Wednesday 17 August 2016

JPM AWAJULIA HALI NDUGAI, MALECELA


RAIS Dk. John Magufuli amewatembelea na kuwajulia hali Spika wa Bunge, Job Ndugai na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu,  John Malecela.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, jijini Dar es Salaam, ilisema pamoja na kuwajulia hali, Rais Dk. Magufuli aliyeongozana na mkewe, Mama Janeth Magufuli, aliwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone na kupata nguvu haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida katika ujenzi wa taifa.

Akizungumza na Rais Magufuli, nyumbani kwake, Salasala, jijini Dar es Salaam, Spika Ndugai alimshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kumtembelea, kumjulia hali na kufuatilia kwa karibu wakati wote alipokuwa akipata matibabu nchini India hadi aliporejea nchini.

"Kwa kweli nimefarijika sana, kwanza naomba nimshukuru sana Rais kwa sababu nilipopata matatizo haya ya maradhi, alikuwa karibu na mimi nikiwa hapa nchini na hata nilipopelekwa India. Alinipigia simu mara kwa mara na kunifariji na hapa amekuja kuniona kwa niaba ya Watanzania, kwa kweli namshukuru na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa moyo huu wa kuwajulia hali wenye matatizo," alisema Ndugai.

Aliongeza: "Niwahakikishie Watanzania kwamba, kwa sasa nina nafuu kubwa, naweza kufanya kazi nyingi tu, lakini tuendelee kuombeana."

Kwa upande wake, Mzee Malecela pamoja na kumshukuru Rais Dk. Magufuli na mkewe, Mama Janeth kwa kumtembelea, alisema afya yake inazidi kuimarika na aliwashukuru madaktari wanaompatia matibabu.

"Rais nakushukuru sana, namshukuru pia mama Janeth kwa kunitembelea na kunifariji, naendelea vizuri na matibabu na afya yangu imeimarika kwa kiasi kikubwa," alisema Malecela.

No comments:

Post a Comment