Monday 15 August 2016

ABOUD JUMBE AZIKWA ZANZIBAR


RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameongoza mamia ya wananchi katika mazishi ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar awamu ya pili na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, yaliyofanyika nyumbani kwake, Migombani, Unguja.

Mwili wa marehemu uliwasili Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, asubuhi na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), akiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.

Mwili huo ulifikishwa nyumbani kwake kabla ya kupelekwa katika Msikiti wa Mwembeshauri, mjini Unguja kwa ibada.

Ibada ya kumsalia marehemu ilifanyika katika msikiti huo, ambao ujenzi wake kwa kiasi kikubwa mchango wake umetokana na marehemu katika miaka ya 1982.

Sala ya maiti iliongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Kabi, ambaye alimtaja marehemu kuwa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha amani na utulivu kwa kujenga  uvumilivu wa kisiasa.

"Waislamu tunapaswa kuiga  mfano wa marehemu Alhaji Jumbe katika kuimarisha umoja na kujenga tabia ya kuvumiliana na kuomba msamaha pale anapowakosea watu," alisema.

Safari ya mwisho ya marehemu Jumbe ilianza nyumbani kwake Migombani, ambapo alizikwa kwa heshima zote za serikali zote mbili, ambazo alizitumikia katika kipindi kirefu cha uhai wake.

Rais Dk. Shein aliongoza kuweka udongo katika kaburi la marehemu, ambalo lipo karibu na makaburi mengine manne ya watoto wake waliozikwa jirani na eneo hilo.

Alifuatiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Wengine waliopata fursa ya kuweka udongo katika kaburi la marehemu ni Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agustine Mahiga, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.

Dua ya kumuombea marehemu ilisomwa na Shekhe Mohamed Kassim kutoka katika Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana.

Msemaji wa familia, Mustafa Aboud Jumbe, alizishukuru serikali zote mbili kwa kumhudumia katika kipindi chote, ikiwemo matibabu ya nje ya nchi na ya ndani.

"Tunazishukuru serikali zote mbili kwa kumhudumia mzee katika kipindi chote cha ugonjwa wake kwa kumsafirisha nje ya nchi na kupata matibabu ya ndani ya nchi,"alisema Jumbe.

Baadhi ya viongozi walimwelezea marehemu Jumbe kuwa ni nguzo imara ya CCM kwa kuunda Chama, ambacho nguvu zake zimekuwa imara hadi leo kwa kushinda katika uchaguzi mbalimbali katika mfumo wa vyama vingi.

Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar, Dk. Shein kufuatia kifo cha Alhaji Jumbe,

Alhaji Jumbe alifariki dunia juzi, nyumbani kwake, Dar es Saalam.

Akitoa salamu hizo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema CCM Zanzibar imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kiongozi huyo, aliyetumikia taifa kwa uadilifu mkubwa na kuongoza harakati mbalimbali za ukombozi ndani na nje ya Tanzania.

Jumbe aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo Rais wa Zanzibar wa  awamu ya pili na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1974-1984).

Kufuatia kifo hicho, Vuai alisema taifa limempoteza kiongozi muhimu aliyejitolea kupigania uhuru, haki na usawa na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika vipindi vya uongozi wake.

Alisema CCM Zanzibar itaendelea kuenzi juhudi na falsafa za marehemu Jumbe, hasa katika kupigania maslahi ya Chama, bila ya kujali vikwazo na changamoto zilizojitokeza katika enzi za utawala wake.

"Hatuwezi kuizungumzia historia halisi ya vyama vya ukombozi ndani ya taifa letu, vikiwemo African Association ilipoungana na Shiraz Party na baadaye kuzaa ASP, ambapo waliungana na TANU na mwaka 1977 kuzaliwa CCM, bila ya kumtaja Alhaji Aboud Jumbe, aliyesimamia harakati hizo na kupatikana chama kimoja kilichokuwa na sera na misingi imara ya kuleta maendeleo ya nchi bila ya ubaguzi,” alifafanua Vuai.

Alisema kwa niaba ya CCM Zanzibar, anapenda kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huo.

Aboud Jumbe alizaliwa Juni 14, 1920, Mkamasini, Unguja. Alishika madaraka ya kuiongoza Zanzibar mwaka 1972, baada ya kifo cha Mzee Abeid Amani Karume, kilichotokana na kupigwa risasi, Aprili 7, 1972, Makao Makuu ya Afro Shirazi Party (sasa Ofisi Kuu ya CCM) Kisiwandui, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment