Wednesday, 17 August 2016

LUSINDE AMLIPUA LOWASSA

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Livingstone Lusinde, amemtaka Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kuacha upotoshaji na uzushi kwamba, wapinzani wanatoka nje kwa ajili ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson.

Lusinde, ambaye pia ni Mbunge wa Mtera, alitoa kauli hiyo jana, mjini hapa, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Morena.

Akizungumzia hoja ya wapinzani kususia vikao vya bunge na kutoka nje pindi vikao hivyo vinapoendeshwa na  Naibu Spika, alisema utaratibu huo umekuwepo hata wakati Spika Job Ndugai, akiwepo hivyo waache porojo.

Pia, alitumia nafasi hiyo kumtaka Lowassa kuacha siasa za uchonganishi huku akishauri watafakari na kuangalia sababu zilizofanya watoke nje ya bunge.

Aliwataka wabunge kutoka kambi ya upinzani kurudi bungeni kama walivyotoka, wasitafute kiki kupitia spika na kusisitiza wamuache Spika apumzike.

Lusinde alisema wabunge wa upinzani imekuwa ni tabia yao kutoka nje ya bunge hata kipindi cha Bunge la Tisa chini ya Spika mstaafu, Samuel Sitta.

Alionyesha kushangazwa na Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, kusema kuwa angekuwepo Ndugai, wasingetoka huku akisema kauli hiyo ni ya kutaka kufitinisha viongozi.

Lusinde alienda mbali zaidi akimtaka Lowassa, kukumbuka kauli iliyotolewa na wapinzani ya kudai kuwa, watazunguka na helikopta kuhakikisha Ndugai hashindi wakati akiwa naibu spika na sasa wanamuona amekuwa mzuri, mambo ambayo alisema ni ya hatari.

“Wakishaingia, wanapaswa warekebishe mtindo huo, ikiwemo kuangalia walitoka kwa masharti gani na wanarudi kwa masharti gani," alisema mbunge huyo machachari.

Akizungumzia operesheni UKUTA, aliwataka Watanzania kupuuza kelele za wapinzani kuhusu oparesheni hiyo, badala yake wamuunge mkono Rais Dk. John Magufuli, katika kazi ya kuleta maendeleo ya wananchi.

Alisema wakati wapinzani wanajipanga kuanza operesheni UKUTA, ni vyema wakatumia muda wao kujenga msingi imara, ambao utasimamisha ukuta huo huku akiwasisitiza wananchi kushirikiana katika kumuunga mkono Rais kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo.

Lusinde alisema operesheni kama hizo si jambo jipya kwa vyama vya upinzani kwa kuwa walishakuwa na operesheni Sangara, M4C na sasa wanakuja na operesheni UKUTA, ambayo kama zilizopita, pia haitabadilisha chochote.

Aliwaasa wanasiasa kutumia vizuri nafasi ya kumuona Spika kwa kumpa pole, badala ya kumpelekea mzigo wa matatizo ili ayatatue.

Katika hatua nyingine,  Lusinde alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa utekelezaji wa agizo la serikali kuhamia Dodoma kwa vitendo huku akiwataka wakazi wa Dodoma kuitumia fursa hiyo vizuri.

Alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma ulikuwepo siku nyingi na upo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, lakini Rais Dk. Magufuli amekuwa na ujasiri wa kuutekeleza kwa kutoa maagizo kupelekwa bungeni kwa muswada wa sheria ya kuitambua Dodoma kuwa makao makuu.

Mbunge huyo alibainisha kuwa fursa hiyo ni adhimu, ambayo kama wakazi wa Dodoma, ni wajibu wao kuitumia vizuri, badala ya kuhama mjini na kukimbilia vijijini.

No comments:

Post a Comment