Tuesday, 16 August 2016

UVCCM KUFANYA MABADILIKO YA KIMFUMO


WAKATI Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, anajipanga kutumbua majipu ndani ya Chama hicho, Jumuia ya Umoja wa Vijana (UVCCM), imejidhatiti kufanya mabadiliko ya kimfumo.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, wakati akizungumza na waandishi wa habari,
baada ya kumalizika kwa kikao cha siku nne cha Baraza Kuu la Jumuia hiyo.

Shaka alisema UVCCM kuanzia Desemba, mwaka jana, ilianza
kujitathimini na kuweka mikakati ya kufanya mabadiliko ya kimfumo, kiutawala na kiuendeshaji ili kukidhi haja ya muda walionao katika kuiongoza taasisi hiyo kitaalamu zaidi.

Alisema aliunda kamati ndogo ndogo za kutathmini miradi yake, ambayo ilionyesha kuwepo na upotevu mkubwa wa fedha za jumuia.

Aliitaja miradi hiyo, ambayo ilionekana kuwa na harufu ya ubadhirifu kuwa ni pamoja na Kinondoni na malipo ya mafao ya watumishi (NSSF).

Pia, alisema walipitia migogoro mbalimbali inayoihusu jumuia hiyo na ucheleweshaji wa utekelezaji wa baadhi ya mikataba, ambapo ripoti za kamati hiyo zinaendelea kufanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa, hatua ya awali iliyochukuliwa na umoja huo ni kuomba kwa Katbu Mkuu wa CCM, Abdulrahmani Kinana, kuwapatia wakaguzi wa hesabu ili kukagua miradi yote ya UVCCM.

“Awamu ya kwanza ukaguzi umeanza katika miradi ya majengo ya makoa makuu Dar es Salaam, miradi ya uwekezaji wa vibanda vya kinondoni na malipo mbalimbali ya watumishi (mishahara na shughuli zote za utawala),”alisema Shaka.

Aliongeza kuwa awamu ya pili ililenga kufanya uchunguzi wa mradi wa uwekezaji darajani Zanzibar, mradi wa uwekezaji Gymkhana Zanzibar, shamba la vijana Tunguu na shamba la vijana Ihemi.

Meneo mengine yaliyofanyiwa ukaguzi ni pamoja na mkutano mkuu maalumu wa ushirikiano kati ya UVCCM na nchi rafiki, uliofanyika Arusha na miradi yote midogo midogo.

Sambamba na hilo, alisema UVCCM inaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi wake wote na mali zake ngazi Taifa hadi wilaya na baada ya kukamilika, ripoti zote zitawasilishwa kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais, Dk. John Magufuli.

No comments:

Post a Comment