tabia yake, matokeo ni kuvunjika kwa amani, kweli hatutaruhusu,” alisema IGP. 

Mkuu huyo wa Polisi nchini aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na wanahabari baada ya mkutano maalumu kati ya NEC na waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi majimboni na makamanda wa polisi wa mikoa yote Tanzania.

Mkutano huo ambao kwa mujibu wa NEC ni wa kihistoria kutokana na kuwakutanisha kwa mara ya kwanza wadau wote wakuu wa uchaguzi nchini, ulikuwa na madhumuni ya kuelezana namna ya kuongeza ufanisi kwenye usimamizi wa uchaguzi mkuu katika hatua zote ili uwe wa huru na haki.

Awali, katika ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema maandalizi ya uchaguzi mkuu yanaendelea vizuri, ambapo mambo mbalimbali ya msingi yanafanyika, ikiwemo kukutana na wadau, wasimamizi wakuu kutoka nchi nzima.

Alisema tofauti na wanavyosema baadhi ya wanasiasa, uchaguzi utakuwa huru na haki na utamalizika kwa amani kutokana na namna Tume ilivyojipanga kwenye kutoa haki kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu mwaka huu.

Jaji Lubuva alitilia mkazo kauli ya IGP kwa kusema kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuwataka wafuasi wao kubaki kwenye vituo vya kupigiakura kwa madai ya kulinda kura, ni cha kulaaniwa na kwamba NEC hawakibariki.

Alisema Tanzania ni kielelezo cha amani duniani kwa miaka mingi, hivyo wanasiasa wasitake kuondoa sifa hiyo kwa ajili ya manufaa yao binafsi kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa kuwashurutisha wafuasi wao kuvunja sheria, ambazo viongozi wa vyama vyote walitia saini kuzikubali kabla ya kuanza kwa kampeni.

“Amani, amani ndio tunayosisitiza, hatutaki misimamo ya Jonas Savimbi hapa kwetu Tanzania, ambaye alisema lazima mtu ukishiriki kwenye uchaguzi ushinde, usiposhinda ni lazima umeonewa au umeibiwa kura, hivyo ni wajibu wako kudai ushindi wako kwa kuingia msituni,” alisema Jaji Lubuva.

“Hakuna sababu ya watu waliokwishapiga kura kuwepo vituoni, wawakilishi wa vyama wanatosha na watakuwepo vituoni kwa mujibu wa sheria ili kutetea na kusimamia maslahi ya wapiga kura wake na chama chake, kwanini kuwepo na watu wengine kulinda kura?” Alihoji.

Aliongeza:“Wajibu wa kuhesabu kura kwa haki ni wa NEC, sasa kama kuna NEC nyingine ambayo iko ndani ya chama fulani cha siasa hatujui na hatuitambui, kwa sababu sisi ndio tunatambulika kikatiba na hatukubali yeyote aingilie majukumu yetu.”

Mara kadhaa, viongozi wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake taifa, Freeman Mbowe, walinukuliwa kwenye mikutano ya waandishi wa habari na ya kampeni za urais maeneo mbalimbali ya nchini, wakiwataka vijana wa chama hicho kutorudi nyumbani baada ya kupigakura Oktoba 25, ili kulinda kura zisiibiwe.

Kauli hizo pamoja na kupingwa vikali na wadau wa uchaguzi, wakiwemo wakurugenzi, wasimamizi na vikosi vya ulinzi na usalama kwenye vikao vya maandalizi ya uchaguzi, wananchi pia kwa nyakati tofauti wamelaani kauli hizo na kuziita za uchochezi zenye lengo la kuharibu amani iliyoko nchini.

Hivi karibuni kwenye mikutano mbalimbali ya mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, amekuwa akiwataka wafuasi wake hasa vijana kubaki vituoni mara baada ya kupigakura.

Kauli hiyo inadaiwa kuwa huenda ikasababisha hofu kwa wananchi wengine na kushindwa kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema hakuna wizi wa kura unaofanyika na kama kuna mtu ana ushahidi huo auwasilishe tume.

Jaji Lubuva aliwataka wananchi kuondoka vituoni mara
baada ya kupigakura na kwamba mwenye mamlaka ya kutangaza matokeo ni tume na sio mtu yoyote.

No comments:

Post a Comment